Jeshi la Polisi limesema taarifa ya kukamatwa mgombea wa Mtaa wa Miembeni Kilimahewa kupitia Chadema mkoani Katavi na ile ya kuvunjwa mkono Herman Mzee na diwani wa CCM ni za kutengenezwa na zimeongezewa chumvi.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Novemba 28, 2024 kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na msemaji wa jeshi hilo, David Misime.
Pia, taarifa nyingine ambayo Polisi imefanyia uchunguzi ni gari ndogo iliyotaka kumteka Christopher Kapaso aliyekuwa anagombea nafasi ya uenyekiti Mtaa wa Kigamboni.
“Baada ya ufuatiliaji huo sambamba na kuchukua maelezo ya watu mbalimbali, imebainika taarifa hizo ni za kutengeneza na kuongeza chumvi ili kudanganya na kupata huruma ya wananchi.
“Ukweli uliopo kulingana na watu walioshuhudia ni kwamba Nsagigwa Mwandembwa, mgombea uenyekiti Mtaa wa Miembeni Kilimahewa alikuwa akifanya fujo kwenye kituo cha kupigia kura cha Miembeni na alionywa mara kadhaa lakini hakusikia.
“Baada ya kufikia hatua ambayo haivumiliki tena alikamatwa akiwa kwenye hicho kituo na kupelekwa kituo cha Polisi na kuhojiwa na baada ya mahojiano na alipoona yeye mwenye athari ya vitendo vyake alidhaminiwa ili akakamilishe taratibu zake za uchaguzi kusubiri hatua zingine za kisheria,”amesema Misime.
Misime ameongeza: “Kuhusu Mzee kupigwa na diwani wa CCM hadi kuvunjwa mkono, ufuatiliaji wa kina umefanyika na imebainika kuwa, kilichokuwepo ni mzozo baina yao kulikosababisha kuchaniana shati na wala hajavunjwa mkono kama mwenyekiti huyo anavyodanganya kwani mtu huyo leo amesafiri kutokà kijijini anakoishi na amewasili Mpanda Mjini mchana huu na kuelekea ofisi ya Chadema Mkoa wa Katavi kwenye kikao na baada ya kikao hicho wakati wowote ule Mwenyekiti huyo wa Chadema ataongea na waandishi wa habari.”
Pia, Misime ameongeza kuwa, kuhusu taarifa ya kuwapo kwa jaribio la kumteka, Christopher Kapaso, habari hizo zimefuatiliwa na hazina ukweli wowote.