Jumuiya ya NATO yaihakikishia Ukraine msaada – DW – 27.11.2024

Nchi za magharibi zimejibu kwa kujiamini jana Jumanne vitisho vya mashambulizi ya makombora na matumizi ya silaha za nyuklia vilivyotolewa na Urusi. Hii ni kufuatia shambulizi la droni la Urusi dhidi ya Ukraine lililoweka rekodi.

Nchi wanachama wajumuiya ya kujihani NATO wamesisitiza msaada wao kwa Ukraine katika mazungumzo na maafisa wa nchi hiyo, kujibu hatua ya Urusi kufanya shambulizi la majaribio la kombora la masafa ya kati wiki iliyopita. Mabalozi walioziwakilisha nchi 32 wanachama wa NATO walipewa taarifa na maafisa wa Ukraine baada ya serikali ya mjini Kiev kuitisha mkutano kati ya NATO na baraza la Ukraine, ambalo ni jukwaa la ushirikiano kati ya pando hizo mbili.

Balozi wa Ukraine katika NATO  Nataliia Galibarenko, amesema katika taarifa yake kwamba wamewasisitiza washirika wao kuwa shambulizi hilo la Urusi lilikuwa dhihirisho la wazi la matumizi ya nguvu na Urusi na juhudi ambayo haikufua dafu kuwatisha washirika.

Katibu Mkuu wa jumuiya ya kujihami NATO Mark Rutte ameuhimiza muungano huo kutoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa Ukraine, akisema jumuiya hiyo inahitaji kujitolea zaidi kuubadili mkondo wa mgogoro wa vita vya Ukraine.

Rutte aidha amesema NATO sharti iiepelekee Ukrainemifumo ya ulinzi wa anga dhidi ya makombora inayoihitaji, pamoja na kutimiza ahadi za misaada ya kijeshi zilizowahi kutolewa kwa serikali ya mjini Kiev katika mkutano wa NATO uliofanyika mjini Washington nchini Marekanii.

NATO itaendelea kuisaidia Ukraine

Jumuiya ya NATO pia imesema hatua ya Urusi kufanya shambulizi la kombora la masafa ya kati dhidi ya Ukraine wiki iliyopita haitaiuzuia kuendelea kuisaidia Ukraine.

Mabaki ya kombora lililotumiwa na Urusi kuushambulia mji wa Dnipro.
Mabaki ya kombora lililotumiwa na Urusi kuushambulia mji wa Dnipro. Picha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Maafisa wa vyeo vya juu wa jeshi la Ukraine wametoa taarifa kwa NATO kwa njia ya video katika mkutano kati ya jumuiya hiyo na baraza la Ukraine, jukwaa la mashauriano, kuhusu shambulizi la kombora la Urusi lilioulenga mji wa Dnipro.

NATO imesema kwenye taarifa kwamba shambulizi hilo lilikuwa jaribio lengine la kuwatisha wale wanaoisaidia Ukraine wakati inapojilinda yenyewe dhidi ya uchokozi usio halali wa Urusi ambao haukuchochewa na kitu chochote kile.

Soma pia: Nchi za NATO zapania kutengeneza silaha Ukraine

Jeshi la Urusi limesema kombora jipya la masafa ya kati lililovurumihshwa katika mji wa Ukraine wa Dnipro wiki iliyopita linaweza kulenga shabaha kote barani Ulaya na haliwezi kuzuiliwa na mifumo ya ulinzi wa anga dhidi ya makombora.

Wakati huo huo, mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la nchi zilizostawi kiviwanda na zinazoinuki a kwa kasi kiuchumi duniani G7 wamelaani vitisho vya Urusi katika tangazo la mwisho la pamoja mwishoni mwa mkutano wa siku mbili uliofanyika katika mji wa Fiuggi nchini Italia.  Mawaziri hao wamesema hawatavumilia vitisho vya kutumia silaha za nyuklia.

Wiki iliyopoita Urusi ilidurusu upya muongozo wake kuhusu silaha za nyuklia na kupunguza kizingiti cha matumizi yake. Sasa inachukulia uvamizi unaofanywa na nchi ambayo yenyewe haina silaha za nyuklia, lakini ambayo inaungwa mkono na kusaidiwa na mataifa yenye silaha za nyuklia, kama shambulizi la pamoja dhidi ya Urusi.

Related Posts