Dar es Salaam. Uongozi wa Kanda ya Afrika wa WHO uko njia panda kufuatia kifo cha Mkurugenzi Mteule, Dk Faustine Ndugulile, kilichotokea usiku wa kuamkia Novemba 27, 2024.
Kifo chake kimeibua maswali kuhusu mchakato wa mpito wa uongozi ndani ya WHO Kanda ya Afrika na nani atakayeingia kujaza nafasi hii muhimu.
Chanzo kilichozungumza na gazeti dada la The Citizen, kilithibitisha kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Mkurugenzi Mteule kufariki kabla ya kuchukua rasmi nafasi ya uongozi na kiliahidi kwamba taarifa rasmi itatolewa hivi karibuni.
Dk Ndugulile (55) alitarajiwa kuanza rasmi jukumu lake la mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Machi 2025, baada ya kipindi cha mpito. Uchaguzi wake ulikuwa sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha juhudi za WHO katika kukabiliana na changamoto za kiafya barani Afrika.
Dk Ndugulile, ambaye ni Naibu Waziri wa zamani wa Afya na mtaalamu mashuhuri wa afya, aliteuliwa Agosti 2024 kuongoza WHO Kanda ya Afrika, nafasi iliyotazamwa kama hatua kubwa katika kazi yake ya kitaaluma.
Habari za kifo chake zimeacha pengo kubwa, siyo tu kwa familia yake bali pia kwa jamii ya afya kimataifa.
Kabla ya kuchaguliwa kwake kwa nafasi ya WHO, Dk Ndugulile alikuwa kiongozi muhimu katika maendeleo ya sera za afya za Tanzania, hasa katika maeneo ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza, miundombinu ya afya na upatikanaji wa huduma za afya kwa jamii zisizojiweza.
Uongozi wake ulikuwa muhimu katika kuimarisha mifumo ya afya ya Tanzania na kukuza ushirikiano na mashirika ya kimataifa yanayolenga kuboresha afya barani Afrika.
Urithi wa uongozi katika afya ya umma
Kifo cha ghafla cha Dk Ndugulile kimewaacha wengi wakitafakari juu ya urithi ambao angeendelea kuujenga kama Mkurugenzi wa Kanda wa WHO Afrika.
Alikuwa ameainisha vipaumbele kadhaa kwa kipindi chake cha uongozi, ikiwemo kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, kuimarisha maandalizi kwa dharura za kiafya na kuendeleza ushirikiano wa kina na taasisi mbalimbali za afya.
Alipanga pia kuleta ushiriki zaidi wa mabunge ya Afrika katika shughuli za WHO, mtazamo wa kipekee aliokuwa akinuia kuingiza katika uongozi wake.
Katika kampeni yake ya kugombea nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ya WHO Afrika, alisisitiza umuhimu wa uongozi thabiti na wa maono katika sekta ya afya barani Afrika.
Alisema nchi za Afrika zinahitaji viongozi wanaochanganya uwezo wa kitaaluma na uzoefu wa kisiasa ili kukabiliana na changamoto kubwa za kiafya zinazolikumba bara hili.
“Ninaamini Afrika inastahili kiongozi anayeweza kuendesha sekta ya afya mbele, hasa tunapokaribia hatua za mwisho za Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs),” alisema Dk Ndugulile wakati wa kampeni yake.
Pia alikiri ushindani mkubwa aliokutana nao kutoka kwa wagombea waliokuwa na uzoefu wa muda mrefu lakini alibaki na imani na uwezo wake wa kufanikisha kipindi chake cha miaka mitano, ambacho kinaweza kuongezwa kulingana na utendaji.
Viongozi wa afya duniani watoa rambirambi zao kufuatia habari za kifo cha Dk Ndugulile.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, alionyesha mshtuko wake kuhusu msiba huo, akiandika kwenye X (zamani Twitter):
“Nimeshtushwa na kuhuzunishwa sana na kifo cha ghafla cha Dk Faustine Ndugulile, Mkurugenzi Mteule wa Kanda ya Afrika wa WHO. Rambirambi zangu za dhati kwa familia yake, Bunge na watu wa Tanzania.”
Dk Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa sasa wa WHO Kanda ya Afrika, pia alielezea huzuni yake akisema:
“Dk Ndugulile alikuwa kiongozi mwenye maono ambaye alijitolea maisha yake kuboresha afya ya umma barani Afrika. Kifo chake ni pigo kubwa kwa bara la Afrika na jamii ya afya duniani. Mawazo yetu yako pamoja na familia yake, marafiki zake na wote walioguswa na maisha yake.”
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliungana na waombolezaji, akitambua mchango mkubwa wa Dk Ndugulile katika sekta ya afya wa nchi na kujitolea kwake kwa dhati katika kuboresha matokeo ya afya barani Afrika.
“Kifo cha Dk Faustine Ndugulile ni pigo kubwa siyo tu kwa Tanzania bali pia kwa bara la Afrika zima,” alisema Rais Samia.