Simanjiro wazungumzia hali ya upigaji wa kura uchaguzi

 Mirerani. Wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wamejitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika leo, Jumatano, Novemba 27, 2024, kote nchini.

Halima Ramadhan (67), mkazi wa Kitongoji cha Msikitini, amesema huu ni uchaguzi wake wa kumi kushiriki tangu aanze kupiga kura mwaka 1975.

“Nimejitokeza kutimiza haki yangu ya kikatiba kwa kumchagua kiongozi ninayemtaka, na nawahamasisha waliojiandikisha kujitokeza kupiga kura,” amesema Halima.

Happy Urassa, mkazi mwingine wa eneo hilo, alieleza kuwa amefurahishwa na utaratibu wa kupiga kura.

“Nimekagua jina na namba yangu kwenye orodha kisha kupiga kura yangu. Utaratibu ni mzuri na unatoa fursa ya kuchagua kiongozi unayemwamini,” amesema.

Mgombea uenyekiti wa Kitongoji cha Msikitini kupitia CCM, Singo Mweta amesema maandalizi yamefanyika vizuri na watu wanashiriki kwa utulivu.

“Namshukuru Mungu kwa amani tuliyo nayo. Watu wamejitokeza kwa wingi na kila mmoja ana fursa ya kumchagua kiongozi anayemtaka,” amesema Mweta.

Mgombea wa Chadema katika kitongoji hicho, Goodlife Sumary amesema zoezi limeanza vyema. “Hakuna changamoto yoyote hadi sasa. Majina yamebandikwa wazi na kila mtu anaweza kuyakagua kabla ya kupiga kura,” amesema Sumary.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Raphael Lulandala, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Wilaya amehimiza wananchi kujitokeza kwa wingi.

“Nawahamasisha watu wapige kura mapema ili jioni wapate nafasi ya kutazama mechi ya timu ya Simba inayoiwakilisha nchi katika mashindano ya Afrika,” amesema.

Related Posts