VIDEO: CCM yakomba mitaa, vitongoji na vijiji, Chadema, ACT-Wazalendo…

Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka kidedea katika nafasi zote zilizowania katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa zaidi ya asilimia 95 huku Chadema na ACT-Wazalendo zikikifuatia.

Matokeo hayo yametangazwa usiku wa jana Alhamisi Novemba 28, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Akisoma matokeo ya nafasi ya uenyekiti wa kijiji, Mchengerwa amesema;“kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji ni 12,271 kati ya nafasi 12,280 zilizopaswa kufanya uchaguzi. Kati ya nafasi hizo, CCM imeshinda nafasi 12,150 sawa na asilimia 99.01, Chadema imeshinda nafasi 97 sawa na asilimia 0.79, ACT Wazalendo imeshinda nafasi 11 sawa na asilimia 0.09, CUF imeshinda nafasi 10 sawa na asilimia 0.08.

“NCCR Mageuzi imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.01, UMD imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.01 na ADC imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.01,”amesema na kuongeza.


CCM yakomba mitaa, vijiji na vitongoji uchaguzi serikali za mitaa

Kwa upande wa wajumbe wa halmashauri ya kijiji, waziri huyo mwenye dhamana ya usimamizi wa uchaguzi huo amesema; “matokeo ya nafasi za wajumbe wa halmashauri za vijiji CCM imeshinda nafasi 229,075 sawa na asilimia 99.31, Chadema nafasi 1,222 sawa na asilimia 0.53.

ACT Wazalendo imeshinda nafasi 232 sawa na asilimia 0.1, CUF imeshinda nafasi 105 sawa na asilimia 0.05, NCCR – Mageuzi imeshinda nafasi 16 sawa na asilimia 0.01.”

“Demokrasia Makini imeshinda nafasi 3 sawa na asilimia 0.001, NLD imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.0004 na ADC imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.0004,” amesema.

Kwa nafasi ya uenyekiti wa kitongoji CCM imeongoza kwa asilimia 98.26 huku ikifautiwa na Chadema iliyoambulia asilimia 1.34.

“Maeneo yaliyofanya uchaguzi Novemba 27, 2024 kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Kitongoji ni 63,849 kati ya nafasi 63,886 zilizopaswa kufanya uchaguzi. Kati ya nafasi hizo, CCM imeshinda nafasi 62,728 sawa na asilimia 98.26, Chadema imeshinda nafasi 853 sawa na asilimia 1.34.

“ACT Wazalendo imeshinda nafasi 150 sawa na asilimia 0.23, CUF imeshinda nafasi 78 sawa na asilimia 0.12, NCCR -Mageuzi imeshinda nafasi 10 sawa na asilimia 0.02.

UDP imeshinda nafasi 6 sawa na asilimia 0.01, UMD imeshinda nafasi 2 sawa na asilimia 0.003 na ADC imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.002,” amesema.

Waziri Mchengerwa amesema kwa upande wa wajumbe wa mitaa, CCM imeshinda kwa asilimia 99.3, Chadema asilimia 0.47 na ACT-Wazalendo imepata asilimia  0.14.

“Matokeo ya nafasi za wajumbe wa kamati ya mtaa CCM imeshinda nafasi 21,148 sawa na asilimia 99.3, Chadema imeshinda nafasi 101 sawa na asilimia 0.47, ACT Wazalendo imeshinda nafasi 29 sawa na asilimia 0.14, CUF imeshinda nafasi 16 sawa na asilimia 0.08.

NCCR -Mageuzi imeshinda nafasi 2 sawa na asilimia 0.01, CCK imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.005 na ADC imeshinda nafasi 1 sawa na asilimia 0.005,” amesema Mchengerwa.

Wagombea waliofariki, uchaguzi kurudiwa

Waziri Mchengerwa amesema vitongoji 37 havikufanya uchaguzi  Novemba 27, 2024, kati ya hivyo, vitongoji vinane havikufanya uchaguzi kwa kuwa wagombea wake walifariki dunia baada ya shughuli ya uteuzi kufanyika.

“Wagombea hao walitoka katika Halmashauri za Wilaya za Kilwa (2), Nanyumbu (1), Itilima (1), Ikungi (1), Manyoni (1), Uyui (1) na Mbarali (1). Aidha, vitongoji 29 havikufanya uchaguzi kutokana na sababu mbalimbali.

“Vitongoji 12 vitarudia uchaguzi kwa kuwa matokeo ya wagombea yalifungana. Vilevile, vitongoji tisa vitarudia uchaguzi kutokana na wagombea pekee kutopata kura za kutosheleza,” amesema na kuongeza.

Related Posts