Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imepanga kufanya kikao cha dharura kesho, Ijumaa, Novemba 29, 2024 kujadili uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, uliofanyika nchini kote jana, Novemba 27, 2024.
Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Alhamisi, Novemba 28, 2024 na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, imesema kikao hicho kitaongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Mrema amesema kikao hicho kitajadili agenda maalumu yaliyojiri kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika jana Jumatano, Novemba 27, 2024.
“Kauli ya chama itatolewa baada ya kikao hicho kumalizika,” amesema Mrema.
Katika uchaguzi huo, baadhi ya mambo ambayo Chadema imekilalamikia ni matukio ya mauaji ya wagombea wake. Wagombea hao ni mgombea ujumbe Mtaa wa Ulongoni A jijini Dar es Salaam, Modestus Timbisimilwa anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na Polisi.
Mwingine ni aliyekuwa mgombea uenyekiti wa Kitongoji cha Stand katika Jimbo la Manyoni Mashariki mkoani Singida, George Mohamedi anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi.
Hata hivyo, Polisi Mkoa wa Dar es Salaam na Singida walizungumzia matukio hayo. Polisi walitoa ufafanuzi huo baada ya taarifa kusambaa mitandaoni zikiwemo zilizochapishwa na Mbowe kwenye akauti zake za kijamii kuzungumzia uchaguzi huo ikiwemo mauaji ya makada wake.
Katika chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii jana Jumatano, Novemba 27, 2024 Mbowe aliandika:“Tunapofunga vituo vya kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Taifa limeendelea kushuhudia tena ubaradhuli wa wazi na wa aibu kutoka kwa mamlaka zote za Serikali kushirikiana kuipatia CCM na wagombea wake ushindi wa aibu hata kwa gharama za maisha ya Watanzania.”
“Tunalaani mauaji na kujeruhiwa kwa wagombea, viongozi na wanachama wetu mbalimbali wakiwemo: Modestus Timbisimilwa, mgombea nafasi ya Ujumbe wa Serikali ya Mtaa wa Ulongoni A, Kata ya Gongolamboto, Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam aliyeuwawa na askari kwa kupigwa risasi, wakati wa purukushani za kuzuia kura bandia na batili kuingizwa kituo cha kupiga kura.”
Katika ufafanuzi wake, Kamanda wa Jeshi hilo Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema Timbisimilwa alifariki kwa kuugua presha.
Alipoulizwa Kamanda Muliro kuhusu tukio hilo pamoja na matukio mengine alisema mgombea huyo alifariki kwa kuugua presha (shinikizo la damu) na kinachosambazwa mitandaoni hakina ukweli.
“Ukweli ni kwamba hakuna kitu kama hicho, tofauti na inavyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, alikuwa anaumwa presha, amekufa na ufafanuzi utatolewa,” alisema Muliro jana jioni alipotafutwa na Mwananchi.
Katika maelezo yake Muliro alisema mtu huyo alikuwa na rekodi ya ugonjwa wa presha na baada ya kwenda katika kituo hicho alikuwa anaomba maji kwa wafuasi wa Chadema.
“Watu wa Chadema walishauri asipewe maji isipokuwa awahishwe zahanati baada kufikishwa akawa amefariki dunia na amekuwa na rekodi ya kuwa na ugonjwa wa presha,” amedai Muliro.
Tukio la Singida, Polisi mkoani humo lilisema linamshikilia askari mmoja wa Jeshi la Magereza kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mgombea huyo kilichotokea Novemba 26, 2024 saa 5.00 usiku.
Taarifa hiyo ya Polisi ilisema; “Chanzo cha tukio hilo ni kwamba katika eneo hilo wafuasi wa CCM walikuwa kwenye kikao cha ndani katika nyumba moja.
“Wakati kikao hicho kikiendelea walivamiwa na kundi la wafuasi wa Chadema na vurugu kutokea, ambapo askari Magereza ambao wapo kwenye moja ya Gereza lililopo jirani na eneo hilo walitaarifiwa na haraka wakafika eneo hilo kuona hali ilivyo.
“Wakati askari hao wanakwenda kwenye eneo hilo waliwasiliana na polisi, walipofika eneo la tukio walianza kushambuliwa kwa mawe jambo lililowalazimu kupiga risasi hewani kutuliza purukushani hizo na risasi moja ilimjeruhi Mohamedi (41), ambaye alikuwa mgombea wa kitongoji cha Stendi kupitia Chadema.”
Kingine ambacho Chadema walikilalamikia jana Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na Mrema ni kukamatwa ama kuonekana kwa kura zilizopigwa nje ya mfumo rasmi. Chadema ilibainisha maeneo ambayo karatasi zilikamatwa ni Chato (Geita), Bariadi Mjini (Simiyu), Msalala na Kahama Mjini (Shinyanga), Kilosa (Morogoro), Igunga (Tabora) na Segerea (Dar es Salaam).
Hata hivyo, alipoulizwa Mwanasheria Mwandamizi wa Tamisemi, Mihayo Kadete alisema kama wamebaini changamoto hiyo na wanaudhibitisho malalamiko yao wapeleke kwa msimamizi msaidizi wa kituo cha kupigia kura.
“Kama wamebaini changamoto ya kura za namna hiyo wawasiliane na wasimamizi wasaidizi wa kituo cha kupigia kura kwa hatua zaidi zichukuliwe,” alisema Kadete