CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu (CC), kujadili yaliyotokea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa ya chama hicho, iliyotolewa na John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, imesema kikao hicho, kitafanyika kesho Ijumaa, tarehe 29 Novemba.
Mrema anasema, kikao hicho, kitakachojadili agenda maalum inayotokana na yaliyojiri kwenye uchaguzi huo na “hatimaye kutoka na msimamo,” kitaongozwa na Freeman Mbowe, mwenyekiti wa taifa wa chama hicho.
Kinachoitwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake, “Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji,” ulifanyika jana Jumatano, tarehe 27 Novemba 2024.
Mapema jana, Chadema kilitoa taarifa kikieleza masikitiko yake na kilichotokea na kuendelea kutokea kwenye uchaguzi huo, ikiwamo mauaji ya wanachama wake watatu.
Wamewataja waliouawa kuwa ni pamoja na Modestus Timbisimilwa, George Juma Mohamed na Steven Chalamila. Taarifa zinasema, Timbisimilwa, aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi jijini Dar es Salaam. Alikuwa akijaribu kuzuia kura bandia kuingizwa kwenye vituo.
Naye George aliuawa kwa kupigwa risasi na Afisa wa Magereza mjini Manyoni, huku Chalamila, akishambuliwa kwa mapanga, nyumbani kwake mjini Tunduma.
Kwa mujibu wa Mbowe, matukio hayo yamefanyika kwa baraka na idhini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Taifa hilo la Afrika Mashariki, lilichagua zaidi ya viongozi 80,000 wa serikali za mitaa, ambao wana mamlaka makubwa katika maeneo yao.
Yaliyotokea katika uchaguzi huo, yanaakisi kitakachotokea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka kesho, wanaeleza wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini.