Mwili wa Dk Ndugulile kuwasili Tanzania kesho, kuzikwa Desemba 3

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni (CCM) na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile anatarajiwa kuzikwa Jumanne ya Desemba 3, 2024 katika makaburi ya Mwongozo yaliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Rasimu ya ratiba ya mazishi ya marehemu Dk Ndugulile Novemba 29 hadi Desemba 3, 2024

Ratiba ya mazishi hayo iliyotolewa na Ofisi ya Bunge la Tanzania, imeonyesha mwili wa kiongozi huyo utawasili nchini kesho Novemba 29, 2024 ukitokea nchini India.

Mwili utawasili saa 6:35 mchana katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere Dar es Salaam kutokea India kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia na kupokewa na Naibu Spika, Mussa Zungu, wajumbe wa Tume, Katibu wa Bunge, wawakilishi wa Serikali na wawakilishi wa chama.

Baada ya mapokezi hayo, mwili utapelekwa kuhifadhiwa Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo. Pia ratiba inaonyesha Novemba 30 mpaka Desemba Mosi maombolezo yataendelea nyumbani kwake Kigamboni.

Desemba 2 mwili wa marehemu utaelekea Kanisa la Mtakatifu Immaculate – Upanga kwa ajili ya misa itakayoanza saa 1:30 mpaka saa 2:30 asubuhi kabla ya kuelekea Karimjee ambako utaagwa rasmi.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan atawaongoza viongozi na wageni mbalimbali kutoa heshima za mwisho katika viwanja vya Karimjee kabla ya mazishi hayo.

Mwili huo utawasili saa 4:00 asubuhi baada ya viongozi wote kuwasili na itafanyika misa takatifu kuanzia saa 4:10 asubuhi mpaka saa 4:20 asubuhi, ikifuatiwa na wasifu wa marehemu na salamu kutoka kwa viongozi mbalimbali.

Saa 4:35 kutakua na salamu za pole kutoka kwa viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa mpaka saa 5:30 kabla ya Rais Samia kuwaongoza viongozi na wageni mbalimbali kutoa heshima zao za mwisho.

Saa 8:30 mchana mwili wa marehemu utaelekea nyumbani kwake Kigamboni.

Desemba 3 saa 2:00 asubuhi mwili utapelekwa viwanja vya Machava kwa ajili ya wananchi kutoa heshima zao za mwisho kabla ya kupelekwa Kanisa la Bikira Maria Consolata kwa ajili ya Misa ya mazishi saa 8:00 mchana.

Kuanzia saa 9:00 alasiri msafara w amwili wa marehemu utaondoka kanisani kuelekea Makaburi ya Mwongozo kwa ajili ya maziko.

Dk Ndugulile alijiunga na siasa mwaka 2010 na amekuwa Mbunge wa Kigamboni jijini Dar es Salaam, Tanzania hadi mauti yake.

Alihudumu kama Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii na Maendeleo ya Jamii,  pia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ukimwi na Matumizi ya Dawa za Kulevya.

Aliongoza Kamati ya Ushauri ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kuhusu Ukimwi, Afya ya Mama na Mtoto yenye makao yake Geneva kati ya mwaka 2015 na 2017. Kati ya mwaka 2008 na 2016, Dk Ndugulile alikuwa mwanachama wa Baraza la Utawala la Jumuiya ya Kimataifa ya Ukimwi (International AIDS Society) yenye makao yake Geneva.

Aidha, Dk Ndugulile alikuwa mwanachama wa Bunge la Afrika (2015-2017), mwanachama wa Jumuiya ya Wataalamu wa Microbiolojia ya Marekani (ASM), Chama cha Afya ya Umma Tanzania (TPHA) kama Katibu Mkuu na baadaye Mwenyekiti wa Muungano wa Wabunge wa Tanzania wa Kupambana na Ukimwi (TAPAC).

Dk Ndugulile aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee kati ya mwaka 2017 na 2020.

Baada ya kuanzishwa kwa Wizara mpya ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Desemba 2020, Dk Ndugulile aliteuliwa kuwa Waziri wake wa kwanza.

Alichaguliwa kuwa Mkurugenzi kikanda wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO), katika kikao cha 74 cha Kamati ya Kanda ya Afrika ya WHO kilichofanyika nchini Congo Brazzaville Agosti 26 hadi Agosti 30, 2024 na alitarajiwa kumrithi Dk Matshidiso Moeti wa Botswana aliyemaliza muda wake.

Related Posts