Tanga wachekelea kuongezeka vituo vya kupigia kura, wakwepa foleni

Tanga. Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Tanga wameipongeza Serikali kwa kuongeza idadi ya vituo vya kupigia kura, wakisema hatua hiyo imewarahisishia kushiriki uchaguzi bila kuathiri shughuli zao za kila siku.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatano Novemba 27, 2024 wakiwa kwenye vituo vya kupigia kura, wananchi hao wamesema ongezeko la vituo limepunguza msongamano, na kuwapa nafasi ya kupiga kura kwa haraka.

Mkazi wa Raskazone, Aminael Paulo amesema amefika kituoni saa mbili kasoro asubuhi na amepiga kura kwa haraka na kuondoka.

“Mimi ni mjasiriamali ninafanya soko la Mgandini. Nimeamka mapema kutimiza haki yangu ya kupiga kura na sasa naendelea na shughuli zangu. Hakukua na foleni kituoni kwetu licha ya watu wengi kujitokeza, hili ongezeko la vituo limesaidia sana kupunguza msongamano,” amesema Aminael.

Naye Shabani Kigoda mgombea wa ujumbe wa mtaa wa Raskazone, amesema utaratibu wa upigaji kura kwa uchaguzi wa mwaka huu  umeboreshwa zaidi ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Amesema vituo vingi vimewekwa maeneo yanayofikika kwa urahisi na viko viwili au vitatu katika eneo moja.

“Hali hii imewasaidia hata wale wenye shughuli nyingi kufika haraka na kupiga kura bila changamoto,” amesema Kigoda.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amesema mkoa huo uliongeza vituo vya kupigia kura kutoka zaidi ya 4,000 hadi kufikia 5,405 ili kuwahudumia wananchi vyema.

Amesema kazi ya upigaji kura bado inaendelea kwa utaratibu mzuri huku akihimiza wananchi kuendelea kujitokeza kwa kuwa vituo vinafungwa saa 10 jioni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi akizungumzia hali ya usalama amesema umeimarishwa kwenye vituo vyote vya kupigia kura, huku akionya mtu asithubutu kuleta vurugu kwa sababu hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayejaribu kuvunja amani.

Mkoa wa Tanga una vijiji 763, vitongoji 4,528, na mitaa 270, ambapo wagombea wa vyama mbalimbali wanashindania nafasi za uongozi kwenye uchaguzi huu.

Related Posts