Mtihani wa kwanza kwa Nswanzurimo Singida BS

KIKOSI cha Singida Black Stars kesho kitakuwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kupambana dhidi ya Azam FC, huku kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Ramadhan Nswanzurimo akianza kibarua cha kwanza.

Nswanzurimo alitangazwa Novemba 25 mwaka huu kuiongoza timu hiyo baada ya Kocha Mkuu, Patrick Aussems na msaidizi wake Denis Kitambi kusimamishwa kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo ambayo kikosi hicho imeyapata katika mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu Bara.

Hatua ya kusimamishwa kwa Aussems na kibarua chake kupewa Nswanzurimo ni kutokana na timu hiyo kutoka sare ya mabao 2-2, dhidi ya Tabora United Novemba 25 mwaka huu na kukifanya kikosi hicho kufikisha michezo mitatu mfululizo bila ya kupata ushindi.

Hadi Aussems anasimamishwa alikuwa ameiongoza Singida Black Stars katika jumla ya michezo 11 ya Ligi Kuu Bara, kati ya hiyo alishinda saba, sare mitatu na kupoteza mmoja, kikosi hicho kipo nafasi ya nne kwenye msimamo na pointi zake 24.

Nswanzurimo ana kibarua kigumu cha kuhakikisha kikosi hicho kinapata ushindi, huku akiwa na kazi kubwa ya kufanya kwani Azam hadi sasa ni timu ambayo imekuwa katika kiwango kizuri, ikiwa imeshinda michezo mitano mfululizo ya Ligi Kuu Bara.

Azam FC ipo nafasi ya pili na pointi 24 nyuma ya vinara Simba yenye 28, huku kwa upande wa Singida Black Stars ikishika nafasi ya nne na pointi 24 sawa na kikosi hicho cha matajiri wa Dar es Salaam ila zikitofautiana tu mabao ya kufunga na kufungwa.

Tangu Kocha Mkuu, Rachid Taoussi ateuliwe kukiongoza kikosi cha Azam Septemba 7, mwaka huu akichukua nafasi ya Msenegali, Yousouph Dabo, ameiongoza timu hiyo katika michezo 10 ya Ligi Kuu Bara ambapo ameshinda saba, sare miwili na kupoteza mmoja.

Kiujumla Azam FC imecheza michezo 11 ya Ligi Kuu Bara msimu huu, ikishinda saba, sare mitatu na kupoteza mmoja tu hadi sasa, ambapo kikosi hicho kimefunga jumla ya mabao 14 na kuruhusu matatu jambo ambalo linasubiriwa kuona kesho itakuwaje.

Timu hizi zinakutana zikiwa na changamoto mbalimbali ambapo licha ya mwenendo mzuri wa matokeo kwa Azam FC ila imekuwa na shida kwa upande wa washambuliaji tofauti na wapinzani wao Singida ambayo imekuwa angalau tishio kwenye eneo hilo.

Katika michezo 11 iliyocheza, Azam FC imefunga mabao 14 na kati ya hayo Nassor Saadun anayo matatu akiongoza kikosini hapo huku kwa upande wa Singida Black Stars kinara wao ni Mkenya, Elvis Rupia aliyefunga manne.

Nyota wengine wa Azam waliofunga ni Lusajo Mwaikenda, Idd Seleman ‘Nado’, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Gibril Sillah wenye mabao mawili kila mmoja wao, huku kwa upande wa Singida Black Stars mbali na Rupia ila anayefuatia ni Marouf Tchakei mwenye matatu.

Bato nyingine itakuwa ni kwa makipa ambapo Metacha Mnata wa Singida Black Stars ana ‘Clean Sheets’ sita hadi sasa huku kwa upande wa Mohamed Mustafa wa Azam akiwa nazo tano, jambo linaloongeza mvuto wakati timu hizo zitakapokutana kesho saa 1:00 usiku.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Nswanzurimo alisema hakuna kitu kikubwa kitakachobadilika katika timu hiyo, huku akieleza itakuwa mechi ngumu kutokana na ubora wa wapinzani wao, ingawa wamejipanga kimwili na kiakili kukabiliana nao.

“Hakuna mchezo mwepesi msimu huu kwa sababu kila timu imejipanga vizuri, jambo kubwa na muhimu ni kuhakikisha wachezaji wote wako katika morali nzuri ya kupigania ushindi, tumekuwa na muda mfupi hivyo, tusitegemee sana mabadiliko makubwa,” alisema.

Kwa upande wa Kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi, alisema wamekuwa na muda mzuri tangu mchezo wa mwisho dhidi ya Kagera Sugar walioshinda bao 1-0, huku akiweka wazi changamoto kubwa imekuwa eneo lao la umaliziaji.

“Tunatengeneza nafasi nyingi ila tumekuwa tukishindwa kuzitumia ipasavyo ingawa jambo muhimu tumekuwa tukipata pointi tatu, sio kila mchezo tutaweza kufanikisha hilo hivyo, hii ni ishara ya kutujenga ili kuendeleza ubora wetu msimu huu,” alisema.

Related Posts