TIMU ambayo ilianza kuleta imani kubwa kijiweni msimu huu ni wazee wa ugali, Fountain Gate ambayo inacheza mechi zake za nyumbani za Ligi Kuu katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa kule Babati.
Jamaa walianza kwa kishindo sana Ligi Kuu msimu huu wakipata ushindi katika mechi nne kati ya sita za mwanzo, wakitoka sare moja na wakapoteza moja ambayo ilikuwa ya kwanza dhidi ya Simba.
Ile ya Simba kila mmoja hakuwashangaa kupoteza kwa sababu iliwakosa baadhi ya wachezaji wake ambao iliwasajili ili iwatumie msimu huu na wapinzani wao walikuwa na kikosi kizuri.
Hivyo walivyovuna pointi 13 baada ya kucheza na Simba na kile kiwango bora walichokuwa wakikionyesha uwanjani tuliamini ile timu italeta ushindani mkubwa kwenye ligi kuu msimu huu.
Hatukuamini kama ingeweza kutwaa ubingwa wa ligi au kumaliza katika nafasi ya pili lakini angalau basi iwepo katika nafasi nne za juu au ikishindwa kabisa iangukie katika nafasi ya tano .
Unajua Watanzania tulio wengi tunapenda Yanga na Simba mojawapo ndio iwe bingwa huo ndio uhalisia maana hizi ni timu za urithi, pia huwa tunatamani ziwepo timu nyingine ambazo zitafanya hizo mbili ziutolee jasho ubingwa.
Lakini ndani ya muda mfupi, Fountain Gate imeshuka na hapa tukiangalia msimamo wa Ligi Kuu Bara tunaiona ipo katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi tena ikizidiwa kwa pointi saba na timu iliyopo nafasi ya nne.
Jamaa zetu wa Fountain Gate wanatakiwa kupambana vilivyo katika mechi zilizo mbele yao ili wapate matokeo mazuri tuweze kuwaona wakiwa pale kwenye nafasi tano za juu katika msimamo wa ligi.
Hatutofurahia kuona wakiwa nguvu ya soda kama baadhi ya timu zilivyowahi kufanya miaka ya nyuma na zilianza vizuri halafu mwishoni zikaishia kuwa katika kundi la timu zinazopambana zisishuke daraja.