Mwenyekiti wa mtaa aliyedumu madarakani kwa miaka 30 achaguliwa tena

Morogoro. Mwenyekiti wa Mtaa wa Makaburi A, Kata ya Mji Mpya, Manispaa ya Morogoro kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM),  Hamis Lukinga maarufu kama ‘Mzee Kiuno’ (70) aliyehudumu kwenye uongozi huo kwa miaka 30 sawa na vipindi sita amechaguliwa tena kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano.

Akizungumza na Mwananchi Digital Lukinga amesema kwa mara ya kwanza aliingia madarakani mwaka 1994 ukiwa ni uchaguzi wa kwanza uliohusisha mfumo wa vyama vingi na tangu hapo aliendelea kuchaguliwa ndani ya chama hadi kwa wananchi wa mtaa huo.

Lukinga ametaja moja ya siri za ushindi wake ni uchapakazi unaowafanya wananchi wamkubali lakini pia uwazi kuwa kusaidia na kushirikiana na wananchi wake katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo.

“Hapa mtaani nimeweza kuwasaidia wananchi wenye shida mbalimbali na msaada huu siyo wa kifedha bali ushauri na kuwapa miongozo hasa pale wanapopata changamoto,” amesema Kukinga.

Siri nyingine anayoamini kuwa imempa ushindi ni jinsi ambavyo ameweza kuwasaidia wazazi waliokuwa wakishindwa kugharamia watoto wao masomo baada ya kufaulu na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza.

“Mimi sina uwezo wa kifedha wa kuwapa wananchi wangu lakini nilichokuwa nafanya nilikuwa nawaombea msaada kwa Mbunge Abdul Aziz Abood ambaye naye amekuwa akiwasaidia kuwapa fedha na mahitaji ya shule ya watoto wao,” amesema Lukinga.

Amesema pia kama mwenyekiti wa mtaa amekuwa akihakikisha maendeleo yanakuwepo mtaani hapo na pia changamoto zinatatuliwa kwa kushirikiana na wananchi lakini pia chama.

Lukinga amesema kuwa katika vipindi vyote vya uchaguzi amekuwa akipata upinzani ndani ya chama na hata baada ya kuteuliwa na chama ambapo kwa mwaka huu mgombea mwenzake kwenye kura za maoni ndani ya chama alipata kura 41 ambapo yeye alipata kura 64.

“Mwaka huu nilipanga kutogombea kabisa uenyekiti lakini viongozi wangu wa chama na wananchi walinifuata na kuniomba nigombee, ilibidi nichukue fomu na kugombea, nashukuru nimepita nimepata kura 508 huku watu waliojiandikisha na kupiga kura wakiwa 528.

Mwenyekiti huyo anayesubiri kuapishwa amesema uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa kwake ni wa mwisho kwa sababu hatagombea tena nafasi yoyote ndani ya chama huku akisema kuwa umri wake umeshakuwa mkubwa na hivyo ni lazima apishe na awaachie wengine.

“Nimepanga mwaka 2029 nisigombee tena uenyekiti kwanza nimeshakuwa mtu mzima, pili lazima nipishe waje watu wapya wataoendeleza haya ninayoyafanya sasa, hiki ndio kipindi changu cha mwisho nataka kustaafu nibaki kuwa mashauri tu japokuwa wananchi wa mtaa huu wanatamani niendelee kuongoza,” amesema Lukinga.

Akieleza nyakati ngumu alizopitia katika kipindi cha uongozi wake Lukinga amesema ni pamoja na changamoto aliyoipata mwaka jana baada ya baadhi ya watu wake wa karibu wakiwa ndugu kumtuhumu uchawi huku wakihusisha uchawi huo na ushindi wake anaoupata kila uchaguzi.

“Ila pamoja na uzushi huu bado wananchi wakiendelea kuniamini na kuniomba nigombee, mimi ni mwenyekiti ninayefanya kazi bila kubagua rangi, kabila wala itikadi ya kisiasa,” amesema Lukinga.

Kwa ipo mikakati mbalimbali aliyojiwekea katika kuleta maendeleo ya mtaa huo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wanawake wa mtaa huo kujiunga kwenye vikundi ili waweze kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri badala ya kukopa mikopo kandamizi maarufu kama ‘kausha damu.

“Kwenye mtaa wangu akina mama wengi wamejiingiza kwenye hii mikopo ya kausha damu na mingine inayofanana ya hii sasa changamoto inakuwa kubwa wengine wanashindwa kurejesha na kujikuta wakikimbia familia zao na kuwaacha watoto wanatangatanga na kuteseka mtaani,” amesema Lukinga.

Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo ameiomba Serikali kuweka utaratibu wa kuwalipa wenyeviti wa mitaa posho ya kujikimu ili waweze kurahisisha shughuli zao tofauti na ilivyokuwa sasa ambapo wenyeviti hawalipwi na wamekuwa wakitumia nyumba zao kama ofisi.

“Sisi wenyeviti hatuna mshahara, hatuna posho, hatuna ofisi, tunafanyakazi Kwa kujitolea tena katika mazingira magumu kiufupi sisi ndio watu wa kwanza kujua shida za wananchi hivyo tunaomba Serikali itutazame Kwa jicho la huruma walau tupate fedha za kujikimu ikiwa ni pamoja fedha za steshenari,” amesema Lukinga.

Kwa upande wake katibu wa chama cha Mapinduzi CCM kata ya mji mpya ,Mary Kunambi amesema chama kimepanga kuwapongeza wenyeviti wote walishinda uchaguzi kwenye kata hiyo na katika pongezi hizo mwenyekiti huyo Lukinga atapewa tuzo kwa kuhudumu katika uongozi kwa muda mrefu.

“Kwa sasa bado tunaendelea na vikao vya chama kwa ajili ya tathimini ya uchaguzi baadaye mamlaka husika itawaapisha na kuanza kazi hapo ndipo tutakapopanga siku ya kuwapongeza lakini kwa huyu Mzee Lukinga lazima tumpe kitu cha ziada amefanyakazi nzuri na amewatumikia wananchi kwa muda mrefu.

Baadhi ya wananchi wa mtaa huo wameeleza namna mwenyekiti huyo wanavyomkubali kutokana na utendaji kazi wake.

Danstan Damian ni mmoja wa wananchi wa mtaa huo amesema mwenyekiti huyo amekuwa akifanya kazi usiku na mchana na  mara zote amekuwa akitumia busara kwenye kufanya maamuzi.

Damian ameeleza moja ya kazi nzuri aliyofanya mwenyekiti huyo ni kuhamasisha wazazi na walezi kupeleka watoto wao shule hasa wale waliofikia umri wa kuanza darasa la kwaza.

“Kwa kweli tunatamani huyu mwenyekiti aendelee kutawala mpaka siku atakapokufa maana yuko bega Kwa bega na sisi wananchi wake.

Related Posts