Camara ashtuka atoa kauli nzito

KIPA wa Simba, Moussa Camara amesema kiwango kilichoonyeshwa na Bravos do Maquis kipindi cha pili ni kama ujumbe kwao kujua jinsi ya kuongeza umakini na kujipanga zaidi katika mechi zilizopo mbele yao.

Camara alionyesha kiwango kizuri katika mchezo huo wa kwanza wa Kundi A katika Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa Novemba 27, 2024 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo ambao Simba ilishinda bao 1-0, Camara alidaka penalti ya Bravos do Maquis dakika ya 47 na kuiweka salama timu yake.

Kipa huyo raia wa Guinea, amesema michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ni migumu inahitaji kutumia zaidi nafasi za kufunga kutokana na ushindani ulivyo.

“Tulivyoanza kipindi cha kwanza tulipata nafasi nyingi za kufunga ni tofauti na kipindi cha pili ambacho nilipokea mashambulizi mengi golini kwangu, hilo linatufumbua akili, kujipanga kuhakikisha tunafanya vizuri mechi zijazo.

“Kiufundi kocha atakwenda kutuelekeza zaidi, kitu gani tunapaswa kukiongeza ama kupunguza, jambo la msingi kwa sasa tumepata ushindi, ambao unazidi kuongeza morali ya kujituma, ili tuzidi kupata ushindi na kufika mbali katika michuano hiyo,” alisema.

Desemba 8 mwaka huu, Simba itakwenda Algeria kucheza na CS Constantine, mechi ambayo Camara alisema wanahitaji maandalizi bora na kuwajua zaidi wapinzani wao, kitu anachokiamini kitawasaidia kupata ushindi.

“Michuano ya CAF inahitaji kutumia nafasi, tofauti na Ligi Kuu unaweza ukafanya makosa mengi lakini bado ukapata ushindi, huko CAF ukishindwa kutumia nafasi inakula kwako,” aliongeza.

Related Posts