Mgombea Chadema Dar adaiwa kuuawa, Polisi yasema amefariki kwa ‘Presha’

Dar es Salaam. Wakati Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe akidai mgombea ujumbe wa chama chake Mtaa wa Ulongoni A, Modestus Timbisimilwa kuwa ameuawa kwa kupigwa risasi na Polisi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema amefariki kwa shinikizo la damu.

Katika chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii leo Novemba 27, 2024 Mbowe ameandika: “Tunapofunga vituo vya kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, Taifa limeendelea kushuhudia tena ubaradhuli wa wazi na wa aibu toka kwa mamlaka zote za Serikali kushirikiana kuipatia CCM na wagombea wake ushindi wa aibu hata kwa gharama za maisha ya Watanzania.

“Tunalaani mauaji na kujeruhiwa kwa wagombea, viongozi na wanachama wetu mbalimbali wakiwemo: Modestus Timbisimilwa, mgombea nafasi ya ujumbe wa serikali ya mtaa wa Ulongoni A, Kata ya Gongolamboto, Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam aliyeuwawa na askari kwa kupigwa risasi wakati wa purukushani za kuzuia kura bandia na batili kuingizwa kituo cha kupiga kura.”

Alipoulizwa Kamanda Muliro kuhusu tukio hilo pamoja na matukio mengine amesema mgombea huyo amefariki kwa kuugua presha na kinachosambazwa mitandaoni hakina ukweli.

“Ukweli ni kwamba hakuna kitu kama hicho, tofauti na inavyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, alikuwa anaumwa presha, amekufa na ufafanuzi utatolewa,” amesema

Katika maelezo yake Muliro amesema mtu huyo alikuwa na rekodi ya ugonjwa wa presha na baada ya kwenda katika kituo hicho alikuwa anaomba maji kwa wafuasi wa Chadema.

“Watu wa Chadema walishauri asipewe maji isipokuwa awahishwe zahanati baada kufikishwa akawa amefariki dunia na amekuwa na rekodi ya kuwa na ugonjwa wa presha,” amedai Muliro.

Muliro amesema ni kweli marehemu huyo alikuwa anagombea nafasi ya ujumbe, Mtaa wa Ulongoni A na taarifa zaidi itatolewa na Msemaji wa Polisi, David Misime.

Related Posts