Wacheza gofu wa timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania wamepania kuianza vyema raundi ya kwanza ya michuano ya gofu ya Afrika inayoanza rasmi leo baada kukamilika kwa mazoezi ya siku tatu katika viwanja vya klabu ya Taghazout mjini Agadir Morocco.
Timu hiyo iliyowasili mwishoni mwa juma nchini Morocco, ilishiriki katika zoezi la siku tatu la kuvifanyia mazoezi viwanja vya klabu ya Taghazout ili kujiweka sawa kwa ajili ya mashindano yanayoanza rasmi leo siku ya Alhamisi, kwa mujibu wa ratiba za mashindano haya.
“ Tumefanya mazezi ya kutosha katika viwanja hivi na tuna matumani ya kufanya vizuri katika raundi ya kwanza siku inayonza kesho,Alhamisi,” alisema Madina Iddi, mmoja wa wachezaji tegemeo wa timu ya Tanzania.
Mashindano haya yanayoshirikisha wachezaji nyota wa kike kutoka nchi zote za bara la Afrika, yatafika tamati siku ya Jumamosi ambapo jumla ya 54 yatachezwa.
Tanzania imepeleka kikosi cha wachezaji watatu na viongozi wawili katika mashindano haya.
Wachezaji wengine ni Neema Olomi kitoka klabu ya Arusha Gymkhana na Hawa Wanyeche kutoka klabu ya Lugalo, ambaye pia ndiye nahodha wa timu.
Viongozi wa timu ni katibu a chama cha gofu ya wanawake nchini(TLGU), Yasmin Challi na Ayne Magombe ambaye ni meneja wa timu.
Kwa kila raundi, kwa mujibu wa kanuni za mashindano, alama bora kutoka kwa wachezaji wawili ndizo zitahesabiwa wakati mchezaji wa tatu atakuwa ni wa akiba.
“Tumevifanyia mazoezi ya kina viwanja vyote 18 kwa muda wa siku tatu. Naamini havitatupa taabu,” alimaliza Madina.
Michuano hii ambyo imepangwa kuanza rasmi leo, Novemba 28, itachezwa katika viwanja vya Klabu ya Taghazout mjini Agadir nchini Morocco.
Wachezaji wote watatu wana uzoefu mkubwa katika michuano ya kimataifa.
Wachezaji hawa, kwa mujibu wa takwimu, waliiwezesha Tanzaania kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki katika michuano iliyofanyika mwaka jana mjini Kigali, Rwanda.
Licha ya michuano hii, Madina Iddi aliweza kutwaa ubingwa wa wanawake katika nchi za Ghana, Zambia na Uganda wakati Olomi na Wanyeche pia walifanya vizuri katika mashindano ya kimataifa nchini Kenya na Uganda.