Usiri unavyoleta ugumu mapambano dhidi ya ukeketaji

Dar es Salaam. Usiri uliojengeka miongoni mwa wazazi, umetajwa kuwa sababu ya kuendelea kuwapo kwa vitendo vya ukeketaji katika Wilaya ya Longido mkoani Arusha.

Usiri huu unalenga kukwepa mkono wa sheria hasa baada ya Serikali kuendelea kuimarisha nguvu zake katika kudhibiti vitendo hivi, huku wanaotekeleza unyama huo wakibuni mbinu mpya za kutekeleza azma yao kimyakimya ikiwemo kutumia sherehe za ubatizo na kipaimara.

Mwananchi ilifunga safari hadi Wilaya ya Longido na kutembelea baadhi ya vijiji katika eneo hilo, kujionea hali ilivyo ili kujua kwa nini mkoa huo unaendelea kuwa kinara katika vitendo vya ukeketaji.

 “Wamebadili mbinu siku hizi, wanakeketa watoto wakiwa wadogo hawajitambui, baadaye watakuja kujua kama kuna kiungo kimepungua mwilini mwao wakianza kufundishwa,” anasema Mary Laiser ambaye ni mhamasishaji kutoka taasisi ya Tembo.

Anasema jambo hilo linaweka ugumu kwa watoto kushindwa kudai haki zao kwa sababu baadhi hudhani ni hali ya kawaida waliyozaliwa nayo.

Tofauti na miaka ya nyuma, sherehe za ukeketaji zilikuwa zikifanyika waziwazi lakini siku hizi usiri umetawala, jambo ambalo linafanya mtoto kukeketwa akiwa mdogo na umri unapofika wa kuvuka rika, inafanyika sherehe tu.

Jambo hili limeufanya Mkoa wa Arusha na Manyara kuendelea kuwa vinara kwa kuwa na asilimia 43 ya ukeketaji ukifuatiwa na Mara wenye asilimia 28.

Licha ya kuwa kiwango hicho bado ni kikubwa, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima akiwa Bungeni jijini Dodoma Mei mwaka huu, alisema kiwango cha ukeketaji kitaifa kimeendelea kupungua.

Alisema takwimu za hali ya afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria Tanzania za mwaka 2022/2023, zinaonyesha kupungua kwa vitendo vya ukeketaji nchini, kutoka asilimia 10 kwa mwaka 2015/2016 hadi asilimia 8 kwa mwaka 2022/2023.

Lakini wakati nuru ikiendelea kuonekana, kinamama wanatajwa kuwa moja ya watu wa kukumbatia suala hilo.

“Wakati mwingine wanaofanya ukeketaji huu kuendelea ni kina mama, wao ndiyo wanaosimamia ukeketaji unapotaka kufanyika, kinababa wanakuwa watu wa kufuata kile wanachokisema,” anasema Paul Tejeni baba na kiongozi wa mila.

Anasema ukeketaji katika eneo hilo ni kama fahari na pindi kitendo hicho kinapofanyika ndiyo mtu huonekana amekamilika na wa maana, na inapotokea mtu anapinga ukeketaji huonekana kama amekengeuka na anatengwa na jamii inayomzunguka.

Hata hivyo, hali hii ni tofauti na zamani, sherehe hizo zilifanyika kwa uwazi na kila mtu alijua, huku wasichana wakiandaliwa kisaikolojia.

Nasanyai Ndete kutoka kijiji cha Oldoko anasema anakumbuka wakati wanakeketwa walikuwa watoto tisa kutoka boma moja na wenzake walikuwa wakijua kitakachotokea isipokuwa yeye.

“Tulipofunga shule mwezi wa 12 na kurudi nyumbani nilikuta wenzangu wako tayari kwa ajili ya kukeketwa na mimi nilitaka, kwa wakati huo nilitamani kwa sababu ilikuwa inaaminika kuwa mtu ambaye hajakeketwa anaonekana kama siyo mtu aliyekamilika,” anasema Nasanyai na kuongeza;

“Babu yangu alisema nibaki kwanza nisikeketwe kwa sababu nilikuwa msichana mdogo (miaka 11) mimi niligoma na nikasema sitakwenda shule bila kukeketwa ninachokumbuka siku hiyo kuna wenzetu walitoka sana damu.”

Maneno ya Nasanyai yanaungwa mkono na Nongishu Kalembu ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Oldoko anayeeleza kuwa zamani ukeketaji ulikuwa hiari, kwa sababu elimu haikuwa imetolewa na kwa wakati huo hakuona madhara lakini alikutana nayo alipokuwa mtu mzima.

