Israel yasitisha vita Lebanon na kuendelea kuishambulia Gaza – DW – 27.11.2024

Baada ya mataifa ya Marekani, Ufaransa, Israel, Lebanon, China na Australia kupongeza makubaliano hayo, sasa imekuwa zamu ya nchi kadhaa za kiarabu kuelezea namna walivyopokea vyema makubailiano hayo ya usitishwaji mapigano kati ya Israel na Hezbollah huko Lebanon.

Misri na Qatar zimeelezea matumaini yao kwamba hatua hiyo huenda ikawezesha kufikiwa kwa mpango mwingine wa kumaliza vita katika Ukanda wa Gaza. Iraq imesema inatumai kuwa makubaliano hayo yatakomesha “vurugu, uharibifu na mateso kwa watu wa Lebanon.” Ikishirikiana na Jordan wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua ili kuvimaliza pia vita vya Gaza.

Soma pia: Jeshi la Lebanon laanza kupeleka askari wake kusini mwa nchi hiyo

Wakati huo huo, Saudi Arabia imepongeza pia mpango huo wa usitishaji mapigano, ikitumai utafanikisha kulinda “uhuru na utulivu wa Lebanon na kuwawezesha raia waliokimbia kurejea kwenye makazi yao. Washirika wa Hezbollah katika eneo hilo ambao ni waasi wa Houthi wa Yemen pamoja na wanamgambo wa Kataib Hezbollah wa Iraq, wamelipongeza kundi la Hezbollah la Lebanon kwa msimamo wao thabiti.

Makubaliano hayo yaliyopongezwa pia na Iran, yanajikita kwanza katika kusitisha mapigano kwa muda wa miezi miwili na kulitaka kundi la Hezbollah kuwaondoa wapiganaji wake katika eneo la kusini mwa Lebanon, huku wanajeshi wa Israel wakirejea pia nchini mwao. Jeshi la taifa la Lebanon kwa ushirikiano na walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL ndio watakao kuwa na jukumu la kulinda usalama eneo hilo la mpakani.

Vita vyaendelea kurindima Gaza

Mashambulizi ya Israel katika eneo la Beit Lahia huko Gaza
Mashambulizi ya Israel katika eneo la Beit Lahia huko GazaPicha: AFP

Wakazi wa Gaza wanaendelea kukabiliwa na mashambulizi makubwa ya Israel ambapo mamlaka za afya eneo hilo zinazodhibitiwa na Hamas zimesema kuwa takriban watu 33 wameuawa katika kipindi cha saa 24 zilizopita, na hivyo kupelekea idadi ya waliouawa huko Gaza tangu kuanza kwa mzozo huo Oktoba 7 mwaka jana kufikia watu 44,282. Raia wa Gaza wanahisi kutelekezwa na Hezbollah kama anavyoeleza Nasser al-Majdalawi.

“Tunajihisi kukatishwa tamaa. Walisimama upande wetu, na tunawashukuru kwa hilo, lakini kila mtu alikuwa na matumaini kwamba usitishaji vita ungewezekana kwa sharti la kusitisha kwanza vita Gaza na kisha Lebanon. Hata hivyo, inaonekana wamepewa vitisho vingi na shinikizo limetolewa kwa Lebanon na kuwalazimisha kukubali kusitisha mapigano, wakitumai kwamba Israel itafanya vivyo hivyo hapa,” alisema mkazi huyo wa Gaza.

Katika hatua nyingine, Ufaransa imesema itaendelea kufanya kazi bega kwa bega na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu licha ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu  ICC  kutoa waranti wa kukamatwa kwa kiongozi huyo. Wizara ya mambo ya Nje ya Ufaransa imesema viongozi wa Israel wana kinga ya kutoshtakiwa na Mahakama hiyo kwa sababu Israel sio mwanachama wa ICC. Mapema wiki hii, Waziri mkuu wa Ufaransa Michel Barnier, alilihutubia bunge na kusisitiza kuwa Ufaransa “ingeliheshimu” majukumu yake kwa mujibu wa sheria ya kimataifa.

(Vyanzo: APE, DPAE)

 

Related Posts