POLISI KATA SERENGETI AMSAIDIA MTOTO KITI MWENDO BAADA YA KULALA KITANDANI KWA MIAKA 16

 

Polisi wa Kata ya Ikoma, Tarafa ya Grumet, Wilaya ya Serengeti, Mkoa wa Mara, CPL Emmanuel Mwikwabe, amemkabidhi kiti mwendo mtoto Vaileth Enock (16), mwenye ulemavu wa kuzaliwa uliosababisha kupooza mwili wake.

CPL Mwikwabe aligundua hali ya mtoto huyo kupitia kampeni ya utoaji wa elimu ya polisi jamii kwa mfumo wa nyumba kwa nyumba katika Kijiji cha Parknyigoti, Kitongoji cha Park B. Hapo alikutana na mzazi wa mtoto huyo, Mzee Enock Komanya, na kugundua changamoto kubwa anayokabiliana nayo binti huyo.

“Nilipofika nyumbani kwa Mzee Enock Komanya, nilikuta watoto, akiwemo Vaileth, ambaye hali yake ilinigusa sana. Nikaamua kumshirikisha Mkuu wa Wilaya, Bi. Kemirembe, ambaye alikubali kunisaidia kupata kiti mwendo,” alisema CPL Mwikwabe.

Baada ya kukabidhi kiti hicho, CPL Mwikwabe alisema kuwa hatua hiyo inalenga kumpa faraja Vaileth, ambaye amekuwa akilazimika kulala kitandani muda wote kutokana na kukosa kiti mwendo.

Aidha, CPL Mwikwabe amewataka wazazi na wakazi wa Kata hiyo kuacha kuwabagua watoto wenye ulemavu, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni ukatili wa kijamii. Aliongeza kuwa ni jukumu la jamii kuwasaidia watoto wenye changamoto kama hizo ili waweze kuishi kwa heshima na kupata nafasi sawa na wengine.  

Related Posts