WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara ikiendelea leo, tayari tumeshuhudia mabao 177 yakifungwa baada ya kuchezwa raundi 12, lakini kuna kitu kimeonekana kutokuwa sawa.
Licha ya kwamba mabao pia yamefungwa machache kulinganisha msimu uliopita hadi kufikia raundi hiyo, lakini pia safari hii hakuna hat trick.
Msimu uliopita kipindi kama hiki yalifungwa mabao 224 huku kukiwa na hat trick nne kupitia Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam dhidi ya Tabora United, Jean Baleke akiwa Simba dhidi ya Coastal Union, Stephane Aziz Ki wa Yanga dhidi ya Azam FC na Kipre Jr wa Azam aliyefunga dhidi ya Mtibwa Sugar.
Kocha wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Charles Mkwasa alisema hali hiyo inatokea kwa sababu wachezaji wetu wamekuwa na viwango vya kupanda na kushuka.
“Wachezaji wetu bado viwango vyao ni vya kupanda na kushuka, hawana mwendelezo wa moja kwa moja. hii ni ishara mbaya, ukiangalia wachezaji wote ambao walifanya vizuri msimu uliopita eneo la ushambuliaji msimu huu wameanza vibaya, hii inaweza kuwa sababu mojawapo,” alisema Mkwasa ambaye hivi sasa anakionoa kikosi cha Timu ya Taifa ya Vijana Wanaume chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes iliyofuzu Afcon U20 mwakani.
Kocha huyo aliongeza kwa kusema kwamba pia walinzi wanatakiwa kupewa heshima yao kwani wameweza kuwadhibiti wachezaji ambao wamekuwa wakisababisha madhara langoni mwao hivyo sifa ziende kwao pia bila kuangalia upande mmoja.
Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda, alisema ushindani umekuwa mkali, washambuliaji wanataka kufunga lakini pia walinzi wapo imara katika kuzuia jambo linaloongeza ubora wa ligi msimu hadi msimu kwani timu hazitaki kurudia makosa.
“Kwa mtazamo wangu ninadhani ubora umekuwa mkubwa kwa makipa na mabeki tusiangalie mapungufu ya washambuliaji tu, pia timu nyingi zimefanya usajili mzuri kwa lengo la kupunguza makosa waliyoyafanya msimu uliopita,” alisema na kuongeza.
“Ni mapema sana naamini kutakuwa na hat trick na zinaweza zisiwepo kama walinzi wataendelea kuwa imara na washambuliaji watakubali kuwa msimu umekuwa mgumu kwao.”
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ ambaye ana rekodi ya kufunga mabao 26 katika msimu mmoja wa ligi inayoishi hadi sasa tangu alipofanya hivyo mwaka mwaka 1999, alisifu ushindani wa ligi, huku akiwahamasisha washambuliaji kufanya kazi zao kwa usahihi kwa kutumia nafasi wanazotengeneza lakini pia mabeki wafanye kazi yao ili kuendelea kuikuza ligi.
Kwa sasa kinara wa mabao ni Seleman Mwalimu wa Fountain Gate aliyefunga sita akifuatiwa na Jean Charles Ahoua wa Simba mwenye matano, huku Edgar William (Fountain Gate), Peter Lwasa (Kagera Sugar), Paul Peter (Dodoma Jiji) na Elvis Rupia (Singida BS) kila mmoja akiwa na matatu.