Nswanzurimo aanza kwa kichapo Singida BS, Azam FC ikishinda

KAIMU Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Ramadhan Nswanzurimo ameanza vibaya majukumu yake ndani ya kikosi hicho baada ya timu hiyo kupoteza kwa mabao 2-1, dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Azam Complex.

Kocha huyo alitangazwa Novemba 25, mwaka huu kuongoza timu hiyo baada ya Kocha Mkuu, Patrick Aussems na msaidizi wake Denis Kitambi kusimamishwa kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo ambayo kikosi hicho imeyapata katika Ligi Kuu Bara.

Hatua ya kusimamishwa kazi kwa Aussems na kibarua chake kupewa Nswanzurimo, ilijiri muda mfupi tu baada ya kikosi hicho kutoka sare ya mabao 2-2, dhidi ya Tabora United mchezo uliopigwa Novemba 25, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.

Katika mchezo wa leo, mabao ya Azam FC yamefungwa na kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ dakika ya 38 huku la pili likifungwa na mshambuliaji Mkolombia, Jhonier Blanco dakika ya 56, baada ya wote kupokea pasi safi kutoka kwa Idd Seleman ‘Nado’.

Bao la Feisal Salum linakuwa  la tatu kwake msimu huu katika Ligi Kuu Bara huku kwa upande wa mshambuliaji wa nyota wa kikosi hicho, Jhonier Blanco akifikisha la pili tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Aguilas Doradas ya kwao Colombia.

Kwa upande wa bao la kufutia machozi kwa upande wa Singida Black Stars limefungwa na mshambuliaji Mkenya, Elvis Rupia dakika ya 62 akipokea pasi ya kiungo, Josaphat Arthur Bada na kufikisha bao lake la tano msimu huu katika Ligi Kuu Bara.

Ushindi kwa Azam FC unakifanya kikosi hicho kufikisha jumla ya michezo saba mfululizo ya Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza tangu mara ya mwisho ilipofungwa mabao 2-0, dhidi ya Simba, mechi iliyochezwa Septemba 26, Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar.

Tangu Kocha, Rachid Taoussi ateuliwe kuiongoza Azam FC Septemba 7, mwaka huu akichukua nafasi ya Msenegali, Yousouph Dabo, ameiongoza timu hiyo katika michezo 11 ya Ligi Kuu Bara, ambapo ameshinda minane, sare miwili na kupoteza mmoja.

Kiujumla Azam FC imecheza michezo 12, ya Ligi Kuu Bara msimu huu, ikishinda minane, sare mitatu na kupoteza mmoja hadi sasa, ambapo kikosi hicho kimefunga jumla ya mabao 16 na kuruhusu manne tu, kikiwa nafasi ya pili na pointi zake 27.

Kwa upande wa Singida katika michezo 12 iliyocheza imeshinda saba, sare mitatu na kupoteza miwili ikiwa nafasi ya nne na pointi zake 24, ambapo kikosi hicho kimefunga jumla ya mabao 16 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane hadi sasa.

Related Posts