Maeneo 57 Zanzibar yatambuliwa, kusajiliwa kupunguza migogoro ardhi

Unguja. Ili kupunguza na kuondoa changamoto za migogoro ya ardhi na kuwapatia wananchi haki ya matumizi ya ardhi kwa njia rahisi na salama, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeyatambua na kusajili maeneo 57.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Novemba 28, 2024 katika mkutano wa 17 wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani Zanzibar.

Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Zawadi Amour Nassor amesema kati ya maeneo hayo, 42 ni ya Unguja na 15 ya Pemba.

“Lengo la kufanya utambuzi na usajili wa ardhi ni kutambua umiliki na kusajili ardhi kwa eneo husika ili kupunguza na kuondoa kabisa changamoto za migogoro ya ardhi na kuwapatia wananchi haki ya matumizi ya ardhi kwa njia rahisi na salama,” amesema.

Alikuwa akijibu swali la mwakilishi Mwantatu Mbarak Khamis (nafasi za wanawake), aliyetaka kujua hali ya utambuzi wa ardhi ikoje kwa sasa na mikakati inayoendelea kupunguza changamoto na migogoro.

Naibu waziri ametaja miongoni mwa maeneo ambayo yametambuliwa ni Shakani, Meya, Paje, Jambiani, Konde, Utaani, Maungani na Makangale.

Kazi hiyo amesema inafadhiliwa na Mradi wa Mkurabita kupitia Tume ya Mipango.

Amesema kazi ya utambuzi na usajili wa ardhi ni endelelevu ambayo kwa kiasi kikubwa inasaidia kuwapatia wananchi haki ya matumizi ya ardhi kwa unafuu zaidi.

Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea kuandaa miradi ya kuimarisha upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya kuendeleza kazi ya utambuzi na usajili, ili ifanyike kwa ufanisi zaidi pamoja na kuongezeka kwa maeneo yaliyotambuliwa na kusajiliwa.

Naibu waziri huyo amesema hali ya utambuzi na usajili wa ardhi ya Zanzibar iko katika hali ya wastani, akieleza Serikali inaendelea kuimarisha mikakati ya upatikanaji wa haki ya matumizi ya ardhi kwa wananchi kupitia utambuzi.

Ametaja miongoni mwa mikakati hiyo ni kupunguza muda wa kumtambua mmiliki kutoka miezi mitatu hadi mwezi mmoja kwa kurekebisha kifungu cha sheria kupitia marekebisho ya sheria ya mwaka 2023.

“Marekebisho haya yatatoa fursa kwa wananchi wengi kusajili ardhi zao na kutumia katika shughuli za kujiimarisha kiuchumi,” amesema.

Amesema wizara kupitia Kamisheni ya Ardhi imeshaandaa Mfumo wa Usajli wa Taarifa za Ardhi (LARIS) nchini ambao mbali na mambo mengine, una sehemu ya utambuzi wa ardhi kuhakikisha ardhi yote ya Zanzibar inatambuliwa na kusajiliwa.

Related Posts