Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa umma akiwemo Profesa David Mwakyusa aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).
Hayo yameelezwa leo Jumatano Novemba 27, 2024 katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga.
Mwakyusa aliyewahi kuwa Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii katika kipindi cha mwaka 2005 hadi 2010 na Mbunge wa Rungwe Magharibi (CCM), ni daktari wa tiba, mwanasiasa na mwanataaluma.
Taarifa hiyo pia imeeleza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) mstaafu, Said Mwema ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania (TSN), akichukua nafasi ya Hab Mkwizu anayemaliza muda wake.
Katika uteuzi huo, amemteua pia Mhandisi Mussa Natty kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB).
Natty ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali ikiwemo Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na Mkurugenzi wa Mji wa Babati mkoani Manyara, anachukua nafasi ya, Joseph Haule aliyemaliza muda wake.