Mawakala CCM, Chadema wakimbia na maboksi ya kura Nzega

Tabora. Mawakala wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Bukene na Wakala wa Chama Cha mapinduzi (CCM) Jimbo la Nzega vijijini, wamekimbia na maboksi ya kupigia kura baada ya wagombea wao kuzidiwa kura kwenye uchaguzi waliokuwa wanausimamia.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Novemba 27, 2024 msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Nzega na Bukene, Modest Apolinary amesema matukio hayo yametokea kwenye majimbo yote mawili ya Nzega vijijini na Bukene.

“Kuna wakala wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoka kituo cha Igusule, kijiji cha Sojo, kitongoji cha Mboya jimbo la Bukene wakati wa kuhesabu kura alipoona mgombea wake hajashinda uchaguzi aliamua kukimbia na boksi mojawapo la kupigia kura, ambapo baada ya hapo wakala huyo alikimbizwa na kukamatwa hivi tunavyozungumza anashikiliwa Polisi.”

Apolinary ameongeza kuwa: “Kwenye kituo cha Malilita, Kata ya Wela Jimbo la Nzega vijijini, wakala wa CCM naye baada mgombea aliyekuwa akimwakilisha alipoona ameshindwa kura na tumeshamaliza kuhesabu, akaamua kukimbia na boksi za kura naye tulimkimbiza na kufanikiwa kumkamata, hivyo anashikiliwa na Polisi,” amesema

Hata hivyo Apolinary amesema pamoja na mawakala hao kuondoka na maboksi ya kupigia kura, hakuna mabadiliko yoyote yaliyoathiri uchaguzi kwenye maeneo hayo.

Related Posts