Anasema ukeketaji huo ulitumia wembe bila ganzi na kila mama mwenye nyumba aliandaa wembe kwa ajili ya kumkeketa mwanaye ambao ulikabidhiwa kwa ngariba alipofika.

Licha ya kuona fahari kwa wakati huo kutokana na kutimiza moja ya takwa la kimila, lakini bado kumbukumbu za kupata fistula zinazunguka katika vichwa vyao ambazo zinawafanya kusimama kupinga watoto wao wasikeketwe.

Mbali na kupata fistula, kwa Anna Simeli ambaye ni ngariba mstaafu kutoka Kijiji cha Oltepes mara zote anakumbuka namna alivyokuwa akishuhudia watoto wakitoka damu nyingi baada ya kukeketwa.

Hali hiyo ilimfanya kuanza kuchukia ukeketaji, mara zote alikumbuka alipokeketwa; “Nashukuru Mungu nilipata elimu ya madhara ya ukeketaji nikaamua kuacha, mimi ni mama wa watoto 10 na ilifika mahali nikawa sitaki kukeketa watoto wangu lakini nikiitwa kwa watoto wa wengine naenda, nimekeketa watoto sita ndani ya boma letu sikutaka kukeketa wa nje.”

Moja ya kumbukumbu za Simeli akiwa mmoja wa watu waliokeketwa ni fistula aliyoipata alipojifungua baada ya kupoteza uwezo wake wa kuzuia mkojo.

Kufuatia ugonjwa wa fistula ambao humfanya mama kushindwa kujizuia haja ndogo au kubwa baada ya kujifungua, wanawake waliokeketwa huzuiwa kula wakati wa ujauzito ili kuepusha kupata watoto wenye uzito mkubwa na kuwasababishia waongezewe njia wakati wa kujifungua.

Alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi wa kupinga ukeketaji ulioandaliwa na Shirika la wanahabari la Maipac, Septemba 17 mwaka huu, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Longido, Dk Methew Majani alisema wamebaini wanawake kuwa dhaifu wanapofikishwa hospitali kujifungua kutokana na kutopewa chakula.

Mwananchi ilizungumza na baadhi ya mabinti ambao wameepuka kufanyiwa ukeketaji huku wakibainisha kuwa wakati mwingine imani anayojengewa mtu ndani ya familia, humfanya mwenyewe kuchagua kukeketwa hata akiwa na elimu.

“Tangu unakua unaaminishwa kuwa kitendo hiki ni kizuri, usipofanyiwa unakua kama umekengeuka, sasa kwa sababu wote wanaokuzunguka wanakuwa wamefanyiwa unajihisi kama umekosa kitu,” anasema Linda Olei.

Hali hiyo huwafanya baadhi ya wasichana ambao tayari wamesoma hadi sekondari kukubali kufanyiwa vitendo hivyo kwa hiari yao, ili kuepuka kutengwa na kunyanyapaliwa na jamii inayowazunguka.

Aliyekuwa Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Longido, Rashid Lugunda anasema ugumu wa mapambano hayo unatokana na kugusa sehemu ya mila ya jamii husika, kwani kadri nguvu inavyoongezwa ndivyo nao wanabuni njia mpya za kutekeleza vitendo hivyo.

“Tulikuja kubaini kuwa kwa sasa wanatumia sherehe za ubatizo na kukeketa watoto wachanga ikiwa ni mbinu za kuukwepa mkono wa Serikali,” anasema.

Anasema Serikali inaendelea kudhibiti suala hilo kwa kuweka watu maalumu wanaoweza kutoa taarifa pindi wanapobaini vitendo hivyo.

“Pia tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria kuhakikisha mila na desturi zilizopitwa na wakati ndani ya wilaya hii zinakomeshwa ikiwemo mimba za utotoni, ndoa na ukeketaji,” anasema Lugunda ambaye siku moja baada ya mahojiano haya, alifariki dunia kwa ajali ya gari.

Katika upande wa watoto zimeundwa klabu za shule zikilenga kuwafundisha kujua haki zao ili waweze kujilinda na wanapoona viashiria vya ukatili watoe taarifa.

Pia wanatumia viongozi wa mila, wenyekiti wa vijiji vitongoji ili kutoa elimu juu ya mambo yanayoenda kinyume na taratibu za serikali.

Kwa upande wake Ofisa Maendeleo Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Mussa Kabula anasema wamekuwa wanalichukua suala la ukeketaji kama ajenda kila wanapokwenda kwenye shughuli za kijamii kwa kutoa elimu.

Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation

Related Posts