Wakati wa kupanga usisahau mipango midogo ya kifedha

Mzee Hamisi alikuwa mwajiriwa katika wizara moja nyeti ya Serikali. Akiwa mtumishi mwandamizi na mkuu wa kitengo, mzee Hamisi alikuwa na kipato ambacho si haba.

Maisha yalikuwa ni mazuri kwake na familia yake. Mwaka 2019, Mzee Hamisi akiwa amebakiza mwaka mmoja kabla ya kustaafu, akaamua kujiandaa na maisha baada ya ajira.

Baada ya kufikiria kwa muda mrefu, akaamua kujiandaa kufanya biashara ya utalii. Kama mkakati wa kuandaa biashara hiyo, akanunua magari mawili aina ya Landcruiser kama kianzio kwa kampuni kubebea abiria. Baada ya kustaafu mzee Hamisi akaanza taratibu za kusajili kampuni ya utalii.

Akiwa katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa kampuni yake, akapata taarifa mbaya. Taarifa ya ajali. Kijana wake, ambaye ndiye mwanaye pekee ambaye alitegemea kuwa msimamizi wa kampuni hiyo ya utalii, alikuwa amepata ajali na moja ya magari yaliyonunuliwa kwa ajili ya kampuni.

Kijana wake aliumia vibaya uti wa mgongo. Na kwa upande wa gari, lilipondeka ovyo. Na kwa kuwa gari bado lilikuwa limepaki nyumbani, MzeeHamisi alikuwa bado hajalikatia bima kubwa, hivyo hakuna kitu atakachoweza kupata kutoka katika gari lile.

Mzee Hamisi akaachana na masuala ya kampuni na kuanza kumfanyia matibabu kijana wake. Kwa kuwa mke wake alishafariki miaka mingi iliyopita, mzee alitakiwa kwenda hospitali na kijana wake kila siku yeye mwenyewe. Alitakiwa kwenda na kijana wake India kwa ajili ya upasuaji ambapo kiasi kikubwa cha pesa yake ya kiinua mgongo ilitumika katika safari na matibabu. Matibabu ya kijana yalikuwa makubwa na mpaka mwaka mzima unaisha alikuwa hajatengamaa kabisa. Mzee alimaliza kiinua mgongo chote. Baadaye akaamua kuuza gari lililobaki ili kuendelea na matibabu ya kijana wake.

Kijana alikuwa ni mtu wa kusogezwa na kurudishwa. Kutokana na hali ya kijana wake, mzee Hamisi alitakiwa kumpeleka kila wiki hospitali kwa ajili ya mazoezi. Gharama za mazoezi na madawa kwa kila wiki ilikuwa ni Sh250,000.

Mzee Hamisi aliachana na wazo la biashara, na pesa yote kutumika kwenye matibabu. Hili linaweza kumpata mtu yeyote. Ndiyo maana wataalamuwanakushauri kuwa ukiwa na mipango ya biashara na uwekezaji usisahau mipango midogo kama bima ya afya na kuwa na akiba kwa ajili ya dharura.

Hii itakusaidia kutochukua akiba uliyoweka kwa ajili ya uwekezaji na kukusaidia kutatua changamoto kama alivyofanya mzee Hamis.

Related Posts