Mgombea wa Chadema auawa, askari Magereza mbaroni

Dar es Salaam. Mgombea uenyekiti wa Kitongoji cha Stand katika Jimbo la Manyoni Mashariki mkoani Singida kwa tiketi ya Chadema, George Mohamedi ameuawa kwa kupigwa risasi.

Awali, taarifa ya Chadema imedai kuwa Mohamedi aliuawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake baada ya kuvamiwa na watu wanaodaiwa ni makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Alivamiwa nyumbani kwake na watu waliofahamika kuwa makada wa CCM ndipo ukatokea mzozo mkubwa, Polisi walifika nyumbani kwake na kumpiga risasi ndugu George Juma Mohamed na kufariki dunia,” imesema taarifa ya Chadema ya leo Novemba 27, 2024.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limesema kuwa linamshikilia askari mmoja wa Jeshi la Magereza kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mgombea huyo kilichotokea Novemba 26, 2024 saa 5.00 usiku.

Taarifa hiyo ya Polisi imesema; “Chanzo cha tukio hilo ni kwamba katika eneo hilo wafuasi wa CCM walikuwa kwenye kikao cha ndani katika nyumba moja.

“Wakati kikao hicho kikiendelea walivamiwa na kundi la wafuasi wa Chadema na vurugu kutokea, ambapo askari Magereza ambao wapo kwenye moja ya Gereza lililopo jirani na eneo hilo walitaarifiwa na haraka wakafika eneo hilo kuona hali ilivyo.

 “Wakati askari hao wanakwenda kwenye eneo hilo waliwasiliana na polisi, walipofika eneo la tukio walianza kushambuliwa kwa mawe jambo lililowalazimu kupiga risasi hewani kutuliza purukushani hizo na risasi moja ilimjeruhi Mohamedi (41), ambaye alikuwa mgombea wa kitongoji cha Stendi kupitia Chadema.”

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts