Arusha. Kuna nyakati ni ngumu kutambua ubaya wa jambo linalofanyika kwa wakati huo kutokana na madhara yake kuchukua muda mrefu.
Hali hii huwafika kina mama wa jamii ya Kimasai waliokeketwa miaka mingi nyuma. Awali jambo hilo lilionekana fahari ndani ya jamii lakini baadaye maumivu na majuto hutawala kwa waliofanyiwa vitendo hivyo.
Kwa Mary Laiser, mmoja wa waliokeketwa akiwa mdogo, majuto, kutofurahia tendo la ndoa, maumivu wakati wa kujifungua ni vitu ambavyo vilimfanya kusimama kupinga utamaduni huu ili watu wengine wasiathiriwe.
Mary mzaliwa wa Kijiji cha Namanga wilayani Longido, ni mama wa watoto watatu, kati ya hao mmoja ni wa kike.
Alipitia tohara iliyoonekana kitu cha kawaida cha kuvuka rika kutoka utoto kwenda utu uzima.
Awali, shughuli ya tohara ambayo ni ukeketaji ulikuwa ukipangwa kwa uwazi na sherehe ilifanyika, huku watoto wakitaarifiwa muda watakaokeketwa.
Anakumbuka siku waliyokeketwa walikuwa watatu na walifanyiwa sherehe.
Mary anasema walikalishwa kwenye vigoda vya miguu mitatu ndani ya nyumba yao, alishikwa mgongoni na mtu ambaye pia alikaa kwenye kigoda.
“Tulikeketwa na ngariba mmoja, siwezi kukumbuka kama wembe uliotumika ulikuwa mmoja au tofauti,” anasema.
Anaeleza maumivu yalikuwa makali na hakuna dawa waliyopewa, zaidi ya kufarijiwa na mama yake.
“Kuna wakati tulipata maumivu tukiwa kitandani tunalia, mama akatuambia msiogope mbuzi akiachiwa kwenda malishoni uchungu utapoa. Alisema mnapata maumivu makali kwa sababu mbuzi anacheua anaendelea kutafuna, kufanya hivyo kunawafanya kuwa na maumivu,” anaeleza.
Kwa mujibu wa Mary, waliamini kauli hiyo na hata walipoulizwa iwapo maumivu yamepungua waliitikia licha ya kuwa haikuwa kweli.
Anasema alikeketwa akiwa kidato cha pili na umri wa miaka 14. Wakati hilo likifanyika alikuwa likizo.
Mary anasema msichana anapokeketwa hupewa vyakula ambavyo kwa kawaida hawapewi vikiwamo maziwa, supu, nyama choma na hunywa mafuta wakielezwa hupunguza maumivu na kuponyesha jeraha mapema.
Kupitia lishe hiyo anasema alinawiri wenzake wakamshangaa baada ya kurudi shuleni.
Kupitia wanafunzi wenzake wa mikoa ambayo haifanyi ukeketaji anasema walizungumzia madhara ya kitendo hicho lakini tayari alishakeketwa.
Alipomaliza kidato cha nne anasema alikaa nyumbani kusubiri matokeo ambayo hakufanya vizuri, pia kutokana na mwamko mdogo wa elimu kwa jamii ya Kimasai aliishia kuolewa.
Anasema hakufurahia tendo la ndoa na alipopata mtoto wa pili alimuuliza mama yake:
“Mbona mimi sifurahii tendo hili, akaniambia wanawake wote duniani hawajawahi kufurahia tendo la ndoa, tendo hili ni kwa ajili ya wanaume tu, sisi wanawake huwa hatufurahii lakini cha kukusaidia ukishaoga usiku hakikisha unapaka mafuta ya mgando sehemu za siri.”
Anasema hali hiyo ilimsaidia kuondokana na ukavu kwa kiasi, lakini pale anapokuwa hajajiandaa aliendelea kupata maumivu.
Anasema kutokana na maumivu wakati wa tendo hilo alishindwa kuvumilia hivyo ndoa yao ilivunjika naye akarudi nyumbani aliokoendelea na kazi mbalimbali ili kutunza watoto.
Mary anasema miongoni mwa kazi alizofanya ni mhudumu wa baa, jamii ikimshangaa kwa nini anafanya shughuli hiyo.
Anaeleza baadaye alipelekwa Shirika la World Vision alikoanza na kazi ya kutunza mabweni ya wageni lakini kutokana na uwezo wake wa kuzungumza, akafanya shughuli ya kupokea wageni.
Anasema akiwa kazini kwake, alipokea wageni kutoka Rwanda akatakiwa awaeleze ukeketaji ni nini.
Kwa mujibu wa Mary, aliwaeleza na hapo ukawa mwanzo wa yeye kubadilishiwa kazi, hasa baada ya wageni kuacha fedha kwa ajili ya utoaji elimu ya ukeketaji kwa jamii.
“Nikawa nimetoka kwenye kutunza mabweni nikajikuta nimepata kazi ya kuelimisha kwa njia hiyo, sikuwa na elimu bali nilikuwa natoa ushuhuda. World Vision waliona ipo haja ya kutufundisha, walitupeleka kwenye masomo zaidi na walituletea wataalamu kutoka hospitali tofauti kutufundisha,” anasema.
Mary anasema akiwa katika masomo alipata majibu ya maswali ya madhara ya ukeketaji.
Anaeleza alikumbuka alipopata mtoto wa kwanza mkwe wake alimuambia namna uchungu wa kujifungua ulivyo na kumtaka akihisi uchungu amuambie ili azalishwe nyumbani kwani akipelekwa hospitali atakatwa na mkasi jambo ambalo hawataki.
“Baadaye darasani nikasikia ukeketaji unachangia kuzaa kwa changamoto, kwani njia ya uzazi haitafunguka kama inavyotakiwa, ndipo nikakumbuka mama mkwe aliniambia nijitahidi nizae nyumbani kuliko hospitali ambako wangeniongezea njia na maumivu yangekuwa makali zaidi kuliko ambavyo angenichana mwenyewe,” anasimulia.
Anasema alizalishwa nyumbani na mpangaji wao ambaye alikuwa muuguzi, aliyemsaidia kujifungua salama licha ya kumuongezea njia.
Anaeleza alifanya kazi World Vision mwaka 2000 hadi mwaka 2006. Akiwa kazini anasema kuna siku alipokea wageni kutoka Canada ambao wakati anawahudumia alizungumza nao kuhusu ukeketaji.
Anasema wageni hao walitamani kuanzisha shirika, hilo likaanzishwa la Tanzania Education And Micro Business Opportunity (Tembo).
Katika shirika hilo anasema alikuwa mhamasishaji aliyezunguka maeneo mbalimbali kutoa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji.
Mnufaika wa kwanza wa masomo hayo anasema ni binti yake aliyedhamiria kumvusha rika bila kumkeketa.
Anasema alianza kumfunza akiwa darasa la nne na alipofika la sita alivushwa rika bila kukeketwa, huku baba wa binti huyo na mama mkwe wake wakiunga mkono suala hilo.
Mary anasema aliyekuwa mume wake ambaye humshirikisha mambo kuhusu watoto alipokea somo hilo kwa urahisi kutokana na kuona adha aliyopitia.
“Mtu wa pili kukubali hili alikuwa mama mkwe wangu, Kimasai mama mkwe ana nguvu na watoto wa kijana wake. Mama yangu alikuwa mpingaji wa ukeketaji,” anasema.
Mary anasema hatua ya kumvusha mwanawe rika bila kumkeketa ilivuta hisia za wengi, wakiwamo viongozi wa kisiasa na Serikali.
Kwa miaka 17 aliyofanya kazi na shirika la Tembo, anasema amewafundisha wengi wakiwamo wanafunzi wa shule za msingi wilayani Longido.
Kutokana na mafunzo hayo, Rahel Jonathan, anajivunia kumvusha rika binti yake wa kwanza bila kumkeketa.
Ameweka nadhiri kwamba wengine watatu waliobaki atawavusha rika bila kuwakeketa kwa sababu amefahamu madhara yake.
“Nilikuwa sijui madhara ya ukeketaji, nilipofahamu nilipinga ukeketaji kwa binti yangu, watu walizungumza sana hadi baadhi wakaanza kunichukia. Msichana wangu ni wa kwanza kuvushwa rika bila kukeketwa katika boma letu,” anasema.
Paul Tejeni, baba na kiongozi wa mila anasema alishadhamiria kutowakeketa watoto wake na kwamba elimu imempa mafunzo zaidi.
“Ukeketaji ulifanya mtoto wa kaka yangu afariki dunia, tangu hapo nilisema nikioa sitakeketa mtoto wangu, nilipitia misukosuko, kutengwa na jamii kuonekana nimekengeuka kutoka mila na desturi, nimepotea lakini sikujali na nilipokutana na shirika hili, liliniongezea nguvu na hakuna mwanangu aliyekeketwa,” anasema.
Pamoja na jitihada zinazofanyika, ukeketaji bado unafanyika kwa siri jambo ambalo Mary anatamani waelimishaji wawe wengi.
“Siyo kila siku jamii inione mimi tu, wakiona leo kaja huyu, kesho huyu, keshokutwa huyu wataogopa kwa kuona sasa wanachokifanya si sahihi. Pia natamani mitalaa ya shule ibadilishwe na iongezwe somo la madhara ya ukeketaji kuanzia shule za awali, msingi na sekondari,” anasema.
Anasema ni vyema waliokeketwa wakajitokeza kuzungumzia madhara yake ili watu wajue.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation