PROF. NOMBO AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA MAWAZIRI WA SAYANSI YA NYUKLIA NA TEKNOLOJIA VIENNA AUSTRIA

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo aongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Sayansi ya nyuklia na Teknolojia wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) unaofanyika jijini Vienna Austria kuanzia tarehe 26-28 Novemba,2024.

Katika Mkutano huo ambao anamwakilisha Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda Prof. Nombo ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Austria Mhe. Naimi Aziz na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Nguvu za Atomiki Nchini, Prof. Malilio Kipanyula.

Akizungumza katika Mkutano huo, Prof. Nombo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama pamoja na Taasisi ya IAEA kupitia matumizi salama ya nyuklia katika kuleta maendeleo hususan kwenye sekta za afya, chakula, kilimo, maji mazingira na mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo ya viwanda.

Prof. Nombo alikitaarifu Kikao hicho juu ya matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini na kutoa tathmini ya matumizi salama ya teknolojia ya Nyuklia katika utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Prof. Nombo ameishukuru IAEA kwa ushirikiano mkubwa inaoutoa kwa Tanzania na kuihakikishia utayari wa Tanzania kuendelea kushirikiana na IAEA.

Mkutano huo umeitishwa kujadili masuala mahsusi yanayohusu sayansi ya nyuklia na matumizi yake.

Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo umepitisha Tamko la Mawaziri Juu ya Sayansi ya Nyuklia, Teknolojia na Mtumizi yake na Mpango wa Mashirikiano ya Kitaalam (The Ministerial Declaration on Nuclear Science, Technology and Applications and Technical Cooperation Programme).

Related Posts