Ikiwa yatadumu, mapatano ya kusitisha mapigano yatamaliza karibu miezi 14 ya mzozo kati ya Israel na Hezbollah, ambao uliongezeka katikati ya Septemba kuwa vita vya jumla na kutishia kumuingiza mdhamini wa Hezbollah, Iran, na mshirika wa karibu wa Israel, Marekani, katika mzozo mpana zaidi.
Mkataba huo hauzungumzii vita vya Gaza, ambapo mashambulizi ya Israeli usiku wa manane kwenye shule mbili zilizokuwa makazi ya muda katika Mji wa Gaza yameua watu 11, wakiwemo watoto wanne, kulingana na maafisa wa hospitali.
Israel ilisema shambulio moja lililenga mplenga shabaha wa Hamas na lingine lililenga wapiganaji waliokuwa wanajificha miongoni mwa raia.
Amani hiyo nchini Lebanon inaweza kuwapa faraja raia milioni 1.2 wa Lebanon waliohamishwa na mapigano na maelfu ya Waisraeli walioondoka nyumbani mwao kando ya mpaka.
Zilikuwa siku 60 chafu na mbaya,” alisema Mohammed Kaafarani, mwenye umri wa miaka 59, ambaye alihamishwa kutoka kijiji cha Lebanon cha Bidias. “Tulifikia hatua ambapo hakukuwa na mahali pa kujificha.”
Soma pia: Mpango wa usitishwaji mapigano Lebanon umegubikwa na nini?
Mkataba ulioratibiwa na Marekani na Ufaransa, na kuidhinishwa na Israel jioni ya Jumanne, unahitaji kusitishwa kwa mapigano kwa muda wa miezi miwili na kuitaka Hezbollah kumaliza uwepo wake wa kijeshi katika kusini mwa Lebanon, wakati wanajeshi wa Israeli wanapaswa kurudi upande wao wa mpaka.
Maelfu ya wanajeshi wa Lebanon na walinda amani wa Umoja wa Mataifa watapelekwa kusini, na jopo la kimataifa litakaloongozwa na Marekani litafuatilia utekelezaji.
Israel inasema inabakiza haki ya kuishambulia Hezbollah ikiwa itakiuka masharti ya mkataba. Ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ilisema wanajeshi waliwakamata watendaji wanne wa Hezbollah, akiwemo kamanda wa eneo, ambao walikuwa wameingia katika eneo lisiloruhusiwa.
Israel bado inapambana na wapiganaji wa Hamas huko Gaza kufuatua mashambulizi ya kundi hilo ya kuvuka mpaka kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023.
Lakini Rais Joe Biden siku ya Jumanne alisema utawala wake utatia msukumo mwingine katika siku zijazo kwa ajili ya kusitisha mapigano huko na kuachiliwa kwa makumi ya mateka wanaoshikiliwa na Hamas.
Wafuasi wa Hezbollah watangaza ushindi licha ya uharibifu mkubwa
Israel inaweza kujivunia ushindi mkubwa katika vita hivyo, ikiwa ni pamoja na kuuawa kwa kiongozi mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah na wengi wa makamanda wake wakuu, pamoja na uharibifu wa miundombinu mikubwa ya wanamgambo hao. Shambulio tata lililohusisha milipuko ya pager na vifaa vingien vya mawasiliano vya Hezbollah, lilionyesha kiwango cha juu cha upenyaji ndani ya kundi hilo lenye usiri mkubwa.
Hezbollah imepoteza sifa zake nyingi ilizozipata kwa kupambana na Israeli hadi mkwamo katika vita vya 2006. Hata hivyo kundi hilo la wapiganaji wa Kishia bado liliweza kutoa upinzani mkali, na kupunguza kasi ya Israeli kusonga mbele huku wakirusha roketi nyingi, makombora na ndege zisizo na rubani kuvuka mpaka kila siku.
Soma pia: Viongozi mbalimbali wapongeza makubaliano ya usitishwaji vita Lebanon
“Huu ni wakati wa ushindi, fahari na heshima kwetu sisi, wa madhehebu ya Shia, na kwa Lebanon yote,” alisema Hussein Sweidan, mkazi anayerejea katika mji wa bandari wa Tiro. Milio ya risasi ya hapa na pale ilisikika kwenye mzunguko mkuu wa barabara jijini, huku madereva wakipiga honi na wakazi wakishangilia.
Israel ilifanya mashambulio makali hadi usitishaji mapigano ulipoanza kutekelezwa, na kulenga shabaha katika vitongoji vya kusini mwa Beirut ambavyo tayari vimeshambuliwa vikali kama Dahiyeh, ambapo Hezbollah ilikuwa na makao yake makuu. Wakazi wanaorejea katika mitaa yake iliyojaa vifusi Jumatano walionyesha kukaidi.
“Hatujali kuhusu vifusi au uharibifu. Tulipoteza riziki yetu, mali zetu, lakini ni sawa, yote yatarudi,” alisema Fatima Hanifa, akikumbushia ujenzi mpya uliofanywa baada ya vita vya 2006. “Itakuwa nzuri zaidi. Na ninamwambia Netanyahu kwamba umepoteza, na umepoteza, na umepoteza kwa sababu tumerudi na wengine (Waisraeli) hawakurudi.”
Walebanon wengine wanaikosoa zaidi Hezbollah, wakiishutumu kwa kuiingiza nchi hiyo iliyoharibiwa kiuchumi katika vita visivyo vya lazima kwa niaba ya mdhamini wake, Iran.
Soma pia: Israel na Lebanon zakubali masharti ya kusitisha vita
“Wanatudhibiti na hatuwezi kufanya chochote juu yake. Vita hivi viliua yeyote viliyemuua na sasa wanatuambia ni ushindi,” alisema kijana mmoja ambaye alikuwa akirejea kutoka nchi jirani ya Syria baada ya kuhamishwa kutoka jimbo la Bekaa mashariki. Alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, akihofia kuadhibiwa.
Baadhi ya Waisraeli wana wasiwasi kuwa mpango huo hauendi mbali vya kutosha nchini Israeli, na hisia zilikuwa za kujizuwia zaidi, huku Waisraeli waliokimbia makazi yao wakiwa na wasiwasi kwamba Hezbollah haijashindwa na kwamba hakukuwa na maendeleo yoyote katika juhudi za kuwarejesha mateka walioko Gaza.
“Nadhani bado si salama kurejea majumbani mwetu kwa sababu Hezbollah bado iko karibu nasi,” alisema Eliyahu Maman, ambaye alifurushwa kutoka mji wa kaskazini wa Kiryat Shmona, ambao uliathiriwa sana na miezi ya mapigano.
Watu wachache waliingia mjini humo siku ya Jumatano, wakikagua uharibifu kutoka na mashambulizi ya awali ya roketi. Jengo la maduka lamji huo, ambalo lilikuwa limeshambuliwa hapo awali, lilionekana kuwa na uharibifu mpya, na roketi lilichimba ardhini karibu na jengo la makaazi.
Inaweza kuchukuwa miezi kadhaa kwa jamii za Waisrael kurejea kwenye makaazi yao, ambayo mengi yameharibika pakubwa kutokana na mashambulizi ya roketi.
Chanzo: AP