Kilimanjaro. Wakati kazi ya kupiga kura ikiwa imemalizika katika vituo vya kupigia kura Mkoani Kilimanjaro na maeneo mengi nchini, baadhi ya wapigakura mkoani hapa wameeleza changamoto waliyokumbana nayo ikiwa ni pamoja na kutumia muda mrefu kutafuta majina yao.
Katika vituo mbalimbali vya wilayani Moshi ambako Mwananchi imepita kuanzia asubuhi vikiwamo vya Makongoro, Karanga, Msaranga, Kilimani na Mawenzi, mwamko wa wananchi ulikuwa mkubwa licha ya changamoto za kupanga foleni.
Sifael Laizer aliyepiga kura katika kituo cha Karanga amesema upigaji kura umeenda vizuri lakini changamoto ilikuwa utafutaji majina iliochukua muda mrefu.
Naye Witness Mziray, mkazi wa Kilimani-Bomambuzi amesema licha ya upigaji kura kumalizika salama, lakini ametoa wito kwa Serikali uchaguzi ujao majina yaandikwe kwa kufuata alfabeti ili kuondoa usumbufu kama uliojitokeza leo.
Mpigakura, Sifael Laizer amesema upigaji kura umeenda vizuri na kwa utulivu licha ya kuwa na changamoto kadhaa.
Amesema anatarajia kupata kiongozi ambaye atawaletea maendeleo wanayoyataka kwenye mtaa wao.
Mpiga kura mwingine aliyepiga kura katika kituo cha Karanga, Adam Marialle amesema uchaguzi ujao Serikali iboreshe uandishi wa majina, tatizo ambalo limeonekana katika maeneo mengi.
Ester Shehiza amesema katika uchaguzi wa leo ameshuhudia mwamko mkubwa katika eneo lake.
“Watu wamejitokeza kwa wingi kupiga kura, sasa tunasubiri kupata matokeo,” amesema.
Hali ilivyo Wilaya ya Hai
Mapema leo Mwananchi Digital ilipita katika vituo mbalimbali vya kupigia kura wilayani Hai na kushuhudia wananchi wengi wakiwa wamejitokeza kutimiza haki yao ya kikatiba.
Mmoja wa wapiga kura katika kituo cha Uduru, Saashisha Mafuwe amesema hatua hiyo imefanyika vema kwa amani na utulivu.
Akizungumzia changamoto zilizojitokeza ikiwamo ya majina kutooneka, Mratibu wa uchaguzi Mkoa wa Kilimanjaro, Jasper Ijiko amesema aliwaelekeza wasimamizi wa uchaguzi mkoani humo kuhakikisha kituo kilichokuwa na changamoto ya majina kutoonekana vizuri, watumie daftari la ndani.
“Niliwaelekeza wasimamizi wetu kwamba wananchi wakibabaika kutafuta majina yao, wachukue majina yao mapema ili waangalie jina lake kwenye daftari la wapigakura, akiwa nje aambiwe yeye ni namba fulani ili iwe rahisi kuondokana na changamoto hiyo,” amesema Ijiko.
Aidha, amesema kazi ya kupiga kura imeenda salama kwa utulivu mkubwa, na kama kutatokea tatizo kwenye hatua inayofuata itafanyiwa kazi kwa haraka na kupatiwa ufumbuzi.
“Watu wamejitokeza kwa wingi na hatua ya upigaji kura imeenda vizuri na vituo vyetu ni 2,461 na tuna wapiga kura 1,090,312 waliotarajiwa kupiga kura leo,” amesema Ijiko.
Amesema vyama vilivyosimamisha wagombea ni 10, huku Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chadema vikiwa na wagombea wengi zaidi.