Sheria ya madini kuchochea uchumi Zanzibar

Unguja. Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar, imeanza maandalizi ya sheria mpya ya madini ikiwa ni mkakati wa kusimamia rasilimali zake kwa uwazi na kuhakikisha zina mchango wa moja kwa moja kwenye kwenye uchumi wa Taifa.

Kwa sasa Zanzibar haina sheria ya madini, badala yake inatumia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2015 ambayo ipo chini Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Mkurugenzi wa Nishati na Madini, Said Haji Mdungi ametoa kauli hiyo leo Novemba 27, 2024 alipofungua mafunzo ya siku moja kwa wakuu wa wilaya na viongozi wa halmashauri na manispaa.

Amesema wizara imeona ipo haja ya kuwepo sheria hiyo kwani hivi karibuni kumefanyika utafiti na kuonekana kuwa Zanzibar kuna baadhi ya madini chini ya ardhi.

“Sheria hiyo inakwenda kutoa nafasi ya kuona namna gani madini na rasilimali nyingine zinapata sheria inayojitegemea katika sekta hiyo, hivyo amewaomba viongozi kuwa weledi katika jambo hilo,” amesema.

Amesema: “Kiuhalisia kwa sasa lazima kupatikana sheria ya madini hapa Zanzibar na sheria hiyo lazima iwashirikishe wadau wake wote kabla ya kutungwa ili watoe maoni,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, sheria hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini kwa kudhibiti uchimbaji, usafirishaji na utoroshaji wa madini, na kuhamasisha uongezaji wa thamani ya madini kabla ya kusafirishwa nje.

“Sisi wasimamizi tumejipanga kuendana na kasi ya maendeleo ya Serikali ya awamu ya nane katika kuwaletea maendeleo wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” amesema.

Amesema ili kufikia mafanikio ya kulinda rasilimali zisizorejesheka ni lazima wakuu wa wilaya na viongozi wa halmashauri kuwa kitu kimoja katika kuzisimamia rasilimali hizo.

Akitoa mada katika mafunzo hayo, mwanasheria kutoka wizara hiyo, Hakimu Mohammed Ame amesema suala la uchimbaji rasilimali zisizorejesheka ni mtambuka kila mtu anahusika nalo, hivyo ni vyema kwa viongozi hao kwenda kuwaelimisha wananchi juu ya kulinda rasilimali hizo.

“Tunafahamu kwa mujibu wa sheria na Katiba wakuu wa wilaya ndio wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama katika kamati zenu za wilaya, kwa maana hiyo mna wajibu wa moja kwa moja kusimamia jambo hilo katika wilaya zenu,” amesema.

Amesema sheria zilizopo kwa sasa zimeshapitwa na wakati lakini mpango wa kuzibadilisha unafanyika ili kuendana na wakati uliopo kwa sasa.

Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Othman Ali Maulid amesema watakuwa mabalozi wazuri katika kuwaelimisha wananchi na kusimamia ipasavyo sheria zilizopo na zitakazotungwa.

Mkuu wa Wilaya wa Kaskazini A, Rashid Simai Msaraka amesema anaamini rasilimali hizo ni muhimu, hivyo ataendelea kukaa na vijana kuwaeleza kwani wao ndio walengwa wakuu.

Related Posts