Wenye nyumba wanavyoweza kuepuka jinai kwa makosa ya wapangaji

Dar es Salaam. Onyo la Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) kwa wamiliki wa nyumba zinazohusishwa na dawa hizo haramu limeibua mjadala wa umuhimu wa wananchi kufuatilia sheria na kanuni za upangishaji ili kuepuka kushtakiwa kijinai kwa makosa ya mpangaji.

Kamishna wa DCEA, Aretas Lyimo amewataka wamiliki wa nyumba kuwa makini na wanaowapangisha ili kuepuka adhabu wanazoweza kukumbana nazo ikiwemo faini, kifungo au nyumba kutaifishwa.

Lyimo Novemba 25, 2024 akizungumzia kukamatwa watu saba kwa tuhuma za kukutwa na kilo 2,207.56 za aina mbalimbali na dawa za kulevya na dawatiba zenye asili ya kulevya, alisema wamebaini wahusika wa biashara haramu ya dawa za kulevya hutumia mbinu ya kupanga nyumba ambazo zinageuza kuwa maghala ya kuzihifadhi, huku wao wakiishi katika maeneo mengine.

“Mamlaka inatoa rai kwa wamiliki wa nyumba kuwa makini wanapopangisha nyumba zao, kwani nyumba inayotumika kwa shughuli za dawa za kulevya ni kinyume cha sheria na inaweza kutaifishwa,” alisema.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95, imeweka katazo kwa mmiliki au msimamizi wa nyumba, msimamizi wa eneo au chombo cha usafirishaji kuruhusu vitumike kwa lengo la kutengeneza, kuvuta, kujidunga, kuza au kununua dawa za kulevya.

Alisema mmiliki anapojua kuwa kosa linatendeka kwenye eneo lake, ana jukumu la kutoa taarifa kwa mamlaka.

“Kushindwa kufanya hivyo ni kosa la jinai, na akitiwa hatiani adhabu yake inaweza kuwa faini kuanzia Sh5 milioni hadi Sh50 milioni au kifungo cha miaka mitano hadi 30 jela au vyote kwa pamoja,” alisema.

Mwanasheria Patience Mlowe amewataka wananchi kutochukulia mambo kienyeji, badala yake wafanye uhakiki wa kina kuhusu mpangaji kabla ya kukubali kumkodisha nyumba.

Amewataka kuangalia historia ya mpangaji, ikiwamo shughuli zake za biashara au binafsi.

“Mwenye nyumba lazima ajue anayempangisha anafanya kazi gani, anafanya kazi wapi na kitambulisho chake kiwepo kwenye mkataba,” amesema.

Katika kuangalia utambulisho huo, Mlowe amesema, mpangaji hapaswi kuwa na historia ya kujihusisha na shughuli haramu.

“Halafu hizo taarifa azipeleke Serikali za mitaa. Tuepuke kufanya mambo kienyeji,” amesema Mlowe.

Amesema wenye nyumba pia wanatakiwa kufuatilia matumizi ya nyumba mara kwa mara, kwa heshima ya faragha ya mpangaji na endapo watabaini kuwepo kwa shughuli haramu waripoti polisi au mamlaka nyingine husika mara moja.

Kwa upande wa wapangaji wana wajibu wa kulipa kodi, kutunza mazingira ya pango au ardhi, kuruhusu mmiliki kukagua eneo, kukabidhi pango au ardhi katika hali ambayo alipangishwa, kutokuweka rehani, kupangisha na kubadilisha umiliki wa pango na kutumia pango kwa matumizi yaliyoidhinishwa kwenye mkataba.

Mkurugenzi wa Taasisi ya HakiArdhi, Cuthbert Tomito amesema Kamishina wa DCEA ametoa tahadhari za kiusalama zinazoelezwa na Sheria ya Serikali za Mitaa namba 7 ya 1982.

“Sheria hiyo inazipa mamlaka za Serikali za vijiji na mitaa kuwa na taarifa za wageni wanaoingia katika maeneo husika. Wajumbe wa nyumba 10 hawapo kisheria, lakini wanaingia humohumo kuwa na taarifa za wageni,” amesema.

Hata hivyo, amesema sheria hiyo haina nguvu kwa sababu haina kanuni za kukazia utekelezaji wake.

