Mahakama yaelezwa magunia 10 ya bangi yalivyosafirishwa, kuuzwa Dar

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imelezwa jinsi dereva, Peter Mdegela alivyokutwa na magunia 10 ya bangi ndani ya gari aina ya Toyota Prado ambayo ni ya bosi wake.

Mdegela ambaye ni mkazi wa Sinza na mwenzake Ally Seif Mayumba (40) mkazi wa Kiwalani Dar es Salaam, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 4/20218 yenye shitaka moja la kusafirisha kilo 194. 46 za dawa za kulevya aina ya bangi iliyokuwa katika magunia 10.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo, Septemba 7, 2017 Mtaa wa Tarangire uliopo Mbezi Beach wilayani Kinondoni.

Akiwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo  jana Novemba 26, 2024 Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele amedai kuwa, Mdegela alichukua bangi hiyo kutoka mkoani Morogoro na kuileta Dar es Salaam kisha kumuuzia Mayumba gunia moja kwa Sh500,000.

Ameeleza kuwa, Mdegela aliyekuwa dereva wa mfanyabiashara Pratap Kushal ambaye ni raia wa India, aliachiwa gari hilo alitunze baada ya bosi huyo kuhamishia biashara zake nje ya nchi na wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka, Kushil anaporudi nchini na huendeshwa na mshtakiwa huyo.

Wakili Mwakamele amewasomea maelezo yao, baada ya upelelezi wa shauri hilo kukamilika na upande wa mashitaka kuwasilisha nyaraka muhimu Mahakama Kuu.

Amebainisha kuwa, upande wa mashitaka unatarajia kuwa na mashahidi 11 na vielelezo sita ikiwamo maelezo ya onyo ya washtakiwa hao, hati ya upekuzi, hati ya ukamataji mali, ripoti ya uchunguzi kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, magunia 10 ya bangi, gari aina ya Prado lenye namba za usajili T664 AVJ ikiwa na funguo zake pamoja na ripoti ya uchunguzi wa vyombo vya moto.

Mwakamele amesema mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao, Mahakama Kuu, Kitengo cha Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.

Akiwasomea maelezo ya mashahidi, wakili Mwakamele amedai, Septemba , 2017 Mkaguzi wa Polisi, Ezekiel Kyoga akiwa Kituo cha Polisi Kawe, alipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa nyumba namba 22 iliyopo Mtaa wa Tarangire eneo la Mbezi Beach imeegeshwa  gari ambayo imebeba dawa za kulevya aina ya bangi.

Amedai baada ya kupata taarifa hiyo, alikwenda katika nyumba akiwa na viongozi wa Serikali ya mtaa huo na walipofika katika nyumba hiyo walimkuta mtu aitwaye Tausi Nungu na walimwambia awaonyeshe mmiliki wa gari hilo aina ya Toyota Prado rangi ya Silver lililokuwa limebeba magunia 10 ya bangi likiwa ndani (uani) katika nyumba hiyo.

 “Inspekta Ezekiel alimuelekeza Tausi ampigie simu mwenye gari hilo na alipompigia, Tausi alidai kuwa anataka kulala hivyo anaomba aje atoe gari yake katika sehemu ya kuegeshea magari ndani ya nyumba hiyo, ombi ambalo Mdegele alikubali na kuja katika nyumba ya Tausi na alipofika alikamatwa na polisi na kuwekwa chini ya ulinzi,” amesema.

Wakili Mwakamele amedai kuwa, baada ya kuhojiwa kwa kina, Mdegela alidai kuwa bangi iliyopo katika gari hilo aliitoa Morogoro kwa mtu aitwaye Master na alikuwa anatarajia kuipeleka usiku Kiwalani kwa Mayumba kwa ajili ya kumuuzia.

Baada ya mahojiano hayo, gari hilo pamoja magunia hayo yalipelekwa Kituo cha Polisi Mbweni kwa ajili ya kuhifadhiwa.

Amedai kuwa, siku hiyo saa 5:50 usiku, Kyoga akiongozana na Mdegela walienda Kiwalani nyumbani kwa Mayumba, ambako bangi hizo alikuwa akipeleka kuuza.

“Hata hivyo, walipofika kwa Mayumba, hawakukuta bangi hiyo kwa kuwa Mayumba alikuwa ameshauza,” amedai Mwakamele.

Akihojiwa mahakamani hapo, Mayumba amedai kuwa, amekuwa akinunua bangi kutoka kwa Mdegela kwa Sh500,000 kwa gunia moja na yeye huenda kuuza bangi hiyo kwa Sh750,000 kwa gunia moja.

Mshtakiwa Mayumba baada ya kukamatwa alipelekwa kituo cha Polisi Kawe kwa ajili ya mahojiano zaidi na maeneo mengine.

Katika ushahidi wake Tausi, amedai kuwa Julai 7, 2017 saa moja asubuhi alipigiwa siku na Mdegela akisema ataacha gari yake kwa Tausi,  lakini ilipofika saa moja jioni walifika watu wakiwa na kiongozi wa mtaa huo na kumuuliza gari lililoegeshwa ndani ya nyumba hiyo ni la nani, aliwajibu ni la Mdegela.

Shahidi mwingine katika kesi hiyo, Edith Malali kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), amedai kuwa alipokea barua kutoka Jeshi la Polisi ikimtaka afanyie uchunguzi gari hilo kujua mmliki wake na baada ya kufanya uchunguzi ilibainika mmliki wa gari hilo ni Pratap Kushal ambaye ni raia wa India.

Katika maelezo ya onyo yaliyosomwa na wakili Mwakamele, imedaiwa kuwa Mayumba alikutana kwa mara ya kwanza na Mdegela Agosti 2017 eneo la Tazara Dar es Salaam, baada ya gari la Mdegela kuharibika.

Wakiwa katika maongezi ndipo Mdegela alimuulizia Mayumba kama anaweza kupata vijana watakaoweza kuuza bangi kwa njia ya siri.

Mayumba alimjibu kuwa anaweza kufanya biashara hiyo, hivyo aliomba ampelekee gunia mbili kwa gharama ya Sh500,000 kwa kila gunia na Septemba 3, 2017 Mdegela alipeleka magunia mawili ya bangi kama alivyoelekezwa.

Pia, Septemba 7, 2017 Mdegela alimpelekea tena magunia mawili ya bangi na kulipwa Sh1 milioni na kwamba Mayumba alikuwa akiyauza kwa Sh750,000 kwa kila gunia.

Katika maelezo ya onyo ya Mdegela, imedaiwa kuwa, alikuja Dar es Salaam miaka mingi iliyopita na kufikia Tabata kuanza kazi ya kuchunga ng’ombe.

Baadaye aliacha kazi hiyo na baadaye aliajiriwa kama dereva katika moja ya kampuni za simu za mikononi na akawa anamwendesha mmoja ya viongozi wa kampuni hiyo.

Alianza biashara ya bangi kwa kununua magunia sita akiyatoa Morogoro na kuja Dar es Salaam, akiendelea na biashara hiyo kwa kutumia gari la bosi wake.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini anayesikiliza kesi hiyo, amesema kwa mamlaka aliyonayo ameihamishia kesi hiyo Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu uchumi na Makosa ya Rushwa kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi wa mashihidi wa upande wa mashitaka.

Mshtakiwa amerudishwa rumande hadi atakapopangiwa na Msajili wa Mahakama Kuu, tarehe ya kuanza kusikiliza kesi hiyo.

Related Posts