Mbeya. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya imeahirisha shauri la Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mdude Nyagali hadi kesho Novemba 29, 2024 saa 8.00 mchana.
Hatua hiyo imefuatia baada ya kuwepo kwa mvutano wa hoja za pingamizi baina ya mleta maombi na mjibu maombi kutokana na kesi ya msingi ya kutaka aachiwe huru au kufikishwa mahakamani.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mussa Pomo ameahirisha shauri hilo lililopangwa kusikilizwa leo Novemba 28 mahakamani hapo.
Shauri hilo namba 33247/2024 lilifunguliwa Novemba 26, mwaka huu na mawakili wa mleta maombi, Boniface Mwabukusi akishirikiana na Philipo Mwakilima .
Awali, Wakili mwandazi wa Serikali, Simon Peres ameeleza mahakamani hapo hoja ya pingamizi za kiapo zilizowasilishwa na mleta maombi hazionyesha mazingira ushahidi wa kutosha kuwa alikuwa kwenye msafara wa Chadema.
“Mheshimiwa Jaji maneno yaliyowasilishwa kwenye kiapo ni uongo hayajaonyesha kushuhudia mleta maombi kupigwa na kuteswa na hivyo naomba Mahakama kutupilia mbali kwa kuwa hayana mashiko,” amesema.
Wakili Peres ameieleza mahakama kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 390 na 391 pamoja na kanuni maombi ya mleta maombi lazima yawe na kiapo sahihi kwa mujibu wa sheria
Amesema kukinzana kwa kiapo kunapelekwa mwombaji kukosa sifa sahihi kwa kutokuwa na vyanzo sahihi vya taarifa na kuomba mahakama kutupilia mbali ombi hilo.
Kuhusu kuendelea kumshikilia Mdude
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Simon Peres amesema bado wanaendelea kumshikilia kwa zaidi ya masaa 48 huku akieleza kuendelea na uchunguzi kufuatia kuwa na makosa mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Tunaendelea na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakami licha ya Mahakama kutaka kuharakishwa kwa mchakato kama ana hatia afikishwe mahakamani kwa mujibu wa sharia,”amesema.
Kwa upande wa waleta maombi.
Awali wakili kiongozi wa mleta maombi Bonifasi Mwabukusi aliomba mahakama kumwachia huru au kumfikisha mahakamani mteja wao kwa sababu anashikiliwa kinyume cha utaratibu.
Pia ameomba mahakama kutoa amri yoyote kwa wajibu maombi kuhakikisha sheria inafuatwa dhidi ya mwombaji kutokana na kutojua aliko na hali ilivyo kwa sasa kufuatia vipigo na mateso aliyopata.
Wakati huohuo Wakili Mwabukusi aliwasilisha hoja tatu ikiwepo wajibu maombi kumshikilia Mdude kinyume cha muda masaa 48 waliopewa kisheria
Hoja nyingine ni pamoja na kiapo chao chote hakijaeleza mfumo walizingatia na misingi na sheria za kuendelea kumshikilia kama ilivyo bainishwa kwenye kifungu cha sheria 32 kidogo cha (i) na (ii) cha makosa ya jinai iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022 kifungu cha 67.
Baada ya kuwasilisha hoja hizo Mwabukusi ameomba Mahakama kumwamuru mjibu maombi kumfikisha mahakamani mleta maombi ili wathibitishe uhalali wa kumshikilia Mdude tangu Novemba 22 mwaka huu.
Awali mleta maombi Wakili Philipo Mwakilima ameileza mahakama kuwa maombi yaliyowasilishwa ya kweli na kuomba Mahakama kutoa amri ya kuletwa mahakamani kwa mteja wao.
Mwakilima ameileza mahakama kuwa suala lingine wajibu maombi wamemzuia mleta maombi kuwasiliana na mawakili wake.
Kufuatia maelezo yaliyotolewa na pande zote mbili za waleta maombi na wajibu maombi Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mussa Pomo ameahirisha shauri hilo mpaka kesho Novemba 29, 2024 saa 8.00 mchana.
Awali, Mdude alikamatwa Novemba 22 akiwa na miongoni mwa viongozi wengine wa Chadema walioshikiliwa na Polisi Mkoa wa Songwe akiwamo Mwenyekiti wake Taifa, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyansa, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.
Hata hivyo makada wengine wa chama hicho waliachiwa kwa dhamana huku Mdude akiendelea kushikiliwa mpaka sasa Novemba 28 mwaka huu. Mwisho.