“Ndiyo maana hata usipokwenda kutambulisha mgeni wako Serikali za mitaa hawakuchukulii hatua. Alichokisema Kamishna ni kuchukua tahadhari kwani sheria ya dawa za kulevya inasema ukikutwa na dawa, nyumba yako itataifishwa,” amesema.

Amesema licha ya kuwepo sheria mbalimbali zinazogusa upangaji wa ardhi na majengo, lakini hakuna iliyo mahususi ya upangaji wa nyumba.

Amesema kutokana na hali hiyo kumekuwa na upangishaji holela wa nyumba, wamiliki wake wakiwa na mamlaka makubwa ya kuamua muda wa kulipa kodi na viwango wanavyotaka.

“Tuna changamoto kubwa ya kutokuwa na sheria mahususi ya upangaji wa nyumba ndiyo maana utakuta mtu anapanga nyumba Sinza analipa Sh100,000 mwingine katika eneo hilohilo analipa bei kubwa zaidi.

“Zile sheria za mikataba, sheria ya ardhi na nyinginezo hazina vifungu mahususi vya kuratibu upangishaji wa nyumba. Kwa mfano, sheria ya mikataba inaeleza mikataba ya kupangisha au kuuziana nyumba, magari na vitu vingine,” amesema.

Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999, Sheria ya Mabaraza ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Namba 2, Sheria ya Udhibiti wa Kodi ya Pango Na. 7 ya 1984 na Sheria ya Mikataba kwa namna fulani zinagusia masuala ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kati ya mmiliki na mpangaji pia mali isiyohamishika kama vile nyumba.

Mmoja wa wapangishaji anayejitambulisha kwenye mtandao wa Facebook kwa jina la Buuh Smart amesema huwa wanachukua taarifa zote za wapangaji.

“Kwanza tunauliza anafanya kazi gani na tunachukua kitambulisho chake, halafu taarifa hizo tunapeleka kwa mjumbe,” amesema.

Hata hivyo, amesema hajawahi kukutana na changamoto kwa wapangaji wake.

Akizungumza na Mwananchi Novemba 26, 2024 kuhusu kauli ya DCEA, mwanasheria Dk Onesmo Kyauke amesema kinachopaswa kuangaliwa ni nia ovu.

“Kwenye masuala ya jinai kuna vitu vinaitwa, Mens Rea yaani nia ovu na Actus Reus yaani kitendo. Kwa hiyo ni lazima kuwe na nia ovu ndipo utende uovu, bila hivyo hakutakuwa na kosa,” amesema.

Amesema sheria zote ni lazima zifuate utaratibu huo na kuongeza: “Sasa kama wewe unajua kwamba umempangisha mtu anayefanya biashara ya dawa za kulevya, maana yake una nia ovu.

“Kama umempangisha mtu ambaye hujui kuwa anafanya biashara hiyo, utakapojua lazima utoe taarifa, usipotoa maana yake una nia ovu.

“Unapompangisha mtu nyumba maana yake mpangaji ana haki za faragha, hivyo siyo rahisi kujua anafanya nini kwenye nyumba hiyo,” amesema.

Maelezo hayo yameungwa mkono na mwanasheria Jebra Kambole anayesema Mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kutaifisha mali.

“Uhusiano kati ya mwenye nyumba na mpangaji ni wa mkataba tu na anapompangisha mtu, yule mpangaji anakuwa na haki zake. Huwezi kuja kumchunguza na hata kama unataka kufanya matengenezo ni lazima umjulishe kwanza. Itakuwa ni Mahakama ya ajabu kutaifisha nyumba ya mtu asiye na kosa,” amesema.

Mwanasheria Alloyce Komba amesema ili mwenye nyumba ahusishwe na kosa hilo ni lazima DCEA ifanye uchunguzi wa kutosha kubaini uhusika wake.

“Inabidi kwanza kamishna afanye uchunguzi wa kutosha kubaini kwamba nilihusikaje? Je, sikufanya uchunguzi wa kutosha wa mpangaji kabla ya kumpangisha?

“Vilevile aangalie wahusika wengine kama madalali ambao sasa wamechukua nafasi za wenye nyumba na wanasheria,” amesema.

Related Posts