Na Mwandishi Wetu
KATIBU wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi CCM Itikadi, Uenezi na Mafunzo CPA Amoss Makalla ameshiriki kikamilifu kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika leo nchini huku akielezea kufurahishwa na hali ya amani na utulivu uliopo katika vituo vya kupiga kura.
CPA Amos Makalla, amepiga kura leo Novemba 27,2024 mapema asubuhi akiwa katika Mtaa wa TPDC Mikocheni B jijini Dar es Salaam na akiwa kituo cha kupiga kura amechagua viongozi wa serikali za mitaa ikiwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wa Serikali za Mitaa.
Akizungumza baada ya kupiga kura CPA Makalla amesema amepata fursa ya kutimiza wajibu wake wa kikatiba na kutumia haki yake ya demokrasia aliyopewa ya kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji.
“Nimefurahi utaratibu ulivyoandaliwa kwani haitaji kutumia muda mwingi kwa kuwa karatasi zimeandaliwa na majina yapo na ukiwa na kitambulisho msaidizi anakusaidia kutafuta jina lako.
“Kwa hiyo niwaombe wale ambao hawajapiga kura wawahi kuja kupiga kura kwani hii ndio nafasi yenyewe ya kutumia wajibu wetu na haki yetu kuchagua viongozi ambao siku zote tutafanya nao kazi katika mitaa, Vitongoji na Vijiji.”
Kuhusu uchaguzi unavyoendelea CPA Makalla amesema ameridhishwa na mchakato mzima wa uchaguzi huo kwani kuna amani na utulivu.”Huoni kampeni zozote,huoni sare za chama kwa maana vyama vyote vya siasa vimezingatia taratibu za kwamba wanachama wao wamekuwa watulivu.
“Nimeridhishwa na hali ya usalama na nimeendelea kupokea taarifa katika maeneo mbalimbali nchini kuwa muamko wa wananchi ni mkubwa na upigaji kura unaendelea vizuri”.