Dar es Salaam. Changamoto ya wananchi kutoyaona majina yao imeendelea kujitokea katika mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam, hatua inayosababisha baadhi kukata tamaa na kuondoka pasipo kupiga kura.
Mwananchi imepita katika mitaa mbalimbali kuangalia mwenendo wa upigaji kura wa kuchagua wenyeviti wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji pamoja na wajumbe wao na kubaini wananchi wakihangaika kutafuta majina yao.
Vituo vya kupigia kura vimeanza kufunguliwa saa 2:00 asubuhi ya leo Jumatano, Novemba 27, 2024. Mwananchi limepita maeneo mbalimbali na kushuhudia mwitikio wa wananchi ukiwa wa kawaida.
Kilio cha majina kutoonekana imejitokeza maeneo mengi. Kuna sehemu yalibandikwa na kuchanwa. Kuna maeneo majina hayaonekani licha ya wananchi kudai walijiandikisha.
Mkazi wa Magomeni, Ashura Khamis amesema amefika kituoni hapo saa 2 asubuhi lakini ametumia muda mrefu kuliona jina lake, ambalo katika karatasi zilizobandikwa halikuonekana.
“Karatasi za majina zilizobandikwa hazionekani vizuri, majina mengine hayaonekani kuna wengine wanakata tamaa na kuondoka.
“Baada ya kutumia muda mrefu kutoliona jina langu ilinilazimu kwenda kwa wasimamizi wa uchaguzi walionifungulia kitabu na kuhakiki hatimaye nikaliona na kupiga kura,” amesema Ashura.
Akizungumza na Mwananchi Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Hanifa Hamza amesema wameshatoa maelekezo kwa wasimamizi kuhakikisha kila mwananchi aliyejiandikisha na amejitokeza kupiga kura jina lake anasomewa na kupiga kura, ili kutimiza haki yake ya msingi.
“Wengine walikuwa wakilalamika kwamba maandishi hayaonekani kwa sababu ya nakala, kwa hiyo tumefuatilia na kulifanyia kazi, changamoto hiyo haipo,” amesema Hanifa.
Mkuu wa Mawasiliano wa Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Nteghenjwa Hosseah amesema kama jina halipo kwenye orodha ya wapiga kura huwezi kuruhusiwa kupiga kura leo.
“Ulitolewa muda wa watu kwenda kuhakiki majina kwa siku mbili, hao wanaodai majina yao hayapo kwenye orodha, walikwenda kujihakiki katika muda uliotolewa,” amehoji.
Amesema sio rahisi mtu kujiandikisha na jina lake lisiwepo katika orodha.
“Wao wanadai walijiandikisha je, ninyi mna uhakika kweli walijiandikisha? anayeweza kulisemea hili ni msimamizi wa hicho kituo, hata kama anawakumbuka kwa sura watu hao kweli walijiandikisha.
“Hata hivyo, kama jina halipo kwenye orodha, huwezi kupiga kura,” amesema Nteghenjwa.
Alipoulizwa kama kwa muda uliosalia kabla ya shughuli kupiga kura kufungwa, endapo itathibitika kweli watu hao walijiandikisha lakini sasa wanadai majina yao hayapo kwenye orodha, watapewa ruksa kupiga kura, amesema hawaruhusiwi kama hawapo kwenye orodha.
Kuhusu majina kuchanganywa bila kufuata alfabeti, amesema majina yaliyobandikwa kwenye vituo yapo kama yalivyoorodheshwa wakati wa kujiandikisha.
“Kwenye kujiandikisha kila mmoja alikuja kwa muda wake, kama alikuja Zubeda kisha akaja Hassan ndivyo yako hivyo.”
Kuwapo kwa vituo vipya vya kupigia kura tofauti na vilivyotumika kuandikisha imetajwa kuwa sababu ya wananchi kutoona majina yao katika sehemu walizojisajili.
Hilo limesemwa na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kata ya Mtoni, wilayani Temeke, Dar es salaam, Nobert Kamugisha baada ya kuwapo kwa malalamiko ya baadhi ya watu kutoona majina yao katika mitaa waliojiandikishia
Mwananchi ilipopita katika vituo tofauti vya kata hii imeshuhudia wananchi wakielekezwa kwenda kuangalia majina yao katika vituo vingine, licha ya kuwa walijiandikisha katika maeneo waliyofika.
