Kutokuwepo kwa uwiano wa kodi kati ya Tanzania na nchi jirani kunatajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazosababisha mazingira yasiyo sawa, hivyo kuchochea usafirishaji wa dhahabu kwa magendo, wataalamu na wadau wameeleza.
Licha ya juhudi za Serikali kudhibiti biashara ya dhahabu, kiasi kikubwa cha dhahabu ya Tanzania kinapita nje ya masoko rasmi, hatua inayovujisha mapato ya nchi na kudhoofisha maendeleo ya kiuchumi.
Agosti 22 mwaka huu Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema wachimbaji wadogo wa dhahabu ndio wanaongoza kwa utoroshaji wa madini nchini na kuikosesha serikali mapato kwa kushindwa kutoza kodi.
Alisema kutokana na vitendo hivyo, Wizara imelazimika kuunda kikosi kazi maalumu cha kupambana na utoroshaji wa madini ili kukomesha tatizo hilo ambalo linaikosesha nchi mabilioni ya shilingi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Madini, katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Machi 2024 Wizara kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali imefanikiwa kukamata madini ya aina mbalimbali, yenye thamani ya jumla ya Sh3.9 bilioni yaliyokuwa yakitoroshwa katika mikoa ya kimadini ya Geita, Songwe, Chunya, Kahama, Mbeya na Kilimanjaro.
Katika hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ilielezwa kuwa wanaofanya utoroshaji ni wachimbaji na wafanyabiashara wa madini wasio waaminifu na katika mwaka wa fedha uliopita, 157 walikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Nchi jirani, hususan Rwanda na Uganda, zinatajwa kutoza kodi ndogo kwa mauzo ya dhahabu ikilinganishwa na Tanzania.
Mathalani, Rwanda imeibuka kama eneo linalowavutia wafanyabiashara wa dhahabu kwa kutoza asilimia 0.5 tu kama ushuru wa mauzo ya nje na asilimia 0.5 kama mrabaha, kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Rwanda.
Mapitio yao waliyoyafanywa Julai 2024, yameongeza mvuto kwa dhahabu ya magendo kutoka nchi jirani, ikiwemo Tanzania.
Vivyo hivyo, Uganda inatoza asilimia 2 pekee. Kwa kulinganisha, wafanyabiashara wa Tanzania hulipa jumla ya asilimia 8.7 katika masoko ya kawaida au asilimia 6.3 wanapouza kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Tofauti hii ni kichocheo kikuu cha biashara haramu.
Mtafiti na mchambuzi wa masuala ya uchumi, Profesa Abel Kinyondo anasema vitendo hivyo vipo nchini Tanzania na watu hivi sasa wana akaunti za pesa katika mataifa tofauti ya nje ili kuficha ukwasi wao.
“Watoroshaji wa dhahabu wanakimbilia Rwanda kwa kuwa kule kuna pepo ya kodi (Tax heaven), hususan kwa bidhaa za madini, hawana madini lakini wana vinu vya kuchenjua (refinery), hivyo wanavutia kila bidhaa ya madini nchini mwao,” anasema.
Profesa Kinyondo anasema utoroshaji wa dhahabu huwaathiri hata watoroshaji wenyewe, kwani nchi ingepata mapato stahiki yangetumika kuleta maendeleo ya huduma ambazo nao wangezifaidi.
“Athari za utoroshaji wa dhahabu ni nyingi, zinawahusu hata watoroshaji wenyewe kwa kuwa ukusanyaji wa Serikali unaathirika, hivyo utoaji wa huduma za jamii unazorota,” anasema Kinyondo, ambaye ni mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Anasema utoroshaji unasababisha kupotea kwa mapato, unasababisha Serikali kutafuta vyanzo vipya vya mapato, ikiwa ni pamoja na kuongeza kodi au kukopa. “Serikali ikichukua mkopo utalipwa hata na kizazi cha aliyetorosha dhahabu”
Hata hivyo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inasisitiza kuwa sera zake za kodi si mzigo mkubwa. Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipakodi na Mawasiliano wa TRA, Richard Kayombo, kodi ya mauzo ya dhahabu ilipunguzwa kutoka asilimia tano hadi mbili mwaka 2023, hivyo kufanya ulipaji wake kuwa rahisi.
“Wafanyabiashara wengi sasa wanalipa kodi zao kama inavyotakiwa,” Kayombo anasema. Hata hivyo, anakiri sio rahisi kwa mamlaka hiyo kubaini kiasi halisi cha dhahabu inayosafirishwa kwa magendo na mapato yanayopotea.
