Dar es Salaam. Uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika juzi umewaibua wadau mbalimbali – vyama vya siasa, Kanisa Katoliki na wengine wakiwa na maoni tofauti kuhusu mchakato huo.
Miongoni mwa wadau hao wamo wanaosema mchakato haukuwa huru na haki, ulighubikwa na kasoro zilizowakosesha ushindi na wengine wakisema ulikwenda vizuri na kuwa hakuna uchaguzi unaokosa kasoro.
Miongoni mwa kasoro zilizoripotiwa siku ya uchaguzi jana Jumatano, Novemba 27, 2024 ni pamoja karatasi za kura zilizopigwa kukutwa mitaani, kura kupigwa nje ya utaratibu, wananchi kukosa majina, kuzuliwa kwa mawakala na vifo vya watu watatu katika maeneo tofauti.
Hata hivyo, baadhi ya waangalizi wa uchaguzi huo waliozungumza na Mwananchi wamesema mchakato huo, ulikwenda vizuri ulinzi na usalama uliimarishwa.
Huku Chama tawala cha CCM kikifurahia kuzoa karibu viti vyote, vyama vinne vya upinzani – Chadema na ACT Wazalendo vimeitisha vikao vyake vya juu kujadili yaliyojiri katika uchaguzi huo.
Kufuatia yaliyojiri katika uchaguzo huo, vyama vya Chadema, TLP, AAFP na ACT Wazalendo vimepanga kuihitisha vikao vya ngazi ya juu ili kujadili mwenendo wa uchaguzi huo na kutoa msimamo wa vyama wa hivyo.
Akizungumza na Mwananchi leo, Novemba 28, 2024, Katibu wa AAFP, Rashid Rai amesema licha chama hicho kushinda uenyekiti na ujumbe katika Mkoa wa Morogoro, lakini uchaguzi huo haukuwa huru na haki.
“Uchaguzi haukuwa ‘fair’, sidhani kama watendaji wa chini wanazijua 4R za Rais Samia (ustahimilivu, mageuzi, kujenga upya na maridhiano) kwa sababu hatukuona kama zimetumika, kila sehemu kulikuwa na malalamiko.
“Kesho tutafanya tathmini kuangalia mwenendo wa uchaguzi huu, kisha tutatoa maazimio ya chama,” amesema Rai.
Kauli kama hiyo ilitolewa na Hashim Rungwe, mwenyekiti wa Chaumma, kuwa licha ya chama hicho, kuibuka kidedea katika mtaa mmoja mkoani Mbeya, uchaguzi huo ulikuwa na vituko na kasoro mbalimbali.
“Sijui hata nisemaje, nimefanikiwa kupata mtaa moja tena kwa mbinde. Haikuwa kazi rahisi, lakini uchaguzi huu ulikuwa na vituko. Malalamiko yetu ni yaleyale Tamisemi isisimamie uchaguzi huu, ili tuondokane na changamoto hizi,” amesema Rungwe, maarufu Mzee wa Ubwabwa.
Kwa upande wake Isihaka Mchinjita, makamu mwenyekiti wa ACT – Wazalendo-Bara, alidai uchaguzi huo haukuwa huru wala haki, ulijaa vitisho na matukio ya viongozi na wagombea wa upinzani kukamatwa na polisi.
“Kulikuwa na changamoto ya uwepo wa kura feki katika maeneo mbalimbali ikiwemo kijiji cha Mchinga 1 (Lindi) lakini pia mkoani Kigoma. Ikionekana umetoa taarifa fulani la kuzuia uhalifu, basi unaishia mikononi mwa polisi,” amesema.
“Tutakutana kamati ya uongozi ili kujadili mwenendo mzima wa uchaguzi huu, lakini tunarudia wito wetu kwamba mchakato kama huu, unapaswa kusimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC),” amesema.
Kauli ya kufanya tathmini pia ilitolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema, “kesho tutakuwa na kikao cha dharura cha kamati kuu, kitakachojadili na kutathmini mwenendo wa uchaguzi, kuazimia na tutatoa tamko la chama kwa umma.”
Mwingine waliozungumzia hali hiyo ni Katibu wa TLP, Richard Lyimo aliyesema bado anaendelea kukusanya taarifa kutoka maeneo mbalimbali kuhusu uchaguzi huo na kuwa watakutana kama chama kisha kutoa taarifa kwa umma.
Kwa upande wake Abdul Mluya, Katibu wa DP, licha ya kuungana na wenzake kusema haukuwa huru na haki na kuwa hawakufanikiwa kushinda kwa sababu ya figisu, alisema “uchaguzi hakuwa na vurugu, ulikwenda vizuri.”
“Lakini hatujafurahishwa na kitendo cha kupindua matokeo dakika za mwisho, watu walipiga kura mara mbili. Lazima sheria za uchaguzi wa serikali za mitaa zifanyiwe mapitio upya, ili kuondokana na changamoto hizi,” amesema Mluya.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kupitia tume yake ya amani, limelaani mauaji ya watu watatu kwenye mchakato wa uchaguzi huo huku likitaka kuona uwajibikaji wa Serikali katika kulinda uhai wa wanasiasa na raia.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya TEC, Askofu Mkuu Thadeus Ruwa’ichi amesema nchi inapita katika kipindi kigumu chenye machungu na maumivu makubwa, hasa inaposhuhudiwa raia wakikatishwa uhai wao wakati wakiwa katika kupigania haki zao za msingi za kisiasa.
Ruwa’ichi ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amesema wanasikitishwa na vitendo hivyo vya kutoa uhai wa watu hao.
“Tunalaani kwa uwezo wote mauaji haya na mengine yoyote yanayowagusa raia wa nchi hii. Tunalaani kwa sababu yanakusudiwa na wauaji. Tukumbuke Mungu ndiye mwenye mamlaka ya uhai wa wanadamu wote. Hapa duniani hakuna mwenye mamlaka ya kuondoa uhai wa mwingine
“Wajibu wetu ni kutetea, kulinda na kutunza uhai wa kila mwanadamu. Tunaonya jamii ya Watanzania kuacha hiyo tabia mbaya ambayo imeanza kujitokeza kwa kasi,” amesema Askofu Ruwa’ichi.
Askofu huyo amesema kutekeleza au kudai haki za kisiasa ni haki ya kila raia, na hilo likifanyika wakati wa uchaguzi, uwe wa serikali za mitaa au uchaguzi mkuu, siyo jambo la kuvunja sheria. Ameonya kuhusu uhalalishaji wa mauaji kwa sababu ya harakati za kisiasa zinazoendelea.
Amesisitiza Serikali inalo jukumu la kuonyesha kuzingatiwa kwa weledi katika hali iliyopo, watu wasijisikie kutishwa na vyombo vya ulinzi wakati wa maandalizi ya uchaguzi na wakati wa uchaguzi wenyewe.
“Ukatili dhidi ya wanasiasa na raia ni matendo maovu ambayo lazima yakomeshwe katika nchi yetu. Sisi sote ni ndugu na watoto wa Mungu muumbaji. Tuheshimu na kuzilinda amri za Mungu, hasa kulinda uhai wa mwingine,” amesisitiza Askofu Ruwa’ichi.
Katika mchakato wa uchaguzo, watu waliouawa ni pamoja na mgombea ujumbe Mtaa wa Ulongoni A jijini Dar es Salaam, Modestus Timbisimilwa, ambaye hata hivyo pilisi walisema amefariki kwa presha.
Mwingine ni aliyekuwa mgombea uenyekiti wa Kitongoji cha Stand katika Jimbo la Manyoni Mashariki mkoani Singida, George Mohamedi anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na askari Magereza.
Alipoulizwa kuhusu tukio la Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema mgombea huyo alifariki kwa kuugua presha na kinachosambazwa mitandaoni hakina ukweli.
Katika tukio la Singida, Polisi walisema wanamshikilia askari mmoja wa Magereza kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mgombea huyo.
Mkoani Songwe, siku ya kuamkia uchaguzi kilitokea kifo cha Stephano Mwambeje (23) Mkazi wa Chawa “A” Wilaya ya Momba Mkoa wa Songwe aliyekatwa na kitu chenye ncha kali.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limesema limkamata mwanaume mmoja mwendesha bodaboda kwa mahojiano zaidi kuhusu tukio hilo.
Mchambuzi wa siasa, Kiama Mwaimu amesema ili kuondokana na sintofahamu zinazojitokeza katika uchaguzi ni wakati mwafaka kwa mamlaka za Serikali kuendesha chaguzi hizo kwa uhuru, haki na uwazi.
Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe amesema kilichotokea katika mchakato huo, kilitarajiwa, ndio maana kwa hatua za mwanzo taasisi hiyo, ikishirikiano na wadau wengine walikimbilia mahakamani kupinga Tamisemi kusimamia uchaguzi huo, lakini hawakufanikiwa.
Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe amesema uchaguzi umekwisha, hivyo wanasubiri walioshindwa kama hawajiridhika kufuata taratibu za kisheria ikiwemo kwenda mahakamani, kama wana ushahidi.
Hata hivyo, Massawe amesema katika tukio la kidemokrasia kusikia mauaji halileti taswira nzuri, kwa sababu matarajio ya wananchi mchakato huo uende kwa amani na utulivu ili Watanzania kubaki salama.
“Unapokwenda katika uchaguzi halafu unapoteza maisha ni kitu kinachoumiza,” alisema aliongeza: Wale waliokataliwa au barua zao au viapo sio sahihi basi wameghushi, tulitarajia mamlaka zingine ziingilie kati kufanya uchunguzi,” amesema Massawe.
Katikati ya malalamiko hayo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Centre For International Policy (CIP), Omary Mjenga amesema uchaguzi ulitawaliwa na amani na utulivu na vituo vilifunguliwa mapema na Watanzania wengi walijitokeza kushiriki mchakato huo.
“Palipotokea changamoto zilirekebishwa na kura zilipigwa, lakini changamoto zingine zilizojitokeza zimekuwa fundisho kwa wasimamizi, kwamba katika uchaguzi ujao ukiwamo uchaguzi mkuu kuna mambo ya kuangalia.
“Nalipongeza Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi na usalama, uchaguzi huu ni tofauti na ule wa mwaka 2019, sasa hivi vyama vya upinzani vimepata ushindi katika maeneo viliyojiimarisha,” amesema Mjenga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Focus On Tanzania Organazations (Foto), ambalo pia lilikuwa waangalizi wa uchaguzi huo, Wallace Mayunga pia amesema mchakato huo ulikuwa huru na wenye usawa.
“Milango ilikuwa wazi, kulikuwa na uhuru wa kukusanyika, uhuru wa maoni na uhuru wa kupiga kura. Pia zilikuwepo kanuni na mifumo ya uchaguzi iliyowekwa ambayo haikuwa kinzani kwa mtu yeyote, ndio maana uchaguzi ulikuwa huru na wenye usawa,” amesema Mayunga.