Akijibu suala hilo, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kata ya Mtoni, Nobert Kamugisha amesema wakati wa kupiga kura vituo vingi vipya vinaanzishwa jambo ambalo limefanya watu kuhamishwa kutoka walikojiandikishia.
“Unapoandikisha wapiga kura mnaandikisha watu wengi katika kituo kimoja, lakini katika upigaji kura kile kituo kimoja kilichotumika kuandikisha huweza kuzalisha vituo vingine vinne hadi vitano, sisi vituo tulivyotumia kuandikisha vimezaa vituo vingine zaidi,” amesema.
Amesema hali hiyo ndiyo iliyofanya wananchi wengi kutoona majina yao kwani hudhani sehemu ambayo walijiandikisha ndiyo watakayoona majina yao pekee, na pindi wanapokosa wanadhani majina yao hayapo.
“Tunashirikiana na mawakala na wasimamizi kuwaelekeza wapiga kura kwenda kwenye maeneo ambayo wanaweza kupata majina yao hasa katika vituo vipya vilivyozalishwa,” amesema Kamugisha.
Amesema eneo lake lina vituo 92 vya uchaguzi na tayari vimefanyiwa ukaguzi ili kuweza kutatua changamoto zilizopo.
“Wananchi wana hamasa, wengine walifika saa moja na nusu asubuhi kabla vituo havijafunguliwa ili wawe wa kwanza kupiga kura na kweli walimaliza mapema na kuendelea na shughuli zao,” amesema Kamugisha.
Changamoto ilikuwepo pia katika eneo la Tandale, ambapo baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Pakacha waliofika kituoni walidai majina yao kutoonekana katika karatasi zilizobandikwa ukutani.
“Tulishazoea zile karatasi zinazopigwa ‘photocopy’ ambazo majina yanaonekana vizuri lakini sio hizi majina ni changamoto kuyaona hadi uombe uhakikiwe kwenye kitabu,” amesema Mussa Ramadhan.
Hata hivyo, baada ya sintofahamu hiyo wananchi wa Pakacha waliojitokeza kupiga kura waliwashauri viongozi wa mtaa huo kusoma kitabu cha majina yao moja baada ya jingine ili kujua hatma yao.
“Tumeamua kumshauri mtendaji asome majina ya wapigakura yaliyopo katika kitabu hata kama itachukua muda mrefu, kikubwa yaitwe ili tupate haki yetu,” amesema Bakari Rashid.
Hata hivyo, baada ya muda mtendaji wa mtaa huo, Judith Mpira akishirikiana na wasaidizi wake alianza kusoma majina ya wananchi ambapo walipata fursa kupiga kura.
“Nina vituo sita, nitahakikisha kila aliyejiandikisha anapata fursa ya kupiga kura, nitasoma vitabu vya majina lakini tunajitahidi kila iwezekanavyo watu wapate haki. Napambana huku na kule kuhakikisha nasolve ‘kutatua’ changamoto hii.”
“Wakati wa uandikishaji baadhi yao wamesahau wamejiandikisha kituo gani, hivyo tunatoa usaidizi wa kuhakikisha wanapata haki yao ya kuona majina na kupiga kura,”amesema Mpira.
Mary John anayeishi Mtaa wa Pakacha amesema, “ukiona jina unapiga kura bila wasiwasi utaratibu mzuri, nilipofika sikuliona jina langu, lakini nilipata usaidizi kutoka kwa wasimamizi wa uchaguzi.”
‘Tulianza na changamoto ya majina’
Huko Kigamboni, Dar es Salaam, msimamizi msaidizi wa uchaguzi Mtaa wa Feri, Kata ya Kigamboni, Vitus Lazary amesema shughuli ya upigaji kura imeanza vizuri isipokuwa wakati wanafungua kulikuwa na mkanganyiko wa majina.
“Mkanganyiko umejitokeza baada ya kuongezeka kwa idadi ya vituo, wakati wanajiandikisha kulikuwa na vituo vinne lakini leo vimeongezeka hadi 17 na imefanyika hivi ili kurahisisha shughuli ya upigaji kura,” amesema Vitus.
