Askofu Ruwa’ichi atoa msimamo wa TEC uchaguzi serikali za mitaa

Dar es Salaam. Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) limeeleza kusikitishwa na matukio ya mauaji yaliyoripitiwa wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika nchini kote Novemba 27, 2024.

Kutokana na hilo, TEC limeitaka Serikali kuwajibika katika kuhakikisha inalinda wananchi wakiwemo wanasiasa nyakati zote. Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya TEC, Askofu Thadeus Ruwa’ichi wakati akizungumza na vyombo vya habari leo Novemba 28, 2024 jijini Dar es Salaam.

Askofu Ruwa’ichi ambaye alikuwa akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika nchini kote jana, Novemba 27, 2024, amesema matukio ya mauaji ya watu wawili yaliyotokea wakati wa mchakato huo yanapaswa kukemewa vikali.

Juzi, Novemba 26, 2024 kuliripotiwa tukio la aliyekuwa mgombea uenyekiti wa Kitongoji cha Stand katika Jimbo la Manyoni Mashariki mkoani Singida, George Mohamedi kuuawa kwa kupigwa risasi katika tukio lililodaiwa kuwahusisha wafuasi wa Chadema na wale wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Tayari Polisi Mkoa wa Singida, limetangaza kuwashikilia watu wawili akiwemo askari mmoja wa Jeshi la Magereza kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mgombea huyo kilichotokea Novemba 26, 2024 saa 5.00 usiku ikiwa ni saa kadhaa kabla ya upigaji kura kuanza.

Pia, limetangaza kuendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kuahidi wanaohusika wote watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Mbali na tukio hilo, mgombea ujumbe Mtaa wa Ulongoni A jijini Dar es Salaam, Modestus Timbisimilwa naye alidaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na askari polisi.

Hata hivyo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilitoa taarifa na kueleza kwamba, mgombea huyo alifariki dunia kutokana na kuugua shinikizo la damu na kwamba, madai yanayosambazwa mitandaoni hayana ukweli.

Akizungumzia matukio hayo, Askofu Ruwa’ichi amesema nchi inapita katika kipindi kigumu chenye maumivu hasa inaposhuhudiwa raia wakikatishwa uhai wao wakati wakipigania haki zao za msingi za kisiasa.

“Tunalaani kwa uwezo wote mauaji haya na mengine yoyote yanayowagusa raia wa nchi hii. Tunalaani kwa sababu yanakusudiwa na wauaji. Tukumbuke kuwa Mungu ndiye mwenye mamlaka ya uhai wa wanadamu wote. Hapa duniani hakuna mwenye mamlaka ya kuondoa uhai wa mwingine.

“Wajibu wetu ni kutetea, kulinda na kutunza uhai wa kila mwanadamu. Tunaonya jamii ya Watanzania kuacha hiyo tabia mbaya ambayo imeanza kujitokeza kwa kasi,” amesema Askofu Ruwa’ichi ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Ameeleza kushangazwa na ukimya wa Serikali ambayo imepewa mamlaka na wananchi, kutotimiza wajibu wake wa kulinda maisha ya watu kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Hatuoni wenye kusimamia sheria na usalama wakilinda uhai wa raia. Hatuwaoni wakilaani na kuonya. Tabia hii ya kuchukulia mauaji ya wanasiasa na raia kama jambo la kawaida, ni tendo linalosababisha kujengeka kwa tabia ya kupoteza na kuzembea katika kutunza uhai na haki ya mwanadamu.

“Hili tunalikuta katika Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wapo waliokabidhiwa jukumu la kulinda ibara hii na kuitekeleza,” amesema kiongozi huyo.

Askofu Ruwa’ichi amesema kutekeleza au kudai haki za kisiasa ni haki ya kila raia, na hilo likifanyika wakati wa uchaguzi, uwe wa serikali za mitaa au uchaguzi mkuu, siyo jambo la kuvunja sheria.

Amesisitiza Serikali inalo jukumu la kuonyesha kuzingatiwa kwa weledi katika hali iliyopo, watu wasijisikie kutishwa na vyombo vya ulinzi wakati wa maandalizi ya uchaguzi na wakati wa uchaguzi wenyewe.

“Ukatili dhidi ya wanasiasa na raia ni matendo maovu ambayo lazima yakomeshwe katika nchi yetu. Sisi sote ni ndugu na watoto wa Mungu muumbaji. Tuheshimu na kuzilinda amri za Mungu hasa kulinda uhai wa mwingine,” amesisitiza Askofu Ruwa’ichi.

Jana usiku, Novemba 27, 2024 akizungumza na vyombo vya habari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa alisema uchaguzi umekwenda vizuri huku amani na utulivu vikitawala.

Mchengerwa amesema uchaguzi wa mwaka huu (2024) umefanyika kwa mafanikio makubwa na kwamba, dosari ndogo ndogo zilizojitokeza zimepatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuhakikisha kila mwananchi anatimiza haki yake ya kupigakura.

“Uchaguzi wa mwaka huu umekwenda vizuri sana na tumefanikiwa kwa asilimia 98. Zipo changamoto ndogo ndogo zilizojitokeza kwenye baadhi ya maeneo machache na zimepatiwa ufumbuzi wa haraka na wananchi wakatimiza haki yao ya kupigakura. Huu ni uchaguzi ambazo amani na utulivu imetawala,” amesema Mchengerwa.

Related Posts