Monduli. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewatunuku Kamisheni maofisa wanafunzi 236 wa Jeshi katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi (TMA)- Monduli, mkoani Arusha.
Maofisa hao wapya wamekuwa maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wengine waliohitimu ni kutoka nje ya nchi.
Tukio hilo limefanyika leo Alhamisi Novemba 28, 2024, TMA Monduli mkoani Arusha.
Kabla ya kutunuku kamisheni, Rais Samia ambaye pia ni Amri Jeshi Mkuu, amekagua gwaride lililoandaliwa na maofisa hao wahitimu.
Aidha, Rais Samia ametoa zawadi kwa wahitimu waliofanya vizuri katika makundi yote.
Waliopewa zawadi katika kundi la 05/21 ni Cloud Ndaiga aliyefanya vizuri katika fani zote kwa ujumla, aliyefanya vizuri katika taaluma ni Exavery Lazaro na katika medani ni Kelvin Tarimo.
Katika kundi la 71/23 aliyefanya vizuri katika fani zote ni John Bahati, kwenye taaluma ni Charles Kashindye, katika medani Apha Gustav na aliyefanya vizuri kutoka nchi rafiki ni Thabo Masuku kutoka Eswatini.
Awali, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amesema mafunzo ya sayansi ya kijeshi ni muhimu kwa jeshi na Taifa kwa ujumla.
“Umuhimu wa mafunzo haya unajidhihirisha kwenye umahiri wa jeshi letu katika kutimiza majukumu yake kwa ufanisi, mafunzo haya huwajengea uwezo kutekeleza operesheni za kijeshi kwa ustadi mkubwa na huwaandaa kuwa viongozi wenye maadili, nidhamu na weledi wa kuongoza vikosi vya jeshi,” amesema.
“Kitaifa mafunzo haya huhakikisha jeshi linapata viongozi wazalendo na wenye uwezo wa kulinda mipaka ya nchi na kukabiliana na vitisho vya ndani na nje ya nchi. Yanajenga jeshi imara na Taifa lenye uwezo wa kudumisha amani, usalama na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” amesema Waziri Tax
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha TMA Monduli, Meja Jenerali Jackson Mwaseba aliwataka wahitimu hao kutambua kuwa jeshi na taifa vimewekeza fedha na rasilimali nyingi kwao kuhakikisha wanapata elimu bora kwa ajili yao binafsi, jeshi na taifa kwa ujumla.
“Taifa linahitaji wasomi walio na uzalendo, nidhamu na maadili mema ambao wataingia kuijenga nchi yetu kwa misingi endelevu, hivyo wahitimu mna dhamana kubwa ya kutumia taaluma zenu katika kutimiza wajibu wenu,” amesema.