Gachagua anusurika kujeruhiwa msibani, gari yake yapasuliwa kioo

Kenya. Vurugu zimeibuka baada ya watu wasiojulikana kutaka kumdhuru aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua akiwa katika mazishi katika Kaunti ya Kiambu nchini Kenya leo Novemba 28, 2024.

Katika maelezo yake, Gachagua amedai kuwa watu hao waliomfanyia vurugu ni maofisa wa Serikali ya Kenya.

Gari la Gachagua lilipigwa mawe na dirisha la nyuma likavunjika, huku waombolezaji kadhaa wakipata majeraha.

“Wahalifu hao waliokodiwa walikuwa wakinilenga. Jiwe kubwa lililovunja dirisha la gari langu lilielekezwa kwangu. Nilikuwa na bahati sijapata madhara,” Gachagua amesema katika mahojiano maalumu na mtandao wa Nation.Africa.

Mvutano huo unajiri huku kukiwa na malalamiko yaliyoanza baada ya Gachagua kuondolewa madarakani na uteuzi wa Profesa Kithure Kindiki kama Naibu Rais, hali inayoongeza joto la kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027.

Gachagua aling’olewa madarakani baada ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye na wabunge wa Bunge la Kitaifa na kisha Bunge la Seneti, Oktoba mwaka huu.

Gachagua amewatuhumu wapinzani wake wa kisiasa kwa kupanga shambulio hilo, akihusisha tukio hilo na kumuondoa madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani mwezi Oktoba na pia kwa chaguzi za 2027.

“Hii ni mbinu ya kunikatisha tamaa kutoka kwa wale ambao tuna matatizo nao kwa ajili ya 2027 ili kunitisha nisiweze kuzungumza na watu wangu, kuwasiliana na Wakenya, na kushiriki juhudi za kuokoa nchi hii,” amesema.

Tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Bibirioni, jimbo la Limuru, wakati wa mazishi ya Erastus Nduati, mwenye umri wa miaka 23. Gachagua alikuwa bado hajazungumza na waombolezaji wakati ghasia zilipoanza.

Inaelezwa vijana hao walioanzisha vurugu hema alilokuwa amekaa Gachagua na wageni wengine.

Wakati vurugu zinaanza, Mbunge wa zamani wa Limuru, Peter Mwathi alikuwa ameanza kuongea masuala ya kisiasa na ghafla sauti ilizimwa na kusababisha vurugu.

Wakati ibada ikiendelea, vijana walijaribu kuvuruga shughuli hiyo mara mbili, lakini viongozi wa kidini waliweza kutuliza hali.

Hata hivyo, mvutano uliongezeka Mwathi alipotoa matamshi yaliyohisiwa kuwa ya uchochezi, ikiwemo kutaja mikakati ya kisiasa ya Gachagua kwa ajili ya 2027 na kumhimiza azungumze kwa lugha ya kabila lake hadharani.

Katika vurugu hizo, walinzi wa Gachagua walimkinga na kumwongoza hadi kwenye gari lake, ambalo lilishambuliwa wakati akiendesha kuondoka eneo hilo.

Viongozi waliokumbwa na ghasia

Viongozi wengine waliokuwapo wakati wa ghasia hizo ni pamoja na Mbunge wa Limuru, John Kiragu, Seneta wa Kiambu, Karungo Wa Thang’wa, Mbunge wa Kajiado Kaskazini Onesmus Ngogoyo, Mbunge wa Mukurweini John Kaguchia, Seneta wa Kajiado Seki Lenku pamoja na wajumbe kadhaa wa Bunge la Kaunti.

Washirika wa Gachagua wamewatuhumu wafuasi wa Rais William Ruto kwa kupanga vurugu hizo.

“Hii ilikuwa shambulio lililopangwa tangu Jumapili iliyopita. Lengo lilikuwa Gachagua. Lilianza kwa kuondoa walinzi wake ili kumwacha kwenye hatari,” alisema Seneta Karungo Wa Thang’wa.

Thang’wa amedai kuwa shambulio hilo lilikuwa jaribio la kuonyesha hali ya wasiwasi katika eneo la Mlima Kenya, akisisitiza kuwa ilikuwa juhudi za makusudi za kupunguza ushawishi wa Gachagua.

Fukuto lazidi Mlima Kenya

Shambulio hilo ni mfululizo wa mivutano ya kisiasa inayoshuhudiwa katika eneo la Mlima Kenya. Rais Ruto na wafuasi wake wamekuwa wakikumbana na upinzani mkali katika mikutano ya hadhara, ikiwemo kuzomewa wakati wa ziara yake ya hivi karibuni katika Kaunti ya Embu.

Imetafsiriwa kutoka Nation.Africa.

Related Posts