Vitus amesema katika shughuli ya upigaji kura wanatoa kipaumbele kwa makundi maalumu ikiwemo wazee, walemavu na wasiojua kusoma na kuandika.
“Wasimamizi wasaidizi walipewa mafunzo maalumu ya kuwasaidia watu wa namna hiyo, ndiyo maana shughuli inaenda vizuri na tunaamini tutamaliza kwa wakati,” amesema
Kuhusu mawakala wa vyama amesema vyama viwili ikiwemo CCM na Chadema wameweka mawakala katika vituo vyote 17 huku ACT-Wazalendo wakiweka mmoja.
Wananchi Kibaha ‘walia’ kutoona majina
Wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani, baadhi ya wananchi wamelalamikia kutokuwepo kwa majina yao katika vituo walivyojiandikishia kupiga kura, hivyo kukosa uhakika wa kutimiza haki yao hiyo ya msingi kikatiba.
Katika kituo cha kupigia kura cha Kumba, kilichopo Kibaha kwa Mfipa baadhi ya wananchi walilalamika kutokuwepo kwa majina yao licha ya kujiandikisha.
Radhia Said amesema amefika kituoni hapo saa 1:30 asubuhi ili kuhakiki jina lake.
“Nimelitafuta zaidi ya mara nne sijaliona, sijui kama nitapata nafasi ya kupiga kura,” amesema kwa unyonge huku akikaa pembeni kusikilizia hatma yake ya kupiga kura.
Mwananchi mwingine, Swema Juma pia alidai kutoona jina lake licha ya kujiandikisha siku ya pili tu baada ya uandikishwaji kuanza.
Katika kituo hicho, wazee walipewa kipaumbele katika upigaji kura, huku utaratibu ukiwa ni kupiga kura za ndiyo au hapana kwa wagombea sita wa nafasi mbalimbali.
Kwenye kituo cha Galagaza, Kibaha pia baadhi ya wananchi walidai kutoona majina yao licha ya kujiandikisha.
Veronica Masatu amesema hana hakika wa kupiga kura licha ya kujiandikisha.
“Silioni jina langu na sijui nitamuuliza nani, japo nilijiandikisha,” amedai.
Changamoto nyingine inayolalamikiwa na majina kutopangwa kwa alfabeti, hivyo wananchi wengi kulazimika kutumia muda mrefu kutafuta majina yao.
Katika vituo hivyo, wananchi walitangaziwa majina kutopangwa kwa mtiririko wa herufu (alfabeti), hivyo katika kujihakiki wanapaswa kupitia jina moja baada ya jingine na utakapoona jina lako ndipo unaendelea na utaratibu mwingine wa kupiga kura.
Mwananchi limefika katika vituo vya kupigia kura vya Ilala Boma na Buguruni na kukuta kilio cha majina kutokupangwa kwa mpangilio wa herufi hali iliyowafanya baadhi kutopiga kura na kuondoka na wengine wakiamua kuvumilia kuyatafuta.
Ramadhani Kiloko, mkazi wa Buguruni amesema kutokana na hilo, mtu mwenye herufi inayoanzia na R anajikuta kachanganywa na wenye herufi nyingine jambo linalowapa shida kuyapata majina yao na kujikuta wanazunguka muda mrefu kituoni kuyatafuta.
“Ukiacha herufi za majina kuchanganywa, pia jingine ni vyumba tulivyojiandikisha majina, sipo unapokuta jina lako na hivyo kuleta usumbufu ukizingatia wengine vibarua, hivyo tumetoka mara moja ofisini kuja kupiga kura,” amesema Kiloko.
Hawa Sultani, mkazi wa Buguruni kwa Madenge, amesema imemchukua saa kutafuta jina lake hadi kulipata kutokana na adha hiyo ya herufi kuchanganywa.
Ukiacha suala la majina pia wananchi wameshauri uchaguzi mwingine picha za wagombea ziwepo ili kuweza kuwajua wagombea wao.
Wilhard Damian, mkazi wa Ilala Maghorofani, amesema kuwepo kwa picha hizo kungesaidia pia wapiga kura kuwajua viongozi wao kwa sura.
Katika hatua nyingine wananchi hao wamesema hali ni shwari katika vyumba vya kupigia kura kwani wasimamizi wamekuwa wakiwaelekeza.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa na habari zaidi