“Wafanya magendo wanajiibia wenyewe na nchi yao. Kwanza wanafanya jambo ambalo ni hatari sana kwao. Wanaweza kudhulumiwa, kwani masoko wanayoyatumia siyo salama, lakini wao wanafanya biashara nayo,” anasema.
Kuhusu vitendo vya utoroshaji wa dhahabu, Mwenyekiti wa soko kuu la dhahabu Geita, George Paul anasema usafirishaji wa dhahabu kwa njia za panya hautamalizika kama TRA haitapunguza kodi, kwani wengi wanakwepa kodi kubwa zinazotozwa na Mamlaka ya mapato nchini TRA wakati nchi jirani zinatoza kidogo.
Anasema kwa sasa kodi zinazotozwa hapa nchini zinafikia asilimia 8.7 ya thamani ya dhahabu inayouzwa kwenye masoko ya kawaida na asilimia 6.3 pale inapouzwa kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kodi hiyo ni pungufu kwa iliyokuwa ikilalamikiwa muda mrefu ya asilimia 9.3 ambayo ilipunguzwa baada ya majadiliano na Serikali. Paul anadai kuwa TRA imekuwa ikipanga kodi bila kufanya tafiti na kushirikisha wafanyabiashara na matokeo yake yanapelekea wafanyabiashara kutafuta mbinu za kukwepa kodi ili wapate faida.
“Kodi hii ya 9.3 ni kubwa mno, kwa wiki mtu akitorosha kilo 10 ya dhahabu amekwepa kodi ya Sh190 milioni na ukweli ni kwamba njiani hakuna mtu anayekataa hela, ukitenga milioni 50 zinakutosha kuvuka hadi Rwanda, ukifika Rwanda unalipa asilimia moja tu mzigo wako unakuwa salama,” alisema Paul, wakati wa mjadala kupunguza kodi hiyo.”
Alisema ukweli ni kuwa mali inapatikana nyingi, lakini asilimia kubwa inatoroshwa, “soko la madini Geita lina wanunuzi wa dhahabu 70 lakini sio wote wanapata mali kwa sababu nyingi inatoroshwa,” anasema Paul.
“Watu wanataka utajiri wa haraka, mtu anawaza kwa nini nimpe Serikali Sh200 milioni wakati nikitoa Sh50 milioni naweza kuvuka na mzigo wangu ukawa salama na nakwambia Kamishna hakuna mtu asiyetaka pesa, huko njiani wanapita vizuri tu hadi wanafika Rwanda, lakini mkiboresha kodi hakuna atakayetorosha,” anasisitiza Paul.
Alitolea mfano wa tozo ya Wizara ya Madini akisema inatoza asilimia saba na wafanyabiashara wanalipa kwa kuwa Wizara ilikaa nao chini na kuwaelimisha pamoja na kujenga mahusiano mema, jambo ambalo TRA wameshindwa kulifanya na hivyo kuwa adui wa mfanyabiashara.
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo mkoani Geita (Mkoa unaosifika kwa uzalishaji wa Dhahabu) Gabriel Luhumbi akizungumza kwenye kikao hicho alisema mazingira rafiki ya kufanya biashara yatawafanya wafanyabiashara kulipa kodi kwa moyo na kuondoa utoroshaji.
“Taarifa nilizopata kwa wafanyabiashara wa dhahabu ni kuwa kodi inayotozwa Uganda kwenye dhahabu ni asilimia 2, jirani zetu Rwanda ni asilimia moja, lakini hapa nyumbani ni asilimia 9.3, kwa hali hii lazima utoroshwaji uendelee,” alisema Luhumbi.
Kwa mujibu wa Luhumbi, mwaka 2022 tani 430 za dhahabu zilitoroshwa Afrika na hii inatokana na wafanyabiashara kuangalia wapi penye unafuu ambako hata akilipa watapata faida.
Mwenyekiti huyo wa TCCIA ameishauri TRA kukaa na wadau na kufanya utafiti wa namna gani ya kuzuia utoroshaji, huku wakifanya jitihada za kuwavutia wafanyabiashara ili waone sababu ya kuchangia ukuaji wa uchumi badala ya kutorosha.
Hata hivyo, kuhusu kiwango cha kodi na utoroshaji, Profesa Kinyondo anasema tatizo linaweza hata lisiwe kiwango kikubwa cha kodi, bali ni tabia kama zilivyo tabia nyingine za uhalifu.
“Mwenye tabia atafanya tu hata kama utabadili viwango vya kodi, kwani mbona watu wanalipa kodi ya kampuni ya asilimia 30. Tatizo hapa ni kuwaeleza watu na waelewe umuhimu wa kulipa kodi sahihi na waone manufaa ya kufanya hivyo.