Walalama majina kutosomeka vizuri | Mwananchi

Musoma. Wakazi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara wanalalamikia majina ya wapiga kura yaliyobandikwa kwenye baadhi ya vituo kutosomeka vizuri.

Hali hiyo imeelezwa kuchangia usumbufu kwa wapiga kura waliojitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaofanyika nchini kote leo Jumatano Novemba 27, 2024.

Akizungumza na Mwananchi, mkazi wa Kata ya Bweri, Stella Wambura amesema ameshindwa kubaini chumba anachopaswa kupiga kura ni kipi.

“Nimefika hapa tangu saa moja asubuhi kila nikijaribu kusoma sioni jina langu na mbaya zaidi maandishi hayaonekani, nashindwa kujua nijipange kwenye foleni ya kwenda chumba kipi cha kupigia kura,” amesema Wambura.

Mpigakura mwingine Yohana Marwa amesema majina mengi yamefifia na kusababisha watu kutumia muda mwingi kuyasoma.

“Mimi nimejaribu kusoma nikashindwa maana maandishi hayasomeki kabisa, nikaamua  kupanga foleni, naingia ndani msimamizi ametafuta jina langu bila mafanikio ikabidi niende kwenye chumba cha pili kuanza upya, nimetumia muda mwingi bila sababu,” amelalamika Marwa.

Naye Emma Masige amesema; “Hapa inatakiwa mtu unafika unasoma jina liko wapi kisha unapanga foleni badala ya kuanza kuhangaika hii itasababisha upigaji kura kuchukua muda mrefu.”

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka akitafuta jina lake kwenye orodha ya wapiga kura iliyobandikwa kwenye kituo cha kupigia kura katika kata ya Mukendo Manispaa ya Musoma. Picha na Beldina Nyakeke

Msimamizi wa uchaguzi katika Manispaa ya Musoma, Bosco Ndunguru amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo.

“Wakati wa uandikishaji kulikuwa na nakala nne, hivyo ni dhahiri kuwa nakala ya tatu maandishi huwa yanafifia, lakini hii haimaanishi kuwa mtu hatapata nafasi ya kupiga kura, majina yote yapo kwenye daftari katika vituo husika,” amesema.

Akizungumza baada ya kupiga kura katika kituo cha Ofisi ya Kata ya Mukendo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amewataka wakazi wa mkoa huo kuendelea kujitokeza kupiga kura ili waweze kupata viongozi wenye sifa.

“Kampeni zimefanyika kwa ustaarabu na amani, hivyo niwahimize wote waliojiandikisha wajitokeze kupigakura muda bado upo mpaka saa 10 jioni leo, ili tumalize ngwe hii ya mwisho kama tulivyoanza mwanzo,” amesema Mtambi.

Amesema Serikali mkoani humo imejipanga kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani na utulivu hivyo kuwataka wananchi kutokuwa na hofu yoyote.

“Kama kuna mtu anawaza kufanya fujo leo, nimtake atoe wazo hilo kichwani mwake lakini pia niwakumbushe kuwa uchaguzi huu unafanyika kwa mujibu wa kanuni, kwa hiyo kama kuna mtu ataona mambo hayajaenda sawa anatakiwa afuate utaratibu akate rufaa kama ilivyokuwa kwenye majina ya wagombea,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema anaridhishwa na namna ambavyo uchaguzi unaendelea hadi sasa na kuwataka wananchi waendelee kujitokeza kupiga kura, huku wakizingatia suala la amani na utulivu.

“Changamoto mlizosema zitafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo lakini hadi sasa sijaona changamoto kubwa ya kutufanya tusikamilishe jambo letu, tuendelee kujitokeza tutumie haki yetu ya kikatiba kuwapata viongozi wetu,” amesema Chikoka.

Related Posts