Dar/ Moshi. Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu, aliyekuwa Waziri wa Afya na Dk Faustine Ndugulile akiwa naibu wake amesema Tanzania na Afrika kwa ujumla imepoteza.
Dk Ndugulile (55), aliyekuwa mbunge wa Kigamboni, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameeleza hayo katika taarifa.
“Alivyonieleza anataka kugombea nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, sikujiuliza maswali mara mbili, nilimwambia sawa. Tuliomba ridhaa ya Rais (Samia Suluhu Hassan) akaridhia, tulianza kampeni. Sikujiuliza mara mbili sababu ni daktari mwenye uwezo, ujuzi na weledi mkubwa katika masuala ya afya ya binadamu na afya ya jamii kwa ujumla,” amesema Ummy akizungumza na Mwananchi leo Novemba 27.
Amesema amefanya kazi kwa karibu na Dk Ndugulile akiwa naibu waziri wake akieleza: “Ni mtu mwenye hekima na unyenyekevu, alinipenda tulifanya kazi kwa wema, upendo na heshima kama waziri wake, nilikuwa namshirikisha mambo mengi.”
Ummy amesema aliwaambia wataalamu wizarani kwamba, naibu waziri ni waziri hivyo: “Sipendi kitu mimi waziri nijue naibu waziri asijue, kwa hivyo tuliwejenga hivyo watu wizarani.”
“Tumefanya mambo mengi mazuri, katika sekta ya afya kuanzia mwaka 2017 mpaka 2020 kuna mchango mkubwa wa Dk Ndugulile,” amesema.
Amesema Dk Ndugulile alikuwa anataka kufanya kazi nzuri Afrika kwa sababu sekta ya afya anaijua.
“Katika kampeni zake alisema kwanza mimi ni daktari mtaalamu, pili mimi ni mbunge najua wananchi wanataka nini, niko kwenye Bunge naweza kushawishi na tatu nimeshawahi kuwa waziri,” amesema.
Ummy amesema alikuwa akisubiri aone utekelezaji wa mipango na mikakati yake katika kufikia afya kwa wote barani Afrika.
“Sina cha kusema zaidi, Nimeumia kwa kweli tumepoteza sana,” amesema.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema amepokea taarifa za kifo cha Dk Ndugulile kwa masikitiko, kwa kuwa ni cha ghafla, hawakuwahi kujua kwamba ni mgonjwa au amelazwa.
“Dk Ndugulile alijiendeleza kwa kusoma na kupata shahada ya udaktari. Ametumika katika kazi zote za udaktari nchini; ametibu wagonjwa, ameshiriki utungaji wa sera na miongozo ndani na nje ya Tanzania akiwa daktari wa afya ya jamii, shahada aliyosomea Afrika Kusini,” amesema.
“Alichagua kuwa mtaalamu wa afya ya jamii katika ubobebzi, ametumika katika uongozi wa siasa za nchi hii kama mbunge wa kuteuliwa, ametumika katika naibu waziri wa afya, tumeshuhudia akigombea nafasi WHO tulikuwa na matarajio makubwa. Tulitarajia kuona akiapishwa kushika wadhifa huo Februari (2025) sehemu aliyopenda kuishi muda wake mwingi na kutoa mchango wake,” amesema.
Amesema Dk Ndugulile amefariki dunia akiwa katika umri mdogo na bado hajachangia vya kutosha vile alivyokuwa anatarajia.
“Inasikitisha, amefariki dunia nje ya Bara lake na Taifa lake, alitamani asaidie ujenzi wa mifumo na miundombinu madhubuti kwa Bara la Afrika, ni jambo linalosikitisha na linaumiza moyo.
“Watu wote wanaweza kuenzi kwa nafasi na matendo maisha aliyotamani kuyaishi, maono yake kwa Bara la Afrika kuwa na huduma bora, ni wajibu wetu kuendeleza yote aliyoyapenda,” amesema.
Aliyewahi kuwa rais wa MAT, Dk Elisha Osati amesema mchango wa Dk Ndugulile katika sekta ya afya ni mkubwa katika tiba, mifumo na marekebisho ya sheria ya mabaraza ya kitaaluma na sera kwa ajili ya mafunzo.
Amesema Taifa limepoteza mtu muhimu kwani uwepo wake WHO ungetoa fursa kwa sekta ya afya nchini katika mafunzo kwa wataalamu, programu za chanjo kwa majaribio, ugunduzi wa dawa na kushirikiana na mashirika mbalimbali ya afya duniani.
Kutokana na utaalamu wake katika afya ya jamii, amesema walitarajia kupata ufadhili wa mafunzo na kubadilishana utaalamu.
“Kama Taifa tumepoteza nafasi, kupitia diplomasia ya uchumi angetuwakilisha,” amesema.
Dk Osati amesema wakati wa kupambana na Uviko 19 akiwa rais wa MAT, alifanya kazi kwa karibu na Dk Ndugulile akiwa Naibu Waziri wa Afya.
“Tulishauriana sana hasa pale mwanzoni ni namna gani twende kama nchini na mependekezo yetu aliyachukua na kuyafanyia kazi, miongoni mwa hayo ni utengenezaji wa barakoa nchini, hata za vitambaa zinaweza kufaa,” amesema.
Mbunge wa Moshi Mjini Priscus Tarimo amesema:
“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa kifo cha mbunge mwenzetu Dk Faustine Ndungulile, na siyo tu mbunge mwenzangu, alikuwa anakaa mbele yangu, hivyo ni mtu ambaye nilikuwa naye karibu.
“Tumeshtushwa kwa sababu hatukuwahi kupewa taarifa ya kuugua kwake wala kusafiri, hivyo nilipoona habari asubuhi nilidhani ni mitandao tu, lakini baada ya muda mfupi nikaingia kwenye mtandao wa Bunge nikakuta ni taarifa rasmi.”