NYOTA wa Simba, Jean Charles Ahoua na Moussa Camara wamekihakikishia kikosi hicho kuondoka na pointi tatu muhimu katika ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika mchezo huo wa kundi ‘A’ uliopigwa juzi, Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, bao hilo pekee lilifungwa na kiungo nyota, Jean Charles Ahoua dakika ya 27 baada ya beki wa Bravos, Antonio Edmilson kuudaka mpira eneo la hatari.
Bao hilo ni la kwanza kwa Ahoua katika michuano ya kimataifa tangu ajiunge na timu hiyo msimu huu akitokea Stella Club Adjame ya kwao Ivory Coast, akiendeleza kiwango bora na kikosi hicho baada ya kuonyesha uwezo mkubwa Ligi Kuu Bara na kukifanya kikosi hicho kukaa kileleni mwa msimamo na pointi 28, baada ya kuhusika na mabao tisa hadi sasa baada ya kufunga matano na kuchangia manne ‘Assisti’ kati ya 22, ya timu nzima.
Licha ya Ahoua kufunga bao hilo muhimu ila shujaa mwingine wa Simba aliyefanya mchezo huo kumalizika kwa ushindi huo ni kipa, Moussa Camara aliyeokoa penalti ya Emmanuel Edmond dakika ya 48 na kukirejesha kikosi hicho cha Msimbazi mchezoni.
Uwezo wa Ahoua ni sawa na kwa kipa, Camara ambaye tangu ajiunge nayo akitokea Horoya AC ya kwao Guinea, amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi hicho hadi sasa.
Katika michezo mitatu ya michuano ya CAF ambayo ameicheza msimu huu akianzia miwili ya mchujo kusaka tiketi ya kufuzu hatua ya makundi, ni mmoja tu alioruhusu bao ambao ni wa ushindi wa mabao 3-1, dhidi ya Al-Ahli Tripoli ya Libya.
Kama haitoshi, kipa huyo ndiye anayeongoza kwa kucheza michezo mingi bila ya kuruhusu bao ‘Clean Sheets’ katika Ligi Kuu Bara kwani hadi sasa tayari amecheza mechi zote 11 na kati ya hizo tisa hajaruhusu nyavu zake kutikiswa langoni mwake.
Ushindi huo umeifanya Simba kuendeleza rekodi bora hadi sasa kwani mchezo huo unakuwa ni wa sita mfululizo kwa timu hiyo chini ya Kocha Fadlu Davids tangu mara ya mwisho ilipofungwa bao 1-0 na Yanga katika Ligi Kuu Bara Oktoba 19 mwaka huu.
Tangu ifungwe mara ya mwisho na Yanga, Simba imekuwa na rekodi bora kwani katika michezo hiyo sita haijaruhusu bao lolote huku ikiwa na wastani mzuri wa kufunga mabao katika vipindi vyote viwili kwa maana ya cha kwanza na cha pili.
Katika michezo hiyo sita Simba imefunga jumla ya mabao 11 na saba kati ya hayo yamefungwa kipindi cha kwanza huku manne yakifungwa cha pili, jambo linaloonyesha wazi kikosi hicho kina balansi nzuri kwenye vipindi vyote viwili.
Hata hivyo, Simba ingefunga mabao mengi zaidi kipindi cha kwanza kama ingekuwa na utulivu wa kumalizia nafasi baada ya Ahoua kukosa dakika ya tisa na 11 na Kibu Denis dakika 16, ambazo ziliokolewa vyema na kipa wa Bravos, Landu Mavanga.
Bravos haikuwa na nguvu kubwa ya kutengeneza mashambulizi kipindi cha kwanza ikifika mara mbili pekee kwenye lango la Simba na kuufanya mchezo huo kwenda mapumziko kwa Wekundu wa Msimbazi kuongoza bao 1-0, ambalo lilidumu hadi mwishoni.
Pia kikosi hicho kimekuwa na rekodi tofauti kwani mchezo wa juzi umeifanya kufikisha michezo mitano bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga bao 1-0, C.R.D. Libolo, ambapo kati ya hiyo imepoteza miwili tu na kutoka sare mitatu.
Wakati rekodi zikionyesha Simba imekuwa hatari zaidi kufunga mabao mengi katika kipindi cha kwanza, kwa wapinzani wao hali ni tofauti kwani kwenye Ligi Kuu ya Angola ‘Girabola’, Bravos imeonyesha uhatari wa kufunga kipindi cha pili.
Katika mabao 11 ambayo timu hiyo imeyafunga saba yamefungwa kipindi cha pili huku manne pekee yakifungwa cha kwanza na ndicho ambacho Bravos ilikionyesha japo ulikuwa ni uimara wa Simba wa kutowapa nafasi za kuweza kuwaadhibu langoni mwao.
Uimara wa Simba katika kujilinda uliifanya Bravos kukosa njia mbadala ya kusawazisha bao hilo na kukifanya kikosi hicho kupoteza mchezo wa kwanza wa michuano ya CAF msimu huu, baada ya kufanya vizuri tangu ilipoanzia katika hatua za awali.
Bravo ilirejea tena jijini Dar es Salaam kwa mara ya pili msimu huu baada ya hatua ya awali kutoka suluhu na ‘Wagosi wa Kaya’ Coastal Union hivyo, kufuzu kwa jumla ya mabao 3-0, baada ya mechi yake ya kwanza ikicheza Angola kushinda kwa 3-0.
Baada ya hapo kikosi hicho kikakutana na FC Lupopo ya DR Congo na kilishinda kwa jumla ya mabao 3-1, na mchezo wa kwanza jijini Ango ilishinda bao 1-0, kisha mechi yake ya marudiano iliyopigwa huko Congo kikashinda tena mabao 2-1.
Licha ya miamba hiyo kutengeneza nafasi kadhaa na kushindwa kuzitumia, ila mchezo huo ulionekana wazi kubalansi kwa pande zote mbili kutokana na takwimu zao ambao Simba ilitawala zaidi kipindi cha kwanza huku Bravos ikiamka kipindi cha pili.
Kijumla Simba ilipiga mashuti 17 langoni wa wapinzani wao ingawa ni matatu tu yaliyolenga lango ‘Shot On Target’, huku kwa upande wa Bravos ikipiga mashuti 11 na manne pekee yakilenga lango, jambo linaloonyesha wazi mchezo huo ulibalansi.
Katika mchezo huo Simba ilipiga pasi 404 ambazo ni sawa na umiliki wa mpira kwa asilimia 54, huku kwa upande wa Bravos ikipiga pasi 352, sawa na asilimia 46, ingawa ni kikosi hicho cha Msimbazi kilichoweza kutumia vyema nafasi iliyoipata.
Katika matokeo mengine juzi ilishuhudiwa CS Constantine ya Algeria ikishinda bao 1-0, ugenini dhidi ya CS Sfaxien kutoka Tunisia na kulifanya kundi ‘A’ kuongozwa na Waalgeria hao wakifikisha pointi tatu sambamba na ilivyokuwa pia kwa Simba.
Kitendo cha CS Constantine kushinda ugenini kinazidisha presha zaidi kwa Simba wakati miamba hiyo itakapokutana katika mchezo wa pili wa hatua ya makundi utakaopigwa Desemba 8, kwenye Uwanja wa Mohamed Hamlaoui uliopo mji wa Constantine.
Ugumu wa mchezo huu unachagizwa na timu zote kushinda michezo yao ya kwanza na licha ya Simba kushinda nyumbani ila itakutana na upinzani mkubwa baada ya wenyeji wao Constantine kujiwekea mazingira mazuri baada ya kuanza vyema ugenini.
Baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids aliwapongeza wachezaji wa kikosi hicho kwa ushindi uliopatikana, huku akieleza licha ya kutocheza vizuri kipindi cha pili ila kuna kitu kikubwa wamejifunza na watakifanyia kazi mbeleni.
“Hatuwezi kucheza katika kiwango bora kila mchezo ila jambo muhimu na nzuri kwetu tumepata pointi tatu zinazozidi kutujengea hali ya kujiamini kwa wachezaji kijumla, tumejifunza kutokana na yaliyopelekea kuzidiwa kipindi cha pili.”