Simba yaichapa Bravos Kwa Mkapa

Simba imeendelea kuwa na matokeo mazuri mfululizo baada ya kuichapa FC Bravos do Maquis ya Angola bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi A katika Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa jioni ya leo Novemba 27, 2024 Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Bao la ushindi la Simba limepatikana dakika ya 27 kupitia kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua akifunga kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa Bravos kushika mpira wakati akipambana kuzima shambulizi la wekundu hao.

Kipindi cha kwanza Simba ingeweza kutoka na uongozi wa mabao zaidi ya moja kama wachezaji wake wangekuwa makini kutumia nafasi walizotengeneza.

Nafasi mbili za Ahoua dakika ya tisa na 11 lakini pia Kibu Denis dakika ya 16 ambayo kipa wa Bravos alicheza ziliinyima Simba mabao ikifanya mashambulizi makali kwenye lango la wageni wao.

Bravos haikuwa na nguvu kubwa ya kutengeneza mashambulizi kipindi cha kwanza ikifika mara mbili pekee kwenye lango la wenyeji lakini mashambulizi yao hayakuwa na nguvu na kufanya mchezo huo kwenda mapumziko Simba ikiongoza kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili Bravos ilirudi na gia kubwa na kutengeneza mashambulizi makali kwa Simba ikiwaweka wenyeji kwenye wakati mgumu.

Presha hiyo ya Bravos ikawapa penalti dakika ya 47 baada ya kiungo wao, Emmanuel Edmond kukwatuliwa ndani ya eneo la hatari na mwamuzi Murtaz Ibrahim kutoka Libya kutoa adhabu hiyo ya pili kwenye mchezo huo.

Hata hivyo penalti hiyo ikapigwa na huyohuyo Emmanuel Edmond ambapo kipa wa Simba, Moussa Camara akaudaka mpira na kuiweka timu yake salama.

Licha ya mabadiliko manne ya Simba kipindi cha pili ikiwaingiza viungo Edwin Balua, Deborah Mavambo, Mzamiru Yassin na mshambuliaji Leonel Ateba lakini bado Bravos ilikuwa na nguvu kwenye mashambulizi yao huku wekundu hao wakipoteza umakini kwenye mashambulizi yao.

Simba katika ushindi huo kazi kubwa ilifanywa na kipa wao Camara ambaye alikuwa imara langoni kuifanya kazi yake ipasavyo akizima mashambulizi manne ya wazi ambayo Bravos iliyatengeneza.

Ushindi huo umeiweka Simba katika nafasi nzuri baada ya kuanza na ushindi nyumbani ambapo mchezo unaofuatia ni ugenini Desemba 8 mwaka huu dhidi ya CS Costantine utakaochezwa nchini Algeria na kukaa kileleni mwa Kundi A kabla ya mchezo wa baadaye saa 1 usiku utakaozikutanisha CS Sfaxien dhidi ya CS Constantine.

Hata hivyo, ushindi huu ni wa sita mfulululizo kwa Simba katika mashindano tofauti msimu huu huku ikiwa haijaruhusu nyavu zake kutikiswa yenyewe ikifunga jumla ya mabao kumi.

Simba tangu mara ya mwisho ipoteze mchezo wa Ligi Kuu Bara Oktoba 19 mwaka huu kwa kufungwa bao 1-0 na Yanga, michezo sita iliyofuatia imeshinda yote ambapo mitano Ligi Kuu Bara na mmoja Kombe la Shirikisho Afrika.

Related Posts