Familia ya Dk Ndugulile yatoa neno, wananchi Kigamboni wakisema…

Dar es Salaam. Wananchi wa Wilaya ya Kigamboni wamesema aliyekuwa Mbunge wao (CCM) na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile amefariki dunia kama shujaa aliyewapigania wakati wote bila kuchoka.

Wananchi hao wametaka atakayerithi mikoba hiyo kuendeleza mema aliyoanzisha na kuwatatulia changamoto zinazowakabili ikiwemo miundombinu ya barabara na maboresho ya vivuko.

Dk Ndugulile aliyeongoza jimbo hilo tangu mwaka 2010, alifikwa na mauti usiku wa kuamia jana Jumatano, Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu. (Bado haijafahamika ugonjwa uliokuwa unamsumbua).

Mwili wake unatarajiwa kuwasilia Tanzania katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kesho Ijumaa Novemba 29, 2024 na ukitarajiwa kuzikwa Jumanne ya Desemba 3, 2024, Kigamboni.

Leo Alhamisi, Mwananchi limefika nyumbani kwa Dk Ndugulile (55) na kukuta waombolezaji mbalimbali na kupata wasaa wa kuzungumza nao ikiwemo wanafamilia ambao wameelezea hatua zake za mwisho kabla ya kusafiri kwenda India.

Mmoja wa wanafamilia hiyo, Gerald Ndugulile amesema marehemu baba yao ameacha mjane na watato wawili wote wanasoma.

“Mara mwisho alikuja mbele ya familia na mama yake mzazi akiwa anacheka kuaga anakwenda nchini India kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa afya yake kuajiandaa na majukumu yake mapya aliyotarajia kuanza kuyatumikia kuanzia Februari 2025,” amesema Gerald.

Gerald ambaye marehemu Dk Ndugulile alikuwa baba yake mdogo, amesema akiwa nchini India walikuwa wanawasiliana mara kwa mara kupitia kundi la WhatsApp la familia na alikuwa asema anaendelea vizuri.

“Alikuja kwa bashasha kubwa akiwa na afya yake na hakuonyesha dalili yeyote ya ugonjwa na hata kwenye group la familia tulikuwa tunachati kama kawaida. Taarifa za kifo chake kama familia zimetushitua na tunaumia,” amesema.

Gerald amesema kimekuwa kifo cha ghafla katika kipindi ambacho familia hiyo ilikuwa inamuhitaji zaidi kwakuwa alikuwa nguzo katika kuunganisha ukoo wa Ndugulile.

“Tumeguswa zaidi kama familia,” amesema Gerald.

Katika hatua nyingine, Msemaji wa familia, Wilibart Ndugulile amesema mwili wa kaka yake utawasili kesho majira ya saa 6:30 mchana Uwanja wa Ndege kutoka India.

“Ratiba itaanza hiyo kesho Novemba 29 hadi Desemba tatu baada ya mwili kupokewa utapelekwa Hospitali ya Lugalo kuanzia Novemba 30 tutaendelea na maombolezo na Desemba mbili mwili utatolewa Lugalo kupelekwa Kanisa la Mtakatifu Magreth Upanga kwa ibada,” amesema.

Amesema baada ya kutoa hapo kanisani mwili utaelekea viwanja vya Karimjee kwa ajili ya shughuli za kitaifa na baadaye mwili utaletwa hapa nyumbani utalala hapa Desemba tatu mwili utapelekwa Kanisa letu la Kigamboni kisha kupelekwa viwanja vya Machava ili wananchi wapate fursa ya kuaga,” amesema.

Wilibart amesema baada ya hapo wataenda kuupumzisha mwili kwenye makazi yake ya milele Katika Makaburi ya Mwongozo Kigamboni.

‘Ameondoka kama shujaa’

Salum Kaberega amesema kuna mambo aliyowasidia kama kuwasogezea huduma za afya lakini kuna mambo ambayo tunahitaji utatuzi wa kina zaidi.

“Kuna miundombinu ya barabara bado nyingi ni mbovu na tunaelekea msimu wa mvua huwa hazipitiki, kama bateti zimetengwa basi zijengwa.

“Suala la wananchi wasilipie wanapovuka daraja la kigamboni alikuwa akilisemea lakini bado kilio hakijasikika, tunatamani kuona hilo pia linafanyiwa kazi,” amesema Kaberega.

Kwa upande wake, Helina Peter amesema kifo chake kimekuwa pigo kwao huku akieleza aliwatumikia kwa uadilifu.

“Ni matumani mwakilishi ajaye atakuja kuendeleza mema yote na kuanzisha mapya kwa maslahi ya Wanakigamboni kote, mbunge wetu kaondoka kama shujaa ambaye hakuchoka kutupigania,” amesema.

Madiwani watakavyomkumbuka

Meya wa Manispaa ya Kigamboni, Ernest Mafimbo amesema walipenda utumishi wake uliotukuka kwa awamu tatu katika kuwatumikia wananchi wa kigamboni katika nafasi ya ubunge.

“Sasa alikuwa anaelekea kuiwakilisha nchi katika nafasi mpya katika Shirika la Afya kwa Kanda ya Afrika, kiujumla tumeumia zaidi, ni tukio lililonje ya uwezo wetu Wanakigamboni tutaendelea kuyaenzi yale yote mema aliyoyafanya,” amesema.

Mafimbo amemzungumzia marehemu wakati wa uhai wake alikuwa kiongozi mwenye sifa ya misimamo isiyoyumbishwa na alikuwa amenyooka siku zote.

“Hakuwa anapenda kona kona au kupindisha kitu sehemu ambayo jambo linatakiwa kwenye mfumo fulani basi alikuwa anasimamia hiyo ilikuwa ni tabia yake hata katika vikao vyetu vya manispaa,” amesema.

Amesema alikuwa kiongozi mwepesi katika kutoa ushauri walipokuwa wanamwendea na wakati mwingine ilikuwa nje ya ofisi walikuwa wanakaa na kujadiliana na kupata mwelekeo.

“Alikuwa mtu shirikishi na hakuwa amejitenga na baraza la madiwani pamoja na kwamba alikuwa waziri na naibu waziri kwa nyakati tofauti muda wote tulikuwa tunampata,” amesema.

Amesema amepita nyakati ngumu na wananchi wake tangu kupata Wilaya ya Kigamboni hadi kupata vivuko vilivyopo sasa tofauti na ilivyokuwa nyuma.

“Amepigania miundombinu ya barabara na vituo vya afya katika kila kata tunakituo cha afya, ukizingatia ni mtaalamu wa eneo hilo alikuwa mfuatiliaji zaidi,” amesema.

Naye, Diwani wa Mji Mwema Kigamboni, Omary Ngurangwa amesema kifo cha kiongozi huyo ni nuru iliyofutika huku akieleza hakuwa mbinafsi alikuwa anataka kuona maendeleo ya wananchi wake.

“Nikiongozi ambaye alikuwa anajifanyia tathimini mwenyewe kwa kueleza amefanikiwa sehemu fulani na amekosea jambo fulani na ni mambo yaliyokuwa yanamsumbua kila kikao alikuwa anazungumzia,” amesema

Amesema ” alikuwa anapambana wananchi wakigamboni wawe wanaingia na kutoka bila kulipa gharama wanapovuka daraja alikuwa wanastahili kupata huduma hiyo bure kama wananchi wengine,” amesema

Amesema moja ya ndoto yake ilikuwa kuona daraja linapitika bila malipo kama ilivyodaraja la Tanzanite.

“Ndoto yake nyingine vivuko vinaingia katika uendeshaji wa sekta binafsi na alikuwa akiishauri Serikali na alipokuja Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa alizungumzia utayari wa serikali wa kufanya ubia huo ili kuhakikisha vivuko vinaboreshwa,” amesema.

Amesema ndoto nyingine iliyokuwa inamsumbua na mrithi wake atakayekuja anapaswa kuitendea haki ni kuhakikisha hali ya kivuko inatengemaa na alitaka Kigamboni ije kuwa mji wa kisasa unaozingatia taratibu za mipango miji.

“Alikuwa anaumia kwanini tunafukwe zaidi ya kilomita 50 lakini hazitoi tija kwa ajili ya kuongeza mapato ya ndani na serikali,” amesema.

Related Posts