Kocha Kagera aibuka na Mkwasa

KOCHA wa Kagera Sugar, Melis Medo amemtaja staa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa kuwa ni kocha mwenye uwezo mkubwa wa kiufundi nchini.

Akizungumza mara baada ya mazoezi ya timu yake, Medo ambaye ana kibarua kizito cha kuinasua Kagera Sugar kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja, alisema kuwa anatambua ubora wa Mkwasa hasa katika suala la kusuka timu yenye nidhamu ya kiufundi na kiushindani. 

“Mkwasa ni mwalimu mzuri sana. Anajua kuandaa timu yenye nidhamu ya hali ya juu, na hiyo ni moja ya sifa kubwa ya kocha wa kiwango cha juu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar.

Kwa sasa, Mkwasa ni kocha wa Ngorongoro Heroes, timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20, ambao hivi karibuni walitawazwa mabingwa wa CECAFA. “Timu kama Ngorongoro Heroes inahitaji kocha mwenye uzoefu na maono. Mafanikio yao CECAFA yameonyesha kuwa Mkwasa ni mtu sahihi kwa kazi hiyo. Anaweza kuongoza timu kwa kujiamini, na ni wazi kuwa ana uwezo wa kupambana hata kwenye michuano mikubwa kama Afcon U-20,”aliongeza Medo.

Ngorongoro Heroes, chini ya Mkwasa, watashiriki Afcon U-20 mwakani. Kwa upande mwingine, Kagera Sugar ambao wapo nafasi ya 14 na pointi nane,  wanakabiliwa na mchuano mkali wa kuwania nafasi salama kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, huku Medo akiahidi kupambana.

“Changamoto zipo, lakini tutapambana. Kagera Sugar ni timu yenye historia, na hatutakubali kushuka daraja. Mafanikio yetu yatategemea nidhamu, bidii, na umoja wa timu,” alisema Medo wakati akizungumza na gazeti hili.

Related Posts