ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, ameendelea kuonyesha umahiri wake wa kiufundi Ukanda wa Afrika Mashariki akiwa na Rayon Sports ya Rwanda.
Kocha huyo amekuwa na mwanzo mzuri wa msimu, akiiongoza timu hiyo kuvuna pointi 23 katika mechi tisa za Ligi Kuu Rwanda ikishinda saba na sare mbili. Chini ya uongozi wake, Rayon imefunga mabao 14 huku ikiruhusu mawili tu, ikionyesha timu hiyo ina ukuta imara na safu bora ya ushambuliaji.
Robertinho aliachana na Simba Novemba 2023, akajiunga na Rayon Sports Julai 2024.
Akiwa Simba kuanzia Januari 2023 hadi Novemba 2023, kocha huyo raia wa Brazil aliiongoza timu hiyo kushinda mechi 29 na kupoteza moja pekee dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga.
Akizungumzia mwanzo wake wa msimu akiwa na Rayon Sports, Robertinho alisema: “Ninafurahia jinsi timu inavyocheza. Tumejipanga vizuri na wachezaji wangu wanaonyesha bidii kubwa. Tunataka kuhakikisha tunashinda kila mechi na kudumisha mwenendo huu.”