Mashambulizi hayo ya jeshi la Israel dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah yameripotiwa maeneo ya kusini katika vijiji vya Markaba, Wazzani, Kfarchouba, Khiyam, Taybe na tambarare zinazotumiwa kwa shughuli za kilimo karibu na Marjayoun. Kutokana na vurugu hizo, jeshi la Israel limetangaza amri ya kutotoka nje usiku katika eneo la kusini mwa Lebanon.
Hayo yanajiri wakati pande zote mbili zimetupiana lawama za kukiuka makubaliano hayo ya usitishwaji mapigano yaliyoanza kutekelezwa jana asubuhi na yaliyotumainiwa kuvimaliza vita vya zaidi ya mwaka mmoja kati ya Israel na kundi la Hezbollah huko Lebanon.
Wakati huohuo, serikali ya Lebanon imewapeleka wanajeshi na vifaru katika maeneo hayo ya kusini katika hatua ya kutekeleza makubaliano hayo ambayo kulingana na vifungu muhimu, jeshi la Lebanon na walinda amani wa Umoja wa Mataifa UNIFIL ndio pekee walipaswa kuwepo kusini mwa Lebanon.
Israel imesema Hezbollah imekiuka makubaliano hayo baada ya wapiganaji wake kusalia eneo hilo ambapo kadhaa wamearifiwa kukamatwa. Kundi hilo kupitia mbunge wake Hassan Fadlallah limewatuhumu wanajeshi wa Israel kwa kuwashambulia raia wanaorejea kwenye makazi yao. Jeshi la Israel limesema litaendelea kuwepo kusini mwa Lebanon na wataondoka kwa awamu.
Israel yakabiliwa na shinikizo la uamuzi wa ICC
Katika mzozo wa Gaza ambapo Israel imeendeleza mashambulizi katika Ukanda huo na makumi ya watu wakiripotiwa kuuwawa, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anaendelea kukabiliwa na shinikizo kutokana na waranti wa kukamatwa kwake uliotolewa na Mahakama ya kimataifa ya Uhalifu ICC, ambapo Mkuu wa sera za Kigeni wa Umoja wa UIaya anayemaliza muda wake mwishoni mwa mwezi huu Josep Borrell amesema ni lazima mataifa ya Ulaya yaheshimu uamuzi wa mahakama hiyo.
” Nataka kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na hasa kwa wanachama wa Umoja wa Ulaya. Hatuwezi kuidhoofisha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu. Ndiyo njia pekee ya kuwa na misingi ya haki ulimwenguni na kutekeleza sheria za kimataifa. Ikiwa Ulaya haitoiunga mkono kikamilifu mahakama ya kimataifa ya ICC bila kuyumbishwa, basi Mahakama hiyo haiwezi kufanya kazi.”
Soma pia: Israel yaendelea kuishambulia Hezbollah licha ya mpango wa usitishwaji mapigano
Israel imesisitiza mara kadhaa kuwa itakata rufaa dhidi ya waranti huo wa kukamatwa Netanyahu na aliyekuwa waziri wa ulinzi Yoav Gallant ambao wanashutumiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu kutokana na mzozo wa Gaza. Akiwa ziarani Jamhuri ya Czech, waziri wa mambo ya nje wa Israel Gideon Saar amesema anaamini kuwa Marekani itaiadhibu Mahakama ya ICC kwa kuchukua uamuzi huo.
Vyanzo: (DPAE, AFP, APE)