Dar/Mikoani. Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini wamejitokeza kwenye vituo vya kupigia kura kufanya uamuzi kwa kuwachagua viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji watakaohudumu kwa miaka mitano ijayo.
Uchaguzi unafanyika leo Novemba 27, 2024 ikiwa ni mapumziko baada ya siku saba za kampeni zilizohitimishwa jana Novemba 26.
Novemba 16, 2024, akitoa takwimu za wagombea, Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alisema nafasi za wenyeviti (mitaa, vijiji na vitongozi) zinazowaniwa ni 80,430 na kati ya hizo upinzani una wagombea kwenye nafasi 30,977 sawa na asilimia 38.
Alisema kwa kuzingatia maeneo ya utawala yaliyotangazwa katika Gazeti la Serikali, Tangazo Na.796 na 797 ya Septemba 6, 2024, vijiji vilivyopo ni 12,333, mitaa 4,269 na vitongoji 64,274.
Alisema hata hivyo, kutokana na Halmashauri za Wilaya za Kaliua, Nsimbo na Tanganyika kuwa na makazi ya wakimbizi ya Ulyankulu, Katumba na Mishamo na wananchi kuhama kwenye baadhi ya vitongoji kutokana na sababu mbalimbali, maeneo yatakayofanya uchaguzi kwa sasa ni vijiji 12,280, mitaa 4,264 na vitongoji 63,886.
Nafasi zitakazogombewa ni 12,280 za mwenyekiti wa kijiji, 4,264 mwenyekiti wa mtaa na 63,886 za mwenyekiti wa kitongoji. Wajumbe wa Serikali ya kijiji watagombea 230,834 na 21,320 wa kamati ya mtaa.
Idadi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi huo ni milioni 31.
Kwenye vituo mbalimbali vya kupigia kura imeshuhudiwa wananchi wakipewa maelekeo na wasimamizi wa uchaguzi na baadaye kupiga kura.
Wananchi wanaofika kwenye vituo hatua ya kwanza ni mchakato wa kuhakiki jina, baadaye wanaelekea kupiga kura ambako kuna masanduku matatu ya mwenyekiti, wanawake na makundi maalumu.
Jana Novemba 26, Rais Samia Suluhu Hassan alisema ni muhimu kuheshimu uamuzi wa wapigakura.
Alisema demokrasia yenye nguvu inajengwa kwa misingi ya heshima na mshikamano, akiwataka wananchi wote waliojiandikisha katika mchakato huo, kujitokeza kupiga kura.
Pia, aliwataka kujiepusha na vitendo vya vurugu, uchochezi na uvunjifu wa amani.
“Niwasihi wasimamizi wa uchaguzi na wanaohusika, kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, uwazi kwa kuzingatia taratibu zilizokubaliwa na wadau. Matumaini yangu mtaendelea kutekeleza majukumu yenu kwa weledi, kulinda haki za wananchi na kudumisha utulivu tunapoelekea mwisho wa mchakato huu,” alisema.
Rais Samia akihutubia Taifa Ikulu jijini Dodoma, kuhusu mchakato wa uchaguzi, alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia kanuni zilizopo.
Aliwataka wadau wa uchaguzi kutoa ushirikiano ili kufanikisha azma ya kuwa na uchaguzi wa amani unaoakisi heshima ya Taifa lenye mshikamano na demokrasia imara.
Endelea kufuatilia Mwananchi.