Siha. Moto ambao chanzo chake kinadaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme, umeteketeza vibanda vitano vya biashara vinavyomilikiwa na Kanisa Katoliki, Mtaa wa Pongo uliopo katika Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk Christopher Timbuka amethibitisha kutokea ajali hiyo ya moto jana Novemba 27, 2024 alfajiri wakati vibanda hivyo vikiwa havina watu.
“Novemba 27, 2024, kuna vibanda vitano vya biashara ambavyo viliteketea kwa moto, moto huu unadaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme kwenye duka moja lililokuwa linasadikiwa kuwa na vifaa vilivyokuwa vinachajiwa,” amesema Dk Timbuka.
Dk Timbuka amesema hakuna madhara yoyote ya kibinadamu yaliyojitokeza zaidi ya uharibifu wa mali.
“Niwasihi wananchi, tuchukue tahadhari zote tunapotumia umeme kuhakikisha kuzima vifaa vya umeme inapofika majira ya usiku inapotokea dharura wasipate madhara,” ametoa rai hiyo Dk Timbuka.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji mkoani hapa, Jeremiah Mkomagi amesema chanzo cha moto huo bado kinachunguzwa na taarifa itatolewa rasmi.
“Baada ya kuripotiwa tukio hili tulifika eneo la tukio na kuweza kudhibiti moto ule kwa kiasi kikubwa na kati ya vibanda 18 vilivyokuwa katika eneo hilo vibanda, vitano vilikuwa vimeteketea kwa moto tayari,” amesema Kamanda Mkomagi.
Aidha, Kamanda Mkomagi amesema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo la moto ili kubaini chanzo chake.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Jones Kanje, ambaye pia ni dereva bajaji, amesema wakiwa kituo cha bajaji kilichopo karibu na eneo hilo walishangaa kuona mlipuko mkubwa wa moto ambao ulizua